Advertisements

Sunday, November 13, 2016

HOJA SITA ZILIVYOTIKISA BUNGE

Licha ya Mkutano wa Tano wa Bunge uliomalizika juzi kuwa mahsusi kwa ajili ya kamati za kudumu kuwasilisha taarifa za hesabu ambazo aghalabu hufuatiwa na mijadala mizito hasa ya ufisadi, safari hii haikuwa hivyo, badala yake hoja sita tofauti na hizo ndizo zilizotikisa vikao vyake.
Mkutano huo uliofanyika kwa siku 10 na kumalizika juzi, pamoja na mambo mengine ulikuwa mahsusi kwa ajili ya kamati hizo kuwasilisha taarifa zao kuhusu hesabu zilizokaguliwa na Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) kwa mwaka wa fedha wa 2013/14 na 2014/15 ambazo safari hii zilipewa umuhimu mdogo ikilinganishwa na mikutano iliyopita.
Kamati zilizowasilisha taarifa zao ni ya Hesabu za Serikali (PAC) na Hesabu za Serikali za Mitaa (Laac) ambazo licha ya kuibua kashfa kama ya Mfuko wa Taifa wa Hifadhi ya Jamii (NSSF) katika Mradi wa Kigamboni na ukopeshaji wa vikundi vya kuweka na kukopa (Saccos), mradi wa vifaa vya utambuzi wa vidole uliokuwa ukifanywa na Kampuni ya Lugumi kwa Jeshi la Polisi na utata wa mizigo kwenye Mamlaka la Bandari Tanzania (TPA), hayakuonekana kupewa umuhimu mkubwa katika mijadala bungeni.
Mambo mengine ambayo hayakupewa umuhimu katika mkutano huo wakati wa majadiliano ni kashfa ya mradi wa Shirika la Usafiri Dar es Salaam (Uda) na mradi wa machinjio wa jiji la Dar es Salaam. Lakini kuna mambo ambayo yalipewa kipaumbele.


Ukata bungeni             
Wabunge wengi wakiwamo wa CCM na wale wa upinzani katika michango yao walijikita zaidi katika hali ya uchumi inayowakabili wananchi pamoja na Bunge lenyewe wakisema hali hiyo imewafanya washindwe kufanya shughuli za ukaguzi wa miradi na taasisi za umma.
Mbunge wa Mpwapwa (CCM), George Lubeleje alisema ni aibu kwa wabunge kukaa kwenye kamati na kusubiri kuletewa taarifa za miradi na maofisa wa Serikali badala ya wao kwenda kuikagua ili kujiridhisha na kile walichoambiwa “Hivi ni nani aliyeua mfuko wa Bunge? Hiki tunachokifanya hapa ni kuisimamia Serikali au kupitisha tulicholetewa na maofisa wa Serikali? Hii si sawa hata kidogo ni lazima tuikatae hali hii,” alisema.
Hoja hiyo, iliungwa mkono na Mbunge wa Tarime Vijijini (Chadema), John Heche akisema hata kamati zinazokaa hadi usiku zimekuwa zikikosa huduma ya maji ya kunywa.

Mikopo
Wabunge pia walivutana na Serikali kuhusu muda wa urejeshwaji wa mikopo ya elimu ya juu kwa wanafunzi walionufaika katika Muswada wa Marekebisho ya Sheria mbalimbali Namba 3 wa mwaka 2016. Katika muswada huo, Serikali iliwataka wanafunzi hao kuanza kulipa, mwaka mmoja baada ya kumaliza au kukatika masomo yao.
Katika mvutano huo ambao wabunge wa pande zote mbili yaani wa CCM na wa upinzani walizungumza lugha moja na Serikali ililazimika kuongeza hadi miaka miwili kwa mnufaikaji wa mikopo hiyo kuanza kufanya marejesho.
Mbunge wa Ukonga (Chadema), Mwita Waitara ndiye aliyepeleka mapendekezo akitaka Serikali kuongeza muda wa wanufaika hao kuanza kulipa mkopo.
Alisema kinyume chake, wanufaika kutoka familia maskini watashindwa kulipa mikopo hiyo kwa muda huo uliowekwa.
Hoja ya Waitara iliungwa mkono na Mbunge wa Kigoma Mjini (ACT - Wazalendo), Kabwe Zitto, Ridhiwani Kikwete (Chalinze - CCM), Ester Matiko (Tarime Mjini - Chadema), Elibariki Kingu (Manyoni Magharibi - CCM) na Fratei Massay (Mbulu Vijijini - CCM).

Uzoefu wa ma-DED
Wabunge pia waliibua mjadala wa uteuzi wa wakurugenzi watendaji wa halmashauri (DED) na watumishi wengine katika Awamu ya Tano wasiokuwa na uwezo wa kuongoza maeneo waliyochaguliwa.
Baadhi ya wabunge walisema wakurugenzi hao walichaguliwa kutoka maeneo tofauti bila kuzingatia Sheria ya Utumishi wa Umma na uzoefu walionao katika utumishi huo hivyo kushindwa kuelewa majukumu yao na kujikuta wakivuka mipaka yao ya kazi na wakati mwingine kutokuwa na ushirikiano na watumishi.
Mbunge wa Rombo (Chadema), Joseph Selasini alisema wengi wao hawana uwezo wala uelewa wa shughuli za Serikali kwa kuwa hawakuwahi kufanya kazi huko na walipochaguliwa hawakupewa semina yoyote.
Hoja yake iliungwa mkono na Mwenyekiti wa Laac, Vedasto Ngombale aliyesema kamati yake imebaini maofisa wa idara na vitengo kwa baadhi ya halmashauri kutokuwa na uwezo wa kutosha kutekeleza majukumu yao.
“Kamati imeshuhudia wakuu wengi wa idara na vitengo wakishindwa kutoa majibu sahihi na kamilifu mbele ya kamati na kushindwa kuelewa shughuli zinazofanyika ndani ya idara zao,” alisema.

Tuhuma ya Sh10 milioni
Madai ya wabunge wa CCM kupewa Sh10 milioni kila mmoja ili wapitishe Muswada wa Huduma za Habari wa mwaka 2016 na Mapendekezo ya Mpango wa Maendeleo kwa mwaka wa Fedha 2017/18, ni moja ya mambo yaliyotikisa Bunge.
Tuhuma hizo ziliibuliwa na Kiongozi wa Kambi ya Upinzani, Freeman Mbowe wakati akimuuliza swali Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa.
Madai hayo yalisababisha Muswada wa Sheria ya Huduma za Habari wa Mwaka 2016, tofauti na miswada mingine ya sheria inayokuja bungeni kutawaliwa na vijembe baina ya wabunge wa upinzani na chama tawala.
Mwenyekiti wa Kamati ya Huduma ya Jamii, Peter Serukamba alisema hakuna mbunge aliyechangia vifungu vya muswada huo ambaye alilenga katika kupinga vifungu vya muswada huo na badala yake walijikita katika vijembe tu.
“Mkitaka kujua muswada huu ni mzuri sikilizeni, hakuna mtu alipinga vifungu kama yupo mtu asimame wote mliamua kucheza katika siasa tu. Lakini kwa maana ya sheria yenyewe hakuna mtu aliyeweka neno kwa sababu kila kitu kimefanywa,” alisema Serukamba.
Mbunge wa Viti Maalumu (CCM), Juliana Shonza alirushiana maneno na Halima Mdee (Kawe – Chadema) aliyemtamkia maneno ‘milioni 10 hizo’ baada ya kuelezea kukerwa kwake na watu wanaoingilia utendaji wa vyombo vya habari.

Kauli moja ya Epa
Kuhusu Mkataba wa Ushirikiano wa Kiuchumi kati ya Jumuiya ya Ulaya na Afrika Mashariki (Epa), wabunge wote waliungana kuipinga Serikali wakisema hauna na masilahi kwa Taifa.
Mbunge wa Sikonge (CCM), Joseph Kakunda alisema mkataba huo una kila dalili ya kuirudisha nchi katika ukoloni kwa sababu vifungu vyake kwa zaidi ya asilimia 80 ni vya ukandamizaji.
Spika, Job Ndugai alipigilia msumari wa mwisho aliposema kwamba haufai.

CAG
Pia, wabunge wengi walizungumzia suala la CAG kutengewa kiasi kidogo cha fedha katika mwaka wa bajeti wa 2016/17 jambo ambalo litamfanya akague taasisi chache na hivyo kuwapa ugumu wabunge kuisimamia Serikali.




No comments: