Kigoma. Jeshi la Polisi mkoani Kigoma limemuua mtu mmoja anayedaiwa kuwa jambazi na kukamata bunduki moja aina ya SMG, magazini saba, maski tisa na risasi 275 baada ya kupambana ana kwa ana na mtu huyo katika Kijiji cha Uvinza wilayani Uvinza.
Kamanda wa Polisi mkoa wa Kigoma, kamishna msaidizi wa Polisi (DCP) Ferdinand Mtui amesema tukio hilo lilitokea Oktoba 14 na kumtaja jambazi huyo kuwa ni Yahya Kamuhanda (49) ambaye ni mkazi wa Kijiji hicho cha Uvinza, pia akiwa na makazi mengine katika Kijiji cha Lukole katika wilaya ya Ngara mkoani Kagera.
Polisi walipata taarifa kutoka kwa raia wema juu ya mikakati ya Kamuhanda kujiandaa kufanya uhalifu, ndipo waliweka mtego wa kumkamata katika eneo la Uvinza madukani ambapo jambazi huyo alikuwa anakwenda kununua mahitaji.
“Jambazi huyo alipofika madukani aligundua kuna Polisi wanamfuatilia kwa nyuma ndipo alitimua mbio kukwepa mkono wa dola, ikabidi Polisi wakishirikiana na raia waanze kumkimbiza.
“Huyo jambazi aliamua kurusha bomu la mkono ili ajiokoe na Polisi mmoja na raia watano walijeruhiwa vibaya katika sehemu mbalimbali za miili yao,” alisema Mtui.
Aliwataja waliojeruhiwa ni Askari Polisi F.3187 D/CPL Isaya. Wengine wananchi wa kawaida ambao ni Saidi Mohamed, Seleman Kashali, Joseph Daudi na Hassan Nasibu, wote ni wakazi wa Kijiji cha Uvinza waliokuwa wamejitokeza kusaidia harakati za kupambana na majambazi.
No comments:
Post a Comment