ANGALIA LIVE NEWS

Monday, October 31, 2016

Lowassa, Sumaye Wapiga Kambi Dodoma Ili Kuteta na Wabunge wa UKAWA


Mawaziri Wakuu wa zamani ambao ni wajumbe wa Halmashauri Kuu ya Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Edward Lowassa na Frederick Sumaye wameweka kambi mjini Dodoma ili kuteta na wabunge wa Ukawa.

Mkurugenzi wa Itifaki, Mawasiliano, Uenezi na Mambo ya Nje wa Chadema, John Mrema alisema kuwa wanasiasa hao wako mjini humo kwa ajili ya kufanya vikao na wabunge wa Ukawa ili kuweka mkakati na msimamo dhidi ya hoja mbalimbali zinazotarajiwa kuibuliwa katika vikao vya Bunge vinavyoanza kesho.

Moja kati ya hoja zinazotarajiwa kuwekewa msimamo ni pamoja na kuupinga muswada wa huduma za habari unaotarajiwa kujadiliwa na kupitishwa kuwa sheria.

“Tutakuwa na kikao cha kuweka msimamo wetu dhidi ya muswada hatari wa huduma za habari,” Mrema anakaririwa. “Vikao vimeshaanza na vitaendelea kesho (leo),”aliongeza.

Kwa mujibu wa Mrema, mbali na Lowassa, Sumaye na mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe, vigogo wengine wa Ukawa waliohudhuria vikao hivyo ni pamoja na Profesa Mwesiga Baregu, Profesa Abdallah Safari na Arcado Ntagazwa.

No comments: