Advertisements

Friday, September 23, 2016

KIKWETE ATUNUKIWA TUZO YA UONGOZI WA KISIASA NA UTETEZI

Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete akipokea Tuzo ya Uongozi wa Kisiasa na Utetezi kutoka kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Speak Up Afrika Bi Kate Campana, katika hafla iliyofanyika siku ya Alhamis New York Marekani. Tuzo hiyo ni kutambua jitihada na juhudi zake za kufikisha huduma za jamii hususani afya kwa kwa wanawake na watoto.
Rais mstaafu Kikwete baada ya kupokea Tuzo yake akirejea kwenye kiti chake
Rais Mstafu Kikwete akizungumza baada ya kukabidhiwa Tuzo yake na katika shukrani zake za kukubali Tuzo hiyo, amesema Tuzo hiyo ni kwa watoto wote wa Afrika ambao ndio wamemwezesha yeye kupata Tuzo
Sehemu ya wageni waalikwa katika hafla ya utoaji tuzo iliyokwenda sawia na miaka mitano ya Speak Up Afrika pamoja na uzinduzi wa uchangiaji kwa kazi za Taasisi hiyo.

Na Mwandishi Maalum, New York

Shirika lisilo la Kiserikali la Speak Up for Afrika limemtunukia tuzo, Rais Mstaafu Jakaya Mrisho Kikwete kutokana na uongozi wake wa kisiasa na utetezi wake kwa makundi ya jamii yaliyo katika mazingira magumu hususani wanawake na watoto.

Utoaji wa Tuzo hiyo ya uongozi wa kisiasa na utetezi , umekwenda sambamba na hafla ya miaka mitano ya kuanzishwa kwa Taasisi ya Speak up Afrika. Hafla hiyo iliyofanyika jana Alhamisi Jijini New York ilikuwa pia ni sehemu ya kuhamasisha uchangiaji wa shughuli za Taasisi hiyo.

Mchango ambao umetambuliwa na Speak Up Afrika, taasisi ambayo imekuwa ikifanya kazi kwa Karibu na Rais Mstaafu Kikwete, ni katika maeneo ya upelekaji na usambazaji wa huduma za msingi za afya hususani afya ya mama na mtoto, udhibiti wa ugonjwa wa malaria kupitia kampeni ya malaria haikubaliki ,usambazaji wa vyandarua vyenye viatilifu, kampeni ya lishe bora, na kampeni ya chanjo kwa watoto.

Pamoja na kutambua juhudi za Rais Mstaafu Kikwete katika kuyasemea maeneo hayo, Taasisi hiyo kupitia Mkurugenzi wake Mtendaji Bi. Kate Campana pia imemtambua kama kiongozi ambaye amekuwa mstari wa mbele wa kulisema Bara la Afrika kila mara alipopata fursa ya kufanya hivyo wakati akiwa madarakani na hata baada ya kustaafu.

Rais kikwete ameelezwa katika hafla hiyo iliyowashirikisha wadau wa kada mbalimbali, kama kiongozi wa kisiasa ambaye amezigusa nyoyo za watu wengi kujitolea kwaajili ya watu wenye mahitajio ya kupata huduma za msingi za kijamii ambazo au wameshindwa kuzipata kutokana na kipato kidogo au haziwafikii kabisa.

Akipokea Tuzo hiyo, Rais Mstaafu Kikwete , amesema Tuzo hiyo ni ya watoto wote waafrika ambao ndio waliomfanya asimame mbele ya wageni waalik

“ Ni kwa sababu yenu ndio sababu nimetenga muda wangu baada ya kustaafu kusukuma mbele agenda ya kuboresha maisha yanu. Ninafanya hivyo kwasababu makuzi yangu yalikuwa kama ya mtoto yeyote yule wa kiafrika, nimeyaishi maisha wanayo ishi. Na kwa hiyo ninaelewa fika hamu na kiu yao ya kuwa na maisha bora na afya njema”. Akasema Kikwete na kushangiliwa na wageni waalikwa.

Akaongeza kuwa , mafaniko ambayo ameyapata katika juhudi hizo za kufikisha huduma za msingi za kijamii kwa makundi yenye mahitaji yametokana na mambo mawili makubwa moja ni aina ya uongozi alioutumia kusukuma harakati hizo. Na pili uhamasishaji uliofanyika katika kupiga vita malaria kupitia Speak Up Afrika na kampeni yao ya malaria haikubaliki.

“ Nisingeweza kuyafanya niliyoyafanya bila uungugwaji mkono na ushirikiano wa karibu nilioupata na ninaoupata kutoka taasisi za kimataifa ikiwamo hii ya Speak Up Afrika. Ndio maana kwa mfano, tumeweza kupunguza visa vya malaria kwa theluthi mbilli, tumefanikisha upatikanaji wa chanjo kwa asilimia 96 kwa watoto wote na kupunguza vifo vitokanavyo na malaria kwa nusu.” Akaeleza Kikwete na kushangiliwa tena.

Akasema, anamini katika ushirikiano na wadau mbalimbali kama akina Ray Chambers kupitia kampeni ya hakuna tena malaria, Taasisi ya Bili na Melinda Gates na Gavi Vaccination Alliance ambayo anashirikiano nayo kwa karibu katika kampeni ya chanjo kwa wote.

Rais Mstaafu amewahakikishia watendaji wa Speak Up Afrika kwamba ataendelea kufanya kazi nao kwa karibu kutokana kile alichosema amejionea mwenye kazi nzuri wanayoifana.

Akawasihi wadau mbalimbali kuichangia taasisi hiyo kwa kile alichosema, inafanya kazi kubwa ya siyo tu kufikisha huduma za kijamii pale zinapotakiwa lakini pia imekuwa ni kipaza sauti cha Afrika.

Wengine waliopewa Tuzo kwa kutambua michango yao kwa jamii ni pamoja na Professa Awa Marie Coll- Seck, Waziri wa Afya wa Senegal, Bibi Toyin Saraki, mwanzilishi wa Taasisi ya Wellbeing Afrika ambayo pia imekuwa ikitoa elimu na misaada kwa wanawake na watoto pamoja na elimu kwa wakunga na kutambua kazi nzuri, kubwa na ngumu ya kuwahudumia wanawake wenzao wanapojifungua. Na Bwana Kabirou Mbodje ambaye ni Mkurugenzi mtendaji wa Taasisi ya Wari.

Taasisi ya Speak Up Afrika imeanzishwa na wanawake na inaongozwa na wanawake. Ni taasisi ambayo imejijengea uweo na sifa kubwa ndani ya kipindi cha miaka mitano tangu kuanzishwa kwake.

No comments: