Advertisements

Tuesday, November 8, 2016

Clinton na Trump wajinadi dakika za mwisho

Kura za maoni zinaonesha Bi Clinton anaongoza

Hillary Clinton na Donald Trump wamefanya mikutano ya dakika za mwisho mwisho kuwahimiza raia wa Marekani wawapigie kura zikiwa zimesalia saa chache kabla ya uchaguzi kufanyika.

Wote wawili wamefanya mikutano ya kampeni katika majimbo ya kushindaniwa ya Carolina Kaskazini, Pennsylvania na Michigan.

Bi Clinton amewahimiza wapiga kura kuunga mkono kuwepo kwa "Marekani yenye matumaini, inayojumuisha wote na yenye ukarimu".

Bw Trump naye amewaambia wafuasi wake kwamba wana "fursa nzuri ya kuvunja mfumo mbovu na usio na maadili".

Kura za maoni zinaonesha Bi Clinton wa chama cha Democratic akiwa asilimia nne mbele ya mpinzani wake Bw Trump wa chama cha Republican.
Obama asikitishwa na Trump
Trump v Clinton: Nani anaongoza?
Mwanamke mwingine aliyedhalilishwa na Trump

Wapiga kura wengi kuliko awali, zaidi ya 46 milioni, tayari wamepiga kura za mapema.

Kuna ishara za wapiga kura wa asili ya Kihispania (Latino/Mexico) kujitoleza kwa wingi, jambo ambalo wengi wanaamini litamfaa Bi Clinton.

Uchaguzi mkuu unafanyika baada ya kampeni kali ambapo wapiga kura walirushiana matusi na kila mmoja alikabiliwa na kashfa.

Kwenye hafla Philadelphia, Pennsylvania, Bi Clinton ameungana na nyota Bruce Springsteen na Jon Bon Jovi jukwaani pamoja na mumewe Bill, Rais Obama na mkewe Michelle.

Bw Obama amewataka wapiga kura kukataa kutawaliwa na woga na badala yake waamue kukumbatia matumaini

Mkutano wa mwisho wa kampeni wa Bi Clinton ulikuwa Raleigh, Carolina Kaskazini, ambao angemshirikisha Lady Gaga.

Awali, alisema kwenye mahojiano redioni kwamba akishinda atampigia simu Bw Trump na kwamba anatumai mgombea huyo wa chama cha Republican anaweza "kutekeleza mchango muhimu" katika kuunganisha tena taifa hilo.
Mke wa Trump amnadi mumewe
Obama: Trump hafai kuwa rais

Bw Trump, kwenye mkutano wake wa kampeni mjini Scranton katika jimbo hilo alisisitiza kwamba kampeni yake imekuwa ikiimarika.

Mkutano wake wa mwisho ulikuwa Grand Rapids, Michigan.

Awali, aliwaambia wafuasi wake jimbo la Florida kwamba yeye "si mwanasiasa" na kwamba anawajali wao pekee.

Mfanyabiashara huyo alimweleza Bi Clinton kama "mtu mwovu zaidi aliyewahi kuomba kuchagulikuwa kuwa rais", akirejelea uchunguzi wa FBI kuhusu hatua ya Bi Clinton ya kutumia sava ya kibinafsi ya barua pepe kutuma barua pepe rasmi alipokuwa waziri wa mambo ya nje kati ya 2009 na 2013.





Jumapili, Bi Clinton alipata nafuu baada ya FBI kusema barua pepe mpya zilizokuwa zimegunduliwa kwenye uchunguzi mwingine hazikutoa ushahidi wowote wa kumpata na hatia.

Hayo yakijiri, meneja wa kampeni wa Bw Trump, Kellyanne Conway amepuuzilia mbali wasiwasi miongoni mwa jamii ya kimataifa kuhusu uwezekano wa mgombea huyo wa Republican kushinda.

Akiongea na BBC Jumatatu, alisema ukosoaji ambao umekuwa ukitoka nje ya nchi "hauashirii sifa halisi za Donald Trump na sababu zinazomfanya awanie urais na sifa atakazokuwa nazo jukwaa la kimataifa akishinda".

Rais wa Ufaransa Francois Hollande alikuwa amesema bilionea huyo humfanya "ahisi kutapika".
Trump alalamika FBI kumuondolea makosa Clinton
Obama: Mustakabali wa dunia utakuwa kwenye mizani

Bw Trump amekabiliwa na shutuma kali hasa kutokana na madai ya kuwadhalilisha kingono wanawake, madai ambayo Bw Trump ameyakanusha.

Aidha, kuna kadha zilizotolewa zikimuonesha akitoa matamshi ya kuwadhalilisha wanawake. Bw Trump alisema mazungumzo hayo yalikuwa ya mzaha na ya faraghani.

Bw Trump pia ametuhumiwa kwa kueneza chuki dhidi ya wageni baada ya kuapa kuwapiga marufuku Waislamu wasiingie Marekani kwa muda kama njia ya kukabiliana na ugaidi.

Aliwaeleza raia wa Maexico kuwa "wabakaji" na kadhalika, alisema angejenga ukuta kwenye mpaka wa Marekani kuwazuia Wamarekani wasiingie nchini humo.

BBC

No comments: