Friday, June 3, 2016

VYAMA VYA UPINZANI KUFANYA MAANDAMANO NCHI NZIMA KUPINGA KUSIMAMISHWA WABUNGE WAKE 7

Leo Juni 3/2016 Chama cha ACT Wazalendo Kimeelezea msimamo wake juu ya uamuzi uliofanywa na Kamati ya Bunge ya Maadili na Madaraka ya Bunge kuwasimamisha wabunge saba wa upinzani akiwemo Mbunge wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe.

Uamuzi huu wa Kamati ya Maadili ambayo sehemu kubwa ya wajumbe wake ni wabunge wa Chama cha Mapinduzi(CCM) unafuatia msimamo wa wabunge wa upinzani wakiongozwa na Mbunge wa Chama chetu kupigania maslahi ya wananchi kupata habari za bunge.

ACT Wazalendo inaamini Wabunge hawa wametolewa kafara kwa kupinga vikali uamuzi wa Serikali kuzuia matangazo ya Bunge kurushwa moja kwa moja.

Chama kimeandaa mapokezi haya yaliyopewa jina maalum la “Opereshen” Linda Demokrasia, lengo likiwa ni kuwapa nafasi mashujaa waliofukuzwa bungeni kwa ajili ya kusimamia maslahi ya umma, kuelezea kilichotokea na kinachoendelea bungeni ambacho watawala hawataki kijulikane.
Pia katika mkutano wa hadhara Kiongozi wa Chama ndugu Zitto Kabwe atafafanua kwa kina muktadha wa siasa za sasa na hatari ya kuua vita dhidi ya ufisadi kutokana na namna demokrasia inavyofifishwa

Kwa kutambua umuhimu wa utetezi wa maslahi ya wananchi na kuisimamia serikali kupitia Bunge Chama chetu baada ya mkutano wa Dar esSalaam utakaofanyika Jumapili ya Juni 5 mwaka huu katika viwanja vya Mbagala Zakiem, pia Chama kitafanya mikutano mingine mikubwa ya hadhara katika mikoa ya Mwanza ( 11 Juni, 2016), Kigoma (12 Juni, 2016), Mbeya (18 Juni, 2016) na Morogoro (19 Juni, 2016).

Chama imeviandikia barua vyama vya CUF, CHADEMA na NCCR-Mageuzi kuviomba kushiriki kwenye mapokezi hayo.Tunasubiri majibu ya vyama tulivyowaalika kwa kuwaandikia barua kwa kuwa mpaka sasa hawajatujibu rasmi kama watashiriki ama la zaidi ya kutufahamisha kuwa wamepokea barua zetu

ACT-Wazalendo,inaamini “Operesheni Linda Demokrasia” ni muhimu ikapiganwa na vyama vyote pasipo kujali itakadi ya vyama kwa kuwa hoja hiyo ya kutaka Bunge lioneshwe moja kwa moja ilipoibuliwa na Mbunge Ndugu Zitto Kabwe kuhoji hatua ya serikali kubana uwazi Bungeni,wabunge wote wa upinzani walisimama na kuiunga mkono hoja na kuitetea

Ndugu Ado Shaibu Ado
Katibu, Itikadi Uenezi na Mawasiliano ya Umma,
ACT Wazalendo

1 comment:

Anonymous said...

Tena kama ingebidi wangefukuzwa wote,maana hawajitambui.Badili ya kupigania maslahi ya wapiga kura wao, wamebakia kuendesha siasa za matukio.
Mathalani,Kigoma ni mkoa uliojaliwa kuwa na rasilimali nyingi lakini ni mmoja ya mikoa iliyonyuma sana kimaendeleo.Nilitegemea huyo Zito ajikite katika kupeleka maendeleo Kigoma lakini amegeuka kuwa an opportunistic politician anaevizia matukio na kuyashupalia na kupoteza muda wake kujifanya mshauri wa raisi ( in proxy ).in short hawana faida kwa wapiga kura wao.