Advertisements

Monday, October 3, 2016

TANESCO DODOMA YAOMBA KUPEWA HADHI YA MKOA MAALUM

MENEJA wa Shirika la Ugavi wa Umeme Tanzania (TANESCO) mkoa wa Dodoma, Mhandisi Zakayo Temu amesema ni vema mkoa huo ukapewa hadhi ya mkoa maalum ili uweze kukabiliana na changamoto za ujio wa Serikali Dodoma. 


Ametoa ombi hilo jana jioni (Jumapili, Oktoba 2, 2016) wakati akitoa taarifa ya utendaji wa TANESCO Mkoa wa Dodoma mbele ya Waziri Mkuu Kassim Majaliwa ambaye alifika kwenye kituo cha kupozea umeme cha Zuzu nje kidogo ya mji wa Dodoma, kukagua mahitaji halisi ya umeme ikilinganishwa na ujio wa watumishi mkoani humo. 

Mhandisi Temu alisema: “Tunaomba mkoa wetu wa Dodoma ambao ni Makao Makuu uangaliwe kwa jicho la pekee na kupewa hadhi ya mkoa maalum kama ilivyo kwa Dar es Salaam ambako kuna mikoa minne ya ki-TANESCO.” 


“Dar es Salaam ina mikoa minne ya Ilala, Kinondoni, Temeke na Mikocheni. Mkoa wetu unatakiwa kubeba majukumu yote ya Serikali kama yanavyofanyika hivi sasa katika Jiji la Dar es Salaam. Hivyo, tunaomba tupewe kipaumbele kwenye rasilmali watu, usafiri na vitendea kazi,” alisema. 

Alisema TANESCO inabidi iende kwa kasi zaidi ili kumudu wimbi la wafanyakazi wanaohamia Dodoma. 

Akifafanua kuhusu uboreshaji wa miundombinu iliyopo, Mhandisi Temu alisema kukamilika kwa njia ya kusafirisha umeme wa kilovolti 400 kutoka Iringa mpaka Shinyanga kupitia Dodoma, kumeboresha upatikanaji wa umeme kwenye mji wa Dodoma. 

“Umeme unapatikana ukiwa na voltage nzuri na hauchezichezi na hivi sasa tatizo la kukatika kwa umeme mara kwa mara limepungua kwa kiasi kikubwa. Kukamilika kwa njia hii kunaleta uwezekano wa kufanya matengenezo kwenye njia moja ya umeme bila kuathiri upatikanaji wa umeme kama ilivyokuwa awali,” alisema. 

Alisema kazi inayoendelea hivi sasa ni kubadilisha nguzo za umeme zilizochakaa; kubadilisha njia za msongo wa kilovolti 11 kwenda kilovolti 33 zenye urefu wa km. 85 na transforma 74 ili kupunguza upotevu wa umeme na kuingiza njia hizo kwenye njia mpya ya 132/33kV katika maeneo ya manispaa ambayo yanapata umeme kupitia njia za 11kV. 

Alisema mbali ya kusambaza umeme kwa njia ya mzunguko wa mji (ring circuit), wataongeza vituo vikubwa viwili vya kupozea umeme katika maeneo ya Msalato na Kikombo. 

Mhandisi Temu alisema wameanza kuboresha miundombinu ya umeme ili kuwezesha baadhi ya wilaya za mipakani zipate umeme kutoka mikoa ya jirani wakati wa matengenezo au kukiwa na hitilafu za umeme. 

“Tunapanga wilaya ya Gairo ipate umeme kutoka Morogoro; Bahi ipate umeme kutoka Manyoni; Mpwapwa hasa maeneo ya Chipogolo yapate umeme kutoka Ruaha Mbuyuni ambako ni karibu zaidi. Pia tunataka wilaya ya Kiteto ipate umeme kutoka Dodoma badala ya Babati kama ilivyo hivi sasa,” alisema. 

Alimhakikishia Waziri Mkuu kwamba umeme unaozalishwa na kituo cha Zuzu unatosha mahitaji ya sasa na hata baadaye kwani wanazalisha megawati 48 wakati mahitaji ya juu ni megawati 25 na hivyo kubakiwa na ziada ya megawati 23. 

Wakati huohuo, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa aliwaagiza viongozi wa TANESCO mkoa wa Dodoma wahakikishe wanapeleka miundombinu ya umeme kwenye maeneo yanayopimwa viwanja ili wanaonunua wakute huduma hiyo ipo tayari. 

“Nimeongea na watu wa idara ya maji, nimewaambia wapeleke miundombinu yao katika maeneo yanayopimwa viwanja. Na ninyi pia mfanye hivyo kama ambavyo watu wa TAMISEMI walijenga barabara za lami katika viwanja vipya vya makazi ili watu wakienda kununua wakute huduma hiyo ipo tayari,” alisema. 

“Nimefarijika kukuta kwamba Dodoma hatuna shida ya umeme, hatuna mgao, kwa hiyo endelezeni kazi hii nzuri mnayoifanya,” alisema Waziri Mkuu. 

IMETOLEWA NA: 

OFISI YA WAZIRI MKUU, 
S. L. P. 980, 
DODOMA. 
JUMATATU, OKTOBA 3, 2016.

No comments: