Advertisements

Monday, October 31, 2016

SERENGETI NA BUNDA WANUFAIKA NA UWEKEZAJI WA SINGITA GRUMETI.

Mkurugenzi wa Singita Grumeti Stephen Cunliffe (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa msaada wa madawati 500 yenye Thamani ya Tshs Milioni 112 kwa ajili ya Wilaya za Serengeti na Bunda katika hafla iliyofanyika Shule ya Msingi Makundusi Wilayani Serengeti.
Mkurugenzi wa Singita Grumeti Stephen Cunliffe (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa nyumba ya kuishi mwalimu yenye thamani ya Tshs Milioni 86 iliyojengwa katika Shule ya Msingi Makundusi Wilayani Serengeti.
Mkuu wa Huduma za Jamii Singta grumeti Richard Ndaskoi (kulia) akimkabidhi Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa msaada wa madawati 500 yenye Thamani ya Tshs Milioni 112 kwa ajili ya Wilaya za Serengeti na Bunda katika hafla iliyofanyika Shule ya Msingi Makundusi Wilayani Serengeti
Madawati yaliyotolewa na Mfuko wa Singita Grumeti kwa ajili ya Wilaya ya Bunda.


Mfuko wa Singita Grumeti umeendelea kuwa mstari wa mbele katika kuboresha hali ya elimu katika Wilaya za Serengeti na Bunda.

Hii imedhihirika kwenye halfa ya kukabidhi madawati 500 kwa Mkuu wa Mkoa wa Mara Dk. Charles Mlingwa ili kupunguza uhaba wa madawati katika Wilaya hizo. Aidha Grumeti wamekabidhi nyumba ya kuishi mwalimu iliyojengwa katika Shule ya Msingi Makundusi.

“Tuko hapa kukabidhi madawati haya 500 yenye thamani ya Tshs Milioni 112 kwa Wilaya za Serengeti na Bunda pamoja na nyumba hii yenye thamani ya Tshs Milioni 86” alisema Richard Ndaskoi ambae ni Mkuu wa Huduma za Jamii toka Mfuko wa Singinta Grumeti.

Akipokea misaada hiyo, Dk. Mlingwa alisema “Nawashukuru Singita Grumeti kwa Msaada huu wa madawati pamoja na nyumba hakika mchango wenu katika Mkoa wa Mara unaoneka” Dk Mlingwa amewataka wawekezaji wengine katika Mkoa wa Mara kuchangia madawati katika Wilaya za Serengeti na Bunda kwani bado zina uhaba wa madawati. 

Aidha Dk. Mlingwa ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Serengeti kwa kuwa na mahusiano mazuri na wawekezaji waliopo katika Wilaya hiyo “Tukiwawekea mazingira mazuri ya kufanya shughuli zao hata wananchi pia watanufaika na uwepo wa wawekezaji hawa” alisema Dk. Mlingwa. 

Naye Mkuu wa Wilaya ya Serengeti, Nurdin Babu pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bunda, Lydia Bupilipili wote kwa nyakati tofauti wameushukuru Mfuko wa Singita Grumeti kwa msaada huo wa madawati na kuuomba mfuko huo kuendelea kuchangia katika shughuli za maendeleo katika Wilaya za Serengeti na Bunda. “Wilaya hii ina wawekezaji wengi lakini wamekuwa nyuma katika kuchangia shughuli za maendeleo, nawapongeza kwa kuwa mstari wa mbele kusaidia jamii inayowazunguka pamoja na kuchangia katika maendeleo ya Wilaya ya Serengeti” alisema Nurdin Babu.

Aidha Bi. Bupilipili ameuomba Mfuko huo kuanzisha kampeni maalumu ya kuongeza kiwango cha ufaulu kwa watoto wa kike kwa shule za sekondari Wilayani Bunda.

Singita Grumeti wamekuwa wawekezaji wenye tija kwa wananchi wa Wilaya za Serengeti na Bunda licha ya kuwa mstari wa mbele kuchangia katika shughuli za maendeleo, kampuni hiyo pia imekuwa ikitoa ajira kwa wakazi toka wilaya hizo mbili pamoja na kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi toka wilaya hizo.


ENGLIBERT THOMAS KAYOMBO
AFISA HABARI NA MAHUSIANO
HALMASHAURI YA WILAYA YA SERENGETI
0763878804

No comments: