Advertisements

Wednesday, August 3, 2016

MBUNGE NASSARI NA MADIWANI 28 WA CHADEMA WAFUTIWA KESI

SERIKALI kupitia Ofisi ya Mwendesha Mashitaka (DPP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali, imetakiwa kufanya utafiti wa kina katika mashauri inayoyafungua mahakamani.

Kauli hiyo ilitolewa mjini Arusha jana na Wakili wa Kujitegemea, Charles Abraham, aliyekuwa akiwawakilisha watuhumiwa 29 katika kesi iliyofunguliwa na Jamhuri dhidi ya Mbunge wa Arumeru Mashariki, Joshua Nassari (Chadema) na madiwani 28 wa chama hicho wakituhumiwa kuvunja uzio wa thamani ya Sh milioni saba.

Akizungumza nje ya viwanja vya Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha baada ya Hakimu Mkazi, Desder Kamugisha kuifuta kesi hiyo, Wakili Abraham alisema uamuzi huo ulitolewa baada ya Serikali kukosa ushahidi.

“Ni rai yangu kwa Serikali  kwamba iwe inafanya utafiti katika mashauri inayoletewa kabla haijapeleka kesi mahakamani. Hii itasaidia kuondoa gharama zisizo za lazima na usumbufu kwa watu na jamii wakiwamo viongozi,” alisema Wakili Abraham.

Awali, mahakamani hapo, upande wa Jamhuri ukiongozwa na Wakili Blandina Msawa, uliwasilisha ombi la kutokuwa na nia ya kuendelea na shauri hilo, hivyo ulimuomba hakimu huyo kuiondoa  hoja ambayo ilikubaliwa na upande wa utetezi.

Akitoa uamuzi wa kuifuta kesi hiyo, Hakimu Kamugisha alisema kwa vile upande wa mashitaka umeamua kuiondoa kesi hiyo, mahakama haitakuwa na kipingamizi.

Mbunge Nassari akizungumzia kufutwa kwa kesi hiyo, alisema ilifunguliwa kisiasa badala ya kuangalia maslahi ya mali za Serikali.

Naye Mwenyekiti mstaafu wa CCM, Yona Nnko ambaye mwaka jana alihamia Chadema, alimpongeza Nassari na madiwani kwa kufanikiwa kupigania haki ya wananchi wa Arumeru Mashariki.

Nassari na madiwani hao walifunguliwa kesi hiyo na Jamhuri wakidaiwa kuharibu mali ya Itandumi Makere katika eneo la Usa River.

1 comment:

Anonymous said...

Kwa mtizamo kesi nyingi zilizo mahakamani na hasa za zinazishabihiana na siasa hasa pindi za uchaguzi ni batili na serikali inapoteza fedha nyingi pia. Hata wafungwa wengi magerezani kesi zao hazijafanyiwa kazi kwa kukosa shahidi na kuendelea kuwaweka humo. Kesi nyingine ni za kijamii na za kiajabu ambazo labda zingemfunga mkosaji kifungo cha nje miezi 3 bila kutoka nje ya mji na kuripoti kituoni kila wiki. Tungepunguza machungu kwa wananchi. Mkwepa kodi!!