Advertisements

Monday, October 31, 2016

Serikali yakanusha kuuza kisiwa

SERIKALI imewahakikishia wakazi wa Wilaya ya Mafia na Watanzania wote kuwa Kisiwa cha Shungi Mbili kilichopo wilayani humo mkoani Pwani, hakijakodishwa wala kuuzwa kwa mtu yeyote kama inavyodaiwa na baadhi.

Badala yake, serikali imeingia mkataba na mwekezaji kwa ajili ya kufanya biashara ya hoteli ya kitalii ya hadhi ya nyota tano katika kisiwa hicho kwa kipindi cha miaka 20, uwekezaji ambao una manufaa zaidi kwa wananchi na serikali kwa ujumla.

Akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa hoteli hiyo iliyopewa jina la Thanda, Meneja Mkuu wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu nchini, Dk Milali Machumu alisema mwekezaji huyo ameingia mkataba huo na serikali kufanya biashara hiyo ikiwa ni sehemu ya kukiendeleza Kisiwa cha Shungi Mbili ambacho kilikuwa hakikaliwi na watu.

“Mimi niwahakikishie tu Watanzania kwamba serikali iliyoko madarakani chini ya Rais John Pombe Magufuli ipo makini na hizo tetesi za kuuzwa kwa kisiwa hiki mzipuuze, kwani kama mnavyoona pamejengwa hoteli ya kitalii kwa makubaliano na serikali na sio kuuzwa wala kukodishwa,” alisema Dk Machumu.

Alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo kutainufaisha serikali kwa kupata mapato kupitia kodi na kutengeneza ajira kwa wakazi wa Mafia pamoja na kuchochea maendeleo na pia wamezingatia sheria ya utunzani wa mazingira ya baharini.

Mkuu wa Wilaya ya Mafia, Shaibu Nunduma alisema kufunguliwa kwa hoteli hiyo kumetoa fursa nzuri ya ajira kwa wakazi wake na pia kutachochea kasi ya maendeleo kwa wilaya hiyo.

Mkurugenzi Mkuu wa hoteli hiyo, Pierre Delvaux aliishukuru serikali kupitia kwa Meneja wa Hifadhi za Bahari na Maeneo Tengefu, Dk Machumu kwa kuwezesha uwekezaji huo, ambao machakato wake ulianza miaka 10 iliyopita.

Delvaux alisema hoteli hiyo ina vyumba vitano vya kulala, bwawa la kuogelea, maeneo ya michezo kama tenisi pamoja na vitu vyote vya kufurahisha na gharama yake ni Dola za Marekani 10,000 (sawa na zaidi ya milioni 20) kwa usiku mmoja.

Pia alisema wamezingatia manufaa kwa wakazi wa Mafia na hivyo kwa upande wa ajira asilimia 65 itakuwa ni kwa wakazi wa kisiwa hicho.

“Leo tumeizindua rasmi hoteli hii, lakini itaanza kufanya kazi katikati ya Novemba mwaka huu,” alisema Delvaux.

Kisiwa cha Shungi Mbili ambacho ni sehemu ya Wilaya ya Mafia mkoani Pwani ni miongoni mwa visiwa 15 ambavyo ni maeneo tegefu vilivyopo katika Bahari ya Hindi na hairuhusiwa kufanya shughuli yoyote ya uvuaji wa samaki.

HABARI LEO

1 comment:

Anonymous said...

Imejengwa kwa manufaa ya wananchi? Hoteli ya vyumba vitano? Itaajiri watu wangapi? Hiyo ni hoteli au nyumba binafsi?