Advertisements

Friday, August 12, 2016

WANAWAKE KENYA WATAFUTA WANAUME ZAO TANZANIA

Arusha. Zaidi ya wanawake wa Kenya 300 wa jamii ya Kimasai wameandamana hadi mji wa Namanga uliopo mpaka wa Tanzania na Kenya kuwasaka waume zao.

Mkuu wa Wilaya ya Longido, Daniel Chongolo amethibitisha kutokea tukio hilo juzi akisema amefanya mazungumzo na wanawake hao na kufikia mwafaka.

Chongolo amesema kuwa hoja za wanawake hao ilikuwa ni waume zao kila wanapopata fedha wamekuwa wakiondoka nyumbani na kuvuka mpaka na kuingia nchini kufanya starehe na baadhi yao wamelowea katika miji ya Namanga na Longido.

“Kwanza kabla ya kuwasikiliza niliwaeleza wamevunja sheria kwa kuingia nchini na kufanya vurugu... walikiri na kuomba radhi,” alisema Chongolo.

Amesema Kamati ya Ulinzi na Usalama ya wilaya hiyo, imeagiza wote walioharibiwa mali kutokana na maandamano hayo kufanya tathimini na kutoa taarifa ya hasara waliyopata.

Chongolo amesema baada ya majadiliano na wanawake hao walikaa kikao cha maridhiano na viongozi wao, akiwamo Gavana wa Wilaya ya Kajiado nchini Kenya, Alex Mutua.

Chongolo amesema baada ya makubaliano, wanawake hao wameridhika na kurejea kwao katika eneo la Kajiado linalopakana na Longido.

Kutokana na malalamiko ya wanawake hao, Chongolo alipiga marufuku unywaji pombe wakati wa saa za kazi katika miji ya Namanga na Longido. “Nimebaini kuna watu wanatoka nchi jirani na kuja kulewa huku kwetu Tanzania,” alisema Chongolo.

Amewataka wanawake wa Tanzania kujiepusha na tuhuma za kuwafungia makwao wanaume kutoka Kenya ili kuepusha migongano.

Baadhi ya wakazi wa Namanga walisema chanzo cha wanaume hao kunywa pombe za kienyeji upande wa Tanzania ni kutokana na kuuzwa kwa bei nafuu.

Mkazi wa mpakani mwa Kenya na Tanzania, Joram Kiseri alisema wamekuwa na uhusiano kwa muda mrefu na raia hao, hivyo kuja Tanzania ni jambo la kawaida.

No comments: