YANGA imemnasa mshambuliaji mpya raia wa Zambia, Obrey Chirwa anayechezea klabu ya Platinum FC ya Zimbabwe kwa kitita cha dola za Marekani 120,000 (zaidi ya Sh milioni 240 za Tanzania).
Kwa mujibu wa gazeti la The Herald la Zimbabwe jana lilieleza kuwa Chirwa ambaye amewahi kuichezea timu ya Konkola Blades ya Zambia, ameifungia Platinum mabao matano katika mechi nane alizocheza kwenye Ligi Kuu ya Zimbabwe.
Chirwa, ambaye yumo kwenye kikosi cha timu ya taifa ya vijana ya Zambia chini ya umri wa miaka 23 imeelezwa na gazeti hilo kuwa aliondoka Zimbabwe juzi kuja Dar es Salaam na alitarajiwa kuwasili Dar es Salaam jana.
Chirwa anatarajia kushirikiana na mshambuliaji mahiri wa Yanga Donald Ngoma, ambaye pia ametokea timu hiyo ya Zimbabwe. Awali Yanga ilikuwa ikimuwania winga Walter Musona kutoka Platinum kabla ya kughairi dakika za mwisho na Chirwa kuonekana mtu sahihi kwa nafasi hiyo.
Kumbuka baadhi ya vyombo vya habari vilimnukuu kiongozi mmoja wa juu wa Simba akitanabaisha kuwa kwa msimu huu wametenga milioni 250 kwa ajili ya usajili,hivyo kwa dau hilo ni sawa na dau ambalo Yanga wamelitumia kumnunua Chirwa.
Viongozi wa Yanga hawakupatikana jana kuzungumzia suala hilo na hata Kocha Mkuu wa timu hiyo, Hans Pluijm ambaye yupo Algeria na Yanga, alipotafutwa kwa njia ya mtandao kuhusu usajili huo alisema hana cha kuzungumza.
Wakati huohuo, Yanga iliwasili salama jana asubuhi nchini Algeria tayari kwa mchezo wa Kundi A Kombe la Shirikisho la Soka Afrika (CAF CC) dhidi ya wenyeji MO Bejaia.
Nahodha wa timu hiyo Nadir Haroub ‘Cannavaro’ alisema wachezaji wote wapo katika ari ya ushindi kwa ajili ya mchezo huo utakaofanyika Uwanja wa Unite Maghrebine mjini Bejaia, Algeria
No comments:
Post a Comment