Jonas Kamaleki-Maelezo
Serikali
imeliagiza Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) kutoagiza
transfoma nje ya nchi na badala yake kutumia zinazotengenezwa hapa
nchini na kampuni ya Tanalec.
Agizo hilo limetolewa leo Bungeni
Dodoma na Naibu Waziri wa Nishati na Madini, Mhe. Dkt. Medard Kalemani
alipokuwa akijibu swali la Mbunge wa Tunduru Kusini, Mhe. Daimu Iddi
Mpakate aliyetaka kujua ni lini Serikali itatoa pesa kukamilisha miradi
ya umeme wa Wakala wa Umeme Vijijini (REA).
Dkt. Kalemani
alisema uzalishaji wa transforma ni mkubwa ikilinganishwa na mahitaji ya
bidhaa hizo kwa mwezi, hivyo hakuna sababu ya kuagiza transforma hizo
kwa bei kubwa wakati zinapatikana hapa nchini.
Kuhusu suala la
kugharamia nguzo kwa Mpango wa REA Dkt. Kalemani alisema mteja hatakiwi
kutozwa gharama yoyote ziadi ya Tshs. 27,000 fedha ya kuunganishiwa
umeme kwa mpango huu.Dkt. Kalemani alisema kuwa Serikali inatekeleza
Mradi wa REA Awamu ya II katika Wilaya ya Tunduru na kazi hii
inategemewa kukamilika mwishoni mwa mwezi Juni, 2016.
Alisema
Kazi ya kupeleka umeme katika wilaya hiyo ni pamoja na ujenzi wa njia ya
umeme msongo wa kilovoti 33 yenye urefu wa Kilomita 293. 2, na ujenzi
wa njia nyingine yenye msongo wa kilovoti 0.4 yenye urefu wa kilomita
76.1 na ufungaji wa transfoma 38 pamoja na kuwaunganishia umeme wateja
wa awali 3,330
“Gharama ya Mradi kwa Mkoa wa Ruvuma ikiwemo
Wilaya ya Tunduru ni Tsh. Bilioni 32.56,” alisema Dkt Kalemani na
kuongeza kuwa mkandarasi amekwishalipwa bilioni 27.22 sawa na asilimia
83.6 ya fedha.
Dkt. Kalemani amesema kuwa katika Wilaya ya Tunduru
ni vijiji vinne ambavyo vimeunganishiwa miundombinu ya umeme na
kufanyiwa majaribio kabla ya kuwashiwa umeme.
Kwa mujibu wa
Dkt. Kalemani mkandarasi anaendelea kufunga transforma na Mita za Luku
katika vijiji 34 vilivyosalia kwa Wilaya ya Tunduru ili viweze kupatiwa
huduma ya umeme ifikapo tarehe 30 Juni, 2016.
No comments:
Post a Comment