Wednesday, June 8, 2016

Vinara Sita Wa Ujangili Wakamatwa Tanzania,Yumo "Shetani na Malikia"


SERIKALI imesema imekamata vinara sita wa ujangili wakiwamo wawili wanaojulikana kwa majina ya ‘shetani na ‘malikia’ ambao walikuwa wakisakwa kwa muda mrefu. 
Mbali ya vinara hao ambao majina yao yamehifadhiwa kwa sababu za usalama, pia msako mkali unaendelea dhidi ya majangili nane. 

Akizungumza wakati wa kufungua wa mkutano wa mwaka wa Hifadhi za Taifa Tanzania (TANAPA) na wahariri na waandishi wa habari waandamizi kutoka vyombo mbalimbali vya habari mjini Morogoro jana, Waziri wa Maliasili na Utalii, Profesa Jumanne Maghembe alisema kukamatwa kwa majangili kunatokana na mkakati wa wizara kuhusu vita dhidi ya ujangili. 

“Tumefanikiwa kukamata shetani na malkia wa ujangili ambao kwa kweli wamekuwa vinara wa ujangili…wapo wenzao wanane ambao wanaendelea kutafutwa, naamini tutawakamata tu,”alisema Waziri Maghembe. 

Alisema vita dhidi ya ujangili hivi sasa inapiganwa kwa ushirikiano mkubwa wa nchi za Jumuiya za Afrika Mashariki na Jumuiya ya Maendeleo ya Kusini mwa Afrika (SADC), kwa vile tatizo hilo limekuwa mtambuka. 

Baada ya kuona tatizo hilo linashamiri, Serikali imeamua kupeleka taarifa Baraza Kuu la Usalama la Umoja wa Mataifa (UN) isaidie kuzibana baadhi ya nchi ambazo zimekuwa vinara wa kununua pembe za ndovu, ikiwamo China. 

“Baada ya kuona vita hii ni kubwa tumelazimika kupeleka kilio chetu pale UN watusaidie kuwabana wanunuzi wakubwa ambao wamekuwa wakitoa fedha nyingi kwa ya biashara hii. 

“Pamoja hawa wakubwa wana nafasi kubwa na mchango mkubwa wa kusaidia tatizo hili, maana fedha zinatokea kwao,”alisema Waziri Maghembe. 

Alisema pamoja na hatua hizo, bado tatizo la mauaji ya wanyama kama tembo, faru na simba bado ni kubwa. 

Kuhusu changamoto katika hifadhi za taifa, Waziri Maghembe alisema limekuwapo wimbi kubwa la uingizaji wa mifugo ambayo inahatarisha uhai wa wanyamapori. 

“Hivi sasa tuna sheria ya kuzuia mifugo kuingia ndani ya hifadhi,” alisema. 

Akizungumzia idadi ya watalii waliongia nchini kuanzia Januari hadi Desemba 2015, alisema waliingia milioni 1.1, huku wizara ikipata Dola za Marekani bilioni 2. 

Naye Mkurugenzi Mkuu wa TANAPA, Allan Kijazi alisema vyombo vya habari vina jukumu la kufichua mitandao ya ujangili, uharibifu wa misitu na vitendo visivyokubalika katika hifadhi za taifa. 

Alisema kuna kila sababu Watanzania kujenga utamaduni wa kutembelea vivutio vilivyopo ili kujenga utalii wa ndani.

No comments: