Tuesday, June 14, 2016

FURSA ZA KIUCHUMI NI CHANGAMOTO KWA WATU WENYE ULEMAVU-MHE. POSSI

Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi ( Mb) akizungumza wakati wa majadiliano ya jumla kuhusu utekelezaji wa Mkataba wa Haki za Watu wenye Ulemavu. Mhe. Possi anaongoza Ujumbe wa Tanzania katika Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Watu Wenye Ulemavu. Mkutano huu wa siku tatu umeanza siku ya Jumanne hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa. Wajumbe wengine katika picha ni kutoka kushoto Mhe. Stella Ikupa Alex ( Mb), Mhe. Riziki Said Lulida ( Mb) na Mhe Elly Marko Macha ( MB). 
Ujumbe wa Tanzania wakati wa Ufunguzi wa Mkutano wa Tisa wa Mkataba wa Watu Wenye Ulemavu, ufunguzi wa mkutano huu ulifanyika katika Ukumbi Mkuu wa Mikutano ya Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa. Mkutano huu wa siku tatu ajenda yake ni "Utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”. Unahudhuriwa na Washiriki kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia Mkataba huu, Asasi zisizo za kiserikali pia zinahudhuria katika mkutano huu ambao ni maalum kwa watu wenye ulemavu wa aina zote.


Na Mwandishi Maalum, New York

Mkutano wa Tisa wa Nchi Wanachama wa Mkataba wa Haki za Watu Wenye Ulemavu ( CRDP), umeanza jana ( Jumanne) hapa Makao Makuu ya Umoja wa Mataifa, New York, Marekani.

Mada au ujumbe wa Mkutano huu wa siku tatu ni “ Utekelezaji wa Agenda ya Maendeleo Endelevu ( Agenda 2030) Kwa Watu Wote Wenye Ulemavu: Pasipo Kumwacha Yeyote”

Ujumbe wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania katika Mkutano huu, unaongozwa na Naibu Waziri, Ofisi ya Waziri Mkuu, Mhe. Dr. Abdallah Possi ( Mb). Wajumbe wengine ni Mhe. Riziki Lulinda ( MB), Mhe. Elly Macha ( Mb) ,Mhe. Stella Ikupa ( Mb) , Bi Josephine Lyengi, Kaimu Kamishna kuhusu watu wenye ulemavu na Bi. Ngusekela Nyerere , Afisa Mambo ya Nje, Wizara ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki

Akizugumza wakati wa majadiliano ya jumla mara baada ya hafla ya ufunguzi , Naibu Waziri. Dr. Abdallah Possi amesema, changamoto kubwa inayowakabilia watu wenye ulemavu nchini Tanzania, ni fursa za kiuchumi.

“Licha ya mafanikio kadhaa yakiwamo ya utungaji wa sera, sheria na mabadiliko mbalimbali kuhusu watu wenye ulemavu, bado kuna changamoto nyingi ambazo zinatakiwa kufanyiwa kazi kwa lengo la kuwapunguzia matatizo watu wenye ulemavu yakiwamo matatizo ya kutokuwa na fursa sawa na kuondokana na umaskini”. Akaeleza Naibu Waziri

Na Kuongeza kwamba, Tanzania kama ilivyo kwa nchi yingine inakabiliwa pia na vipaumbele vinavyokinzana na ambavyo ni muhimu lakini vikiwathiri zaidi watu wenye ulemavu.

Akavitaja baadhi ya vipaumbele hivyo kuwa ni pamoja na upatikanaji wa maji safi na salama, chakula, huduma za afya, elimu na ukosefu wa ajiria.

Vile vile Naibu Waziri ameleza kuwa mtazamo hasi kuhusu watu watu wenye ulemavu ni changamoto nyingine ambayo inatatiza ujumuishi wa watu wenye ulemavu katika fursa mbalimbali za maendeleo ya kiuchumi na kijamii ambazo wangeweza kunufaika nazo bila ya kujali hali zao.

Akizungumzia kuhusu mahitaji ya watu wenye ulemavu nchini Tanzania, Mhe. Dr. Possi, ameeleza washiriki wa mkutano huu kutoka nchi 164 ambazo zimeridhia mkataba wa watu wenye ulemavu kwamba, watu wenye ulemavu nchini Tanzania wanakabiliwa na tatizo kubwa la kutokuwa vifaa saidizi ambavyo vingewasaidia na kuwawezesha katika shughuli zao za kila siku.

Vivile akabainisha kuwa mwaka 2015, Tanzania ilikuwa moja ya wadhamini wakuu wa Azimio kuhusu watu wenye ualibino, azimio ambalo pamoja na mambo mengine limelenga katika kutafutia ufumbuzi baadhi ya changamoto zimazowakabili watu wenye ualibino katika maeneo mbalimbali yakiwamo ya elimu, afya na ajira.

“ Bila ya kuwa na vifaa saidizi watu wenye ulemavu wa aina yoyote ile wanashindwa kupata fursa anuai ambazo kwayo zingewawezesha kuishi pasi utegemezi na hivyo kuchangia katika yao binafsi na maendeleo ya nchi yao” akasisitiza Naibu Waziri. Na akatumia fursa hiyo ya kuhimiza upatikanaji wa vifaa saidizi kwa watu wenye ulemavu ili wawe kujitegemea.

Awali akifungua mkutano wa tisa wa Mkataba wa Watu Wenye ulemavu, Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa, Bw. Mogens Lykketoft, amesema nchi ambazo zimeridhia mkataba huo zinaowajibu wa kuchukua hatua zote muhimu zikiwamo za maendeleo jumuishi kwa watu wenye ulemavu.

“ Kila nchi mwanachama wa mkataba huu na asiye wamanachama anakazi ya kufanya, lakini katika dunia ya leo mafanikio hayamo katika mikono ya serikali peke yake” akasisitiza Rais wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa.

Na kwa sababu hiyo, ametoa wito kwa serikali zote pamoja na wadau mbalimbali kufanya kazi kwa pamoja kwa lengo la kuwawezesha watu wenye ulemavu zaidi ya bilioni moja.

Pamoja na hotuba kutoka kwa nchi wanachama, mkutano huu ambao ni wa siku tatu utakuwa na mijadala ya pembezoni yenye mada tofauti. Mkutano huo pia unashirikisha Asasi zisizo za kiserikali zinazojihusisha na masuala ya watu wenye ulemavu.

No comments: