Advertisements

Tuesday, July 5, 2016

WALEMAVU WALIA NA UPUNGUFU WA WALIMU.

Mtoto Clara Damian mwanafunzi wa darasa la saba asiyeona akiwa darasani  akitumia mashine maalumu ya kuandikia na kusoma katika shule ya msingi  patandi iliyopo wilaya ya arumeru mkoani arusha shule hiyo inakabiliwa na upungufu wa walimu na vitabu.


Na Woinde Shizza, Arusha.
Wanafunzi wenye ulemavu katika shule ya msingi Patandi iliyopo wilaya ya Arumeru Mkoani Arusha wamelalamikia tatizo la upungufu wa walimu,vitabu na vifaa vya kufundishia kwa wanafunzi hao wenye mahitaji maalumu hali inayokwamisha maendeleo ya kitaaluma hivyo wameiomba serikali na taasisi binafsi kutatua changamoto hiyo.

Mwanafunzi asiyeona anayesoma darasa la saba Clara Damian ni alisema kuwa kumekua na uhaba wa vitabu kwa watoto wasioona na mashine za kuandikia maandishi yenye nundu ambazo ni chache na kwa sasa ni mashine tatu pekee zinafanya kazi ukilinganisha na idadi kubwa ya wanafunzi.


Alisema kuwa miundombinu ya majengo ya madarasa pia yamekua si rafiki kwa watoto wenye ulemavu hivyo anashauri miundombinu ya majengo na shule iendane na mahitaji wa watoto hao.

Mibaku Limba Mwanafunzi asiyesikia (kiziwi) alisema kuwa walimu walioko kwa sasa wanaofundishwa kwa lugha za alama ni wachache ukilinganisha na idadi ya masomo hali ambayo inachangia kuwarudisha nyuma.

Mratibu wa Kitengo Cha Walemavu Mwalimu Anna Shayo Katika Shule hiyo Mwalimu Shayo alikiri kuwepo kwa upungufu wa walimu na vitabu kwa watoto wenye mahitaji maalumu na kuiomba jamii,taasisi na serikali kushiriki katika kuboresha maendeleo ya watoto hao ambao wakijengewa misingi bora ya elimu wanaweza kuwa na mchango kwa jamii badala ya kuwa tegemezi.

Mwalimu Marko Alois Mamuya anayefundisha watoto viziwi ameiomba serikali itoe motisha kwa walimu wanaofundisha watoto wenye mahitaji maalumu ili kuongeza ari na hamasa itakayosaidia kupata idadi kubwa ya walimu.

“Tunawaomba wazazi wasiwafiche watoto wenye ulemavu majumbani bali wawalete mashuleni huku waweze kupata elimu ,lishe na mazoezi badala ya kuwafungia nyumbani kwani wanazidi kuwa tatizo licha nya uwezo,vipaji na ubunifu walioanao ambao unaweza kuwasaidia wao na jamii yao” alisema Mwalimu Marko.

No comments: