Advertisements

Saturday, July 2, 2016

MAJENGO YA MAHAKAMA YA MAFISADI KUKABIDHIWA JUMATATU

WAKATI Mahakama Maalumu ya Ufisadi na Uhujumu Uchumi ikitarajiwa kuanza wakati wowote, majengo ya mahakama hiyo yanatarajiwa kukabidhiwa keshokutwa jumatatu.

Jaji Mkuu, Mohamed Othman Chande, alisema jana kuwa mkandarasi aliyekabidhiwa kazi ya kukarabati majengo hayo yaliyopo katika Shule Kuu ya Sheria, pembeni mwa kituo cha mabasi cha Simu 2000, Ubungo Dar es Salaam, yako katika hatua za mwisho za ukarabati.

Akizungumza katika viwanja vya Karimjee baada ya kuapisha mawakili wapya 623 wa Mahakama Kuu, Jaji Chande alisema tayari Bunge limeshapitisha muswada wa sheria ya uanzishwaji wa mahakama hiyo.
Alisema kwa sasa muswada huo utawasilishwa kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania kwa ajili ya kuusaini ili uwe sheria, kisha sheria hiyo itatangazwa katika gazeti la Serikali ili kuruhusu shughuli za mahakama hiyo kuanza.

Kwa mujibu wa Jaji Mkuu, Mahakama iko tayari kuendesha Divisheni hiyo ya Mahakama na baada ya kukabidhiwa majengo hayo, wataanza kutoa semina kwa majaji na watumishi wengine wa mahakama hiyo, kuhusu divisheni hiyo itakavyoendesha shughuli zake.

Aliweka wazi kuwa mpaka sasa hakuna kesi hata moja iliyokwishatambuliwa kwamba itashughulikiwa na mahakama hiyo.

1 comment:

Anonymous said...

Hatua nzuri tunaimani kuanziswa kwa mahakama hii itaharakisha maamuzi katika kesi husika . Tunaimani pia wahudumu wa mahakama hizi watakuwa watu wenye uwezo wa kutosha katika kuendesha kesi husika hasa kimaadili. Imani yetu watanzania yakwamba mahakama hizi zitatoa haki sawa kulingana na kosa husika bila ya kujali wadhifa wa mtu,uwezo wa mtu au nguvu yake kipesa au cheo kwani fisadi ni fisadi awe raisi,waziri,mkurugenzi,mtumishi wa umma au mfanya biashara mkubwa au mdogo akihusika na ufisadi basi imani yetu watanzania kuwa kuanzishwa kwa mahakama hizi chini ya usimamizi wa serikali ya Magufuli haki itapatikana na kuwa muarubaini wa kukomesha tabia mbovu iliojengeka katika jamii yetu yakwamba mwenye pesa hana dhambi na yupo juu ya sheria.