Advertisements

Wednesday, July 20, 2016

TUNATEKELEZA ELIMU JUMUISHI-TANZANIA

Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa, Balozi Tuvako Manongi akizungumza jambo na Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Erna Solberg wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa Lengo Namba Nne la Maendeleo Endelevu kuhusu Elimu
Sehemu wa Washiriki wa Majadiliano hayo ambayo yalijikita zaidi katika kuhakisha ni kwa namna gani serikali zinatekeleza utoaji wa elimu jumuishi , nyenye kiwango bora pasipo kumwacha yeyote nyuma, changamoto zake na nini kifanyike.

Na Mwandishi Maalum
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeanza kwa namna moja ama nyingine utekelezaji wa lengo namba Nne ya Maendeleo Endelevu kuhusu Elimu la Maendeleo Endelevu (SDG4) kwa kutoa elimu bure kuanzia shule ya msingi hadi sekondari ikiwa ni pamoja na kuifanya jumuishi kwa makundi yote ya jamii wakiwamo walemavu wa aina mbalimbali.

Hayo yameelezwa na Mwakilishi wa Kudumu wa Tanzania katika Umoja wa Matifa, Balozi Tuvako Manongi wakati wa majadiliano kuhusu utekelezaji wa lengo namba Nne ambalo ni kati ya Malengo 17 ya Maendeleo Endelevu, maarufu kama agenda 2030 yaliyopitishwa mwezi septemba mwaka jana na viongozi wakuu wa nchi na serikali.

Balozi Manongi alikuwa mmoja wa wazungumzaji wakuu katika majadiliano hayo, ambayo yalimhusisha pia Waziri Mkuu wa Norway, Mhe. Erna Solberg na Mkurugenzi Mkuu wa UNESCO Bi. Irina Bakova na yaliandaliwa kwa ushirikiano wa UNESCO na UNICEF kama sehemu ya Mkutano wa Kilele wa Kisiasa wa Baraza la Uchumi la Umoja wa Mataifa ( ECOSOC) unaoendelea hapa Umoja wa Mataifa.

SGD4 pamoja na mambo mengine inatilia mkazo na kutoa kipaumbele cha pekee katika utoaji na upatikanaji wa elimu ambayo ni jumuishi, yenye ubora na inayowafikia makundi yote ya jamii, hususani watoto, wanawake na walemavu.

Akielezea namna Tanzania ilivyojipanga katika utekelezaji wa SDG4 kwa sasa na kwa baaday,Balozi Manongi amesema Tanzania imejipaga vema kisera, kisheria na kimkakati katika kuhakikisha kwamba kila mtanzania bila kujali ni wa kundi gani anapata fursa ya elimu na si elimu tu bali elimu yenye ubora wa hali ya juu na inayokidhi mahitaji na mazingira ya sasa.

Pamoja na kuainisha sera na sheria mbalimbali ambazo serikali inazitekeleza katika eneo hilo la elimu, Balozi Manongi anasema, kuwa na sera nzuri, sheria nzuri na mikakati mizuri hakuwezi kuwa kigezo pekee cha kufanikisha utekelezaji wa SDG4.

“ Kwa Tanzania tatizo siyo sera, sheria au mipango na mikakati, tatizo ni raslimali fedha ya kutosha ( bajeti) itakayowezsha utekelezaji wa SDG4 na malengo mengine kwa ukamilifu unaotakiwa”. Anasema Balozi

Kutokana na changamato hiyo ya ufinyu wa raslimali fedha, Mwakilishi huyo wa Tanzania katika Umoja wa Mataifa anasisitiza haja na umuhimu wa ushirikiano wa karibu baina ya Serikali Kuu, Sekta Binafsi na Wadau wa Maendeleo kwa lengo la kuhakikisha kwamba hakuna yeyote atakaye achwa nyuma.

Akizungumzia zaidi utekelezaji wa SGD4 achia mbali utoaji wa elimu bure kuanzia ngazi ya msingi hadi sekondari, na kuhakikisha elimu inawafikia wote, Balozi Manongi amewaeleza wajumbe wa mkutano huo kwamba hivi karibuni Serikali imetangaza kutenga kiasi cha fedha kwaajili ya kuwasomesha watu wenye matatizo ya ualibino.

“pamoja na changamoto mbalimbali serikali yangu inajitahidi sana kuyafikia makundi mbalimbali ya jamii, wawe ni watoto wa kike, watoto wanaoishi katika mazingira magumu, ama jamii za wafugaji na wawindaji lakini pia imekwenda mbali zaidi katika kuhakikisha kwamba jamii yenye mahitaji maalum nayo inafikiwa” akasisitiza Balozi Manongi.

Akizungumzia zaidi kuhusu uamuzi wa Serikali ya awamu ya Tano wa kuifanya elimu ya msingi hadi Sekondari kuwa bure. Balozi amewaeleza wajumbe wa majadiliano hayo kwamba, maana ya uamuzi huo ni kuwa mtoto wa kitanzania atafaidika na elimu ya bure kwa miaka kumi na moja. Na vile vile Tanzania inakuwa sehemu ya utekelezaji wa baadhi ya kipengele cha SDG4 kinachopendekeza utoaji wa elimu bure ili iwafikia watu wengi zaidi.

Washiriki wengine katika majadiliano hayo walikuwa ni Mwakilishi wa Kudumu ya Jamhuri ya Korea Balozi Oh Joon ambaye pia ni Rais wa ECOSOC, Waziri wa Elimu kutoka Bolivia Bw. Bw. Roberto Iván Aguilar Gómez, Bw. Guy Ryder, Mkurugenzi Mkuu wa Shirika la Kazi Duniani (ILO) Mwakilishi wa Kudumu wa Ufalme wa Morroco katika Umoja wa Mataifa, Balozi Omar Hilale, Bi. Alice Albright kutoka Global Partnership for Education (GPE),Bi Silvia Montoya, kutoka Tasisi ya Takwimu ya UNESCO na Bi. Josephine Bourne kutoka UNCEF.

No comments: