ANGALIA LIVE NEWS

Monday, May 9, 2016

SERIKALI MKOANI MANYARA KUJENGA KITUO CHA MICHEZO CHA MKOA

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye akijibu swali toka kwa Mheshimiwa Martha Umbulla ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum lililokuwa likiuliza ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu na kujenga Senta ya michezo ya riadha mkoani Manyara ili vijana wengi wenye vipaji waweze kunufaika, leo Bungeni mjini Dodoma.

Na Benedict Liwenga-MAELEZO, Dodoma.

Serikali inaendelea kuendeleza sekta ya michezo nchini ikiwemo kutafuta maeneo ya kuwawezesha vijana kuibua, kukuza na kuendeleza vipaji vya vijana ikiwemo kuwapatia ajira vijana.

Kauli hiyo imetolewa leo Bungeni mjini Dodoma na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mhe. Nape Nnauye wakati akijibu swali toka kwa Mheshimiwa Martha Umbulla ambaye ni Mbunge wa Viti Maalum lililokuwa likiuliza ni lini Serikali itasikiliza kilio cha muda mrefu na kujenga Senta ya michezo ya riadha mkoani Manyara ili vijana wengi wenye vipaji waweze kunufaika.

Mhe. Nnauye amesema kuwa Mkoa wa Manyara pamoja na Wilaya zake una vijana wenye vipaji vya riadha na michezo ambapo Serikali inatambua pia umuhimu wa kuwa na kituo kikubwa cha michezo hasa ya riadha ambacho pamoja na mambo mengine kitasaidia kuibua, kukuza na kuviendeleza vipaji vya vijana ikiwa ni pamoja na kuwapatia ajira vijana mkoani humo.

Amesema kuwa, Serikali ya Mkoa wa Manyara imepanga kujenga Kituo cha Michezo cha Mkoa, mara bada ya kukamilisha mazungumzo na kukiubaliana na wananchi wanaomiliki ardhi mkoani humo.

Aidha, ameeleza kuwa kwa kipindi hiki ambacho Uongozi wa mkoa hauna Kituo cha Michezo, mkoa umepanga kutumia kambi ya michezo ya Hifadhi ya Taifa ya Tarangire kwa muda, wakati wanasubiri kupatikana kwa eneo la kudumu la mkoa.

“Hii inatokana na sababu kuwa hifadhi ya Taifa ya Tarangire ina hosteli za kutosha na viwanja vya michezo vya kutosha”, alisema Mhe. Nnauye.

Aliongeza kuwa, kujengwa kwa kituo hicho kutaongeza ajira na kupanua shughuli za kibiashara na hata kukua kwa uchumi wa mkoa wa Manyara.

“Serikali inaendelea na mazungumzo na wananchi wamiliki wa ardhi ili kupata eneo la ujenzi”, aliongeza Mhe. Nnauye.

Kwa upande mwingine ameziomba Halmashauri kuisadia Serikali katika kulinda maeneo ya michezo ambayo baadhi ya watu pasipo utaaratibu wanavamia na kugeuza kuwa maeneo yao ya kufanyia shughuli zao ikiwemo makazi.

1 comment:

Unknown said...

Ijemgwe Babati kwa sababu Babati in makao makuu ya mkoa wa Manyara.