Advertisements

Wednesday, July 20, 2016

Waziri Mahiga asaini Mkataba wa uenyeji wa Benki ya EADB

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Dkt. Augustine Mahiga (Mb) amesaini Mkataba wa uenyeji (Host Agreement) wa Ofisi za Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki (EADB) na Mkurugenzi Mkuu wa Benki hiyo Bi. Vivienne Yeda. Mkataba huo umesainiwa leo katika Ofisi za Wizara  kwa lengo la kurasimisha kisheria Ofisi za Benki hiyo zilizopo nchini.
Aidha, uwekaji saini wa mkataba huo ni utekelezaji wa agizo la Mkutano wa Wakuu wa Nchi  Wanachama wa Jumuiya ya Afrika Mashariki  uliofanyika tarehe 2 Machi, 2016  Mjini Arusha -Tanzania. Mkutano huo pamoja na mambo mengine uliazimia kuanzishwa kwa Ofisi za Benki hiyo katika Makao Makuu ya kila nchi Mwanachama ili kuwezesha utekelezaji madhubuti wa shughuli za Benki hiyo.  
Benki ya Maendeleo ya Afrika Mashariki ni Taasisi ya Fedha iliyoanzishwa mwaka 1967 chini ya iliyokuwa  Jumuiya ya Afrika Mashariki, kwa lengo la kutoa misaada ya kifedha na misaada mingine  ndani ya Jumuiya ya Afrika Mashariki.
EADB ilianzishwa wakati iliyokuwa Jumuiya ya Afrika Mashariki ikiwa na wanachama watatu ambao ni Tanzania, Kenya na Uganda.  Rwanda ilijiunga na Benki hiyo  mwaka 2007 na kufanya nchi wananchama waliojiunga kufikia wanne.

Kwa upande wa Tanzania, EADB imeisaidia kutoa mikopo mbalimbali katika miradi ya maendeleo kupitia Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) na Benki ya Uwekezaji Tanzania (TIB). Pia, katika kulipa kipaumbele suala la Afya, Benki hiyo  imeweka mpango wa kusaidia afya ya uzazi kwa akinamama hususan,  katika maeneo ya vijijini.
Miradi mingine inayofadhiliwa na EADB hapa nchini ni pamoja na miradi ya Umeme hasa kwa maeneo ya vijijini, na miradi ya maji na usafi wa mazingira.
Akiongea katika hafla hiyo,  Mhe. Waziri Mahiga aliahidi kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kutoa ushirikiano wa karibu katika kuhakikisha uendeshaji wa Benki hiyo unafanikiwa. “Karibuni sana na pale inapotokea  mmekwama katika jambo lolote linalohitaji usaidizi wa Serikali au ushauri tupo tayari kutoa ushirikiano” alisema Waziri Mahiga.

No comments: