Ivo Mapunda ambaye ni golikipa wa zamani wa timu ya taifa ya Tanzania na vilabu vikongwe nchini vya Simba na Yanga ameamua kurejesha uwezo wake uwanjani kwa kuwajenga vijana wadogo kwa kwa ajili ya siku za baadaye baada ya kuanzisha kituo chake cha kuibua vipaji maeneo ya Kitunda-Mwanagati.
Mapunda ambaye kwa sasa hachezi mechi za kiushindani tangu alipoachwa na Azam FC baada ya mkataba wake wa muda mfupi kumalizika amekuwa nyumbani tangu kuanza kwa msimu huu wa VPL 2016-17.
Golikipa huyo aliyepata kucheza soka la kulipwa kwenye vilabu vya Ethiopia na Kenya kabla ya kurejea tena Tanzania amesema, lengo la kuanzisha kituo hicho ni kusaidia vijana ambao hawana kazi za kufanya na huenda ikawa ni fursa kwao kupata ajira kupitia vipaji vyao.
“Nimeandaa ufunguzi wa kituo changu cha michezo kitakuwa kinaitwa Ivo Mapunda Sports Center, ni kituo ambacho kitakuwa kinachukua vijana wadogo kuanzia miaka 5 hadi 18 na hii nimeifanya ili kujaribu kuibua vipaji kwa watoto wadogo kwasababu sasahivi limekuwa tatizo kwa vijana kupata ajira na sehemu za kucheza,” anasema golikipa huyo wa zamani wa Taifa Stars aliyepata kuvitumikia vilabu vya Simba na Yanga kwa nyakati tofauti.
“Kwa eneo ambalo nakaa mimi nimeona kuna vijana wengi ambao hawana shughuli za kufanya sasa nimeamua nifungue hiki kituo kuwapa fursa ya kuonesha vipaji vyao. Tayari nimeshapata eneo kutoka serikali za mitaa na natarajia kufanya ufunguzi rasmi Novemba 26 mwaka huu siku ya Jumamosi ijayo,” alifafanua Mapunda ambaye amesema kituo kitakuwa Kitunda-Mwanagati.
“Utaratibu wa namna ya kujiunga utafahamika siku hiyohiyo ya ufunguzi pamoja na mambo mengine mengi.”
Tangu Ivo alipomaliza mkataba wake na Azam hajatangaza kustaafu soka la ushindani lakini huenda aliamua kustaafu kucheza soka bila kutangaza.
No comments:
Post a Comment