Advertisements

Tuesday, November 8, 2016

Chadema kortini saa 7 kumsubiri Lema

WAFUASI wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wamekaa kwa muda wa saa saba wakimsubiri Mbunge wa Arusha Mjini, Godbless Lema kufikishwa Mahakama ya Hakimu Mkazi Arusha.

Wafuasi hao akiwemo Mwenyekiti wa chama hicho Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa na Mbunge wa Viti Maalumu, Joyce Mukya walikuwa wamekaa kwa saa kadhaa kumsubiri Mbunge huyo.

Walisubiri bila mafanikio huku saa za mahakama zikiwa zinayoyoma.

Lema ambaye hadi jana anasota mahabusu kwa siku ya sita sasa, hata hivyo ilipofika saa saa 8:52 mchana Wakili wa Mbunge Lema, John Mallya alisema inashangaza hadi sasa ni kwa nini Mbunge huyo alikuwa hajafikishwa mahakamani.

Mallya alisema Lema alikamatwa Jumatano iliyopita mkoani Dodoma na kuletwa hadi Arusha na amekaa mahabusu kwa zaidi ya saa 175 na ni kinyume cha haki za binadamu kwani Polisi wanapaswa kukaa na mshitakiwa kwa saa 24.

Alisema wamefungua kesi ya jinai namba 56/2016, ambayo ipo kwa Jaji Salma Magimbi ambaye atasikiliza kesi hiyo kesho asubuhi.

Katika kesi hiyo waliyofungua mahakamani hapo jana ni kutaka Lema aitwe mahakamani ili kesi yake ya msingi anayoshtakiwa nayo isomwe na mshitakiwa apate dhamana.

Pili wamemshtaki Mkuu wa Kituo cha Polisi, Mkuu wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (RCO), Kamanda wa Polisi (RPC), Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP) na Mwanasheria Mkuu wa Serikali ambao pia katika kesi hiyo waliyofungua, wakili Mallya anataka walipwe gharama za usumbufu wa kesi ikiwemo kufuatilia huku na kule ili Lema atoke.

Katibu wa Chadema Kanda ya Kaskazini, Amani Golugwa alidai utawala wa sheria unagandamizwa na sheria imekiukwa.

HABARI LEO

No comments: