Advertisements

Monday, November 14, 2016

KIDATO CHA PILI WAANZA MITIHANI LEO

Wanafunzi wa kidato cha pili nchini wameanza kufanya mitihani yao ya upimaji leo katika shule za sekondari 4,669 zilizopo Tanzania Bara.

Jumla ya wanafunzi 435,221 wamesajiliwa kufanya mitihani hiyo wakiwamo 67 wasioona na 306 wenye uoni hafifu.

Mbali na mitihani hiyo, Katibu Mtendaji wa Baraza la Mitihani la Taifa (Necta), Dk Charles Msonde amesema mtihani wa Taifa wa darasa la nne utafanyika Novemba 23 na 24, mwaka huu.

"Mitihani hii inafanyika katikati ya mafunzo ili kubaini changamoto zilizopo na kutafuta namna ya kuboresha mafunzo hayo," amesema Dk Msonde.                      


Wakati huo huo, Dk Msonde amefafanua kuwa mafunzo ya ualimu wa shule ya msingi ngazi ya stashahada yamefutwa lakini wanafunzi waliopo vyuoni watamalizia masomo yao kwa muda uliobaki.

Dk Msonde amesema mafunzo hayo ya walimu yataendelea kwa utaratibu wa zamani ambao ulikuwa ngazi ya cheti.

Amesema usimamizi wa mitihani hiyo itakuwa chini ya Necta kama ilivyokuwa zamani badala ya Nacte.

"Wanafunzi walio vyuoni wataendelea na mafunzo hayo, isipokuwa kuanzia mwaka huu hatutadahili kwa ngazi ya diploma, tutadahili ngazi ya cheti kama ilivyokuwa zamani," amesema Dk Msonde. 

No comments: