ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, December 20, 2016

BALOZI SEIF - KUKAMILIKA KWA UWANJA WA NDEGE WA KIMATAIFA WA ABEID AMAN KARUME KUTAKUZA UCHUMI WA NCHI

 Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kushoto akizungumza na Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya BCEG Mhandisi Fan Jun  Kushoto kwenye Makao Makuu ya Kampuni hiyo Jengo la Jian Going laza Mjini Beijing Nchini China.
 Meneja Mkuu wa Shirika la Bima la China (SINO SURE) Bwana Wu Han Kulia akibadilishana mawazo na Balozi Seif mara baada ya kumalizika kwa mazungumzo yao Mjini Beijing.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif wa Pili kutoka Kushoto akiwa na Ujumbe wake akizungumza na Uongozi wa Shirika la Bima la China (SINO SURE) Mjini Beijing akimalizia ziara ya siku Tano Nchini China.
  Balozi Seif Kati kati walioko mbele akiwa katika picha ya pamoja na Uongozi wa Juu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya BCEG mara baada ya kumaliza mazungumzo yao ya ushirikiano. Kushoto ya Balozi Seif ni Naibu Meneja wa Kampuni ya BCEG Bwana Yongchun Chang, Waziri wa Fedha na Mipango wa Zanzibar DSr.id Salum Mohamed, Katibu Mkuu wake Nd. Khamis Mussa, wakati upande wa kulia ya Balozi Seif ni Meneja Mkuu wa Kampuni ya BCEG Mhandisi Fan Jun na Naibu Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Usafirishaji Zanzibar Mh. Mohamed Ahmed Salum na Msaidizi Meneja wa BCEG wa masuala ya Kimataifa Bwana Shulong Ma. Picha na –OMPR – ZNZ.



Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema kumalizika kwa ujenzi wa uwanja wa ndege wa Kimataifa wa Abeid Aman Karume  ni mwanzo wa safari ndefu ya mafanikio  kwa Zanzibar katika azma yake ya kuitumia Sekta ya Utalii kuwa muhimili wa Uchumi Mkuu wa Visiwa vya Zanzibar.
Alisema azma hiyo ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar imelenga kutafuta njia nyengine mbadala za kukuza uchumi wake na mapato ya Taifa ambayo kwa sasa yanaendelea kutegemea zao moja tu la karafuu.
Balozi Seif Ali Iddi alitoa kauli hiyo wakati akizungumza na Uongozi wa juu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi { BCEG } ambayo ndio inayojenga  eneo la maegesho ya Ndege kwenye Uwanja wa ndege wa Zanzibar kwenye Makao Makuu yake Jengo la Jian Geing laza Mjini Beijing Nchini China.
Akimalizia ziara yake ya siku Tano Nchini Jamuhuri ya Watu wa China akiuongoza Ujumbe wa Viongozi Wanne wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Balozi Seif  alisema ongezeko la idadi ya Watalii wanaoingia Zanzibar kwa sasa ni vyema ikaenda sambamba na uimarishwaji wa sekta hiyo muhimu kwa wakati huu.
Balozi Seif aliueleza Uongozi huo wa juu wa BCEG ukiongozwa na Meneja Mkuu wa Kampuni hiyo Bwana  Fan Jun kwamba Kampuni na Taasisi za ujenzi za China kutokana na umakini wake katika kazi zitaendelea kushirikishwa na Serikali katika uimarishaji wa miundombinu tofauti ya Maendeleo.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliwapongeza  watendaji na Uongozi mzima wa Kampuni ya Ujenzi ya BCEG kwa kazi kubwa wanayotekeleza katika ujenzi wa miradi  mikubwa ya mawasiliano akiitolea mfano ile ya Bandari na Viwanja vya Ndege.
Balozi Seif alifahamisha kwamba Wananchi wa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla wameshuhudia uweledi mkubwa  wa wahandisi wa Kampuni hiyo katika uwajibikaji wao kitendo ambacho  kinatoa fursa kwa Kampuni hiyo kuendelea kuaminiwa na hatimae kupewa miradi mipya kwa ajili ya ujenzi.
Naye Waziri wa Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed  alisema Zanzibar  bado ni changa katika muelekeo wake wa kujiwezesha Kiuchumi na ustawi wa maendeleo ya Wananchi wake.
Dr. Khalid alisema juhudi kubwa zinazofanywa  na Makampuni na Taasisi za masuala ya uwekezaji kutoka Nchini China hasa katika miradi ya ujenzi wa miundombinu zinahitajika kusaidia nguvu za Serikali kuelekea katika malengo iliyojipangia.
Mapema Meneja Mkuu wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya Nchini China Bwana Fan Jun alisema Taasisi hiyo iliyoasisiwa mwaka 1963 ikiwa miongoni mwa Makampuni makubwa Duniani itaendelea kuiunga mkono Zanzibar katika miradi yake ya Maendeleo.
Bwana Fan alisema  Kampuni ya BCEG  yenye wataalamu na wafanyakazi wasiopungua  22,000 imeanza kuingiza Tanzania  mnamo Mwaka ya 1970  ikihusika na mradi wa  ujenzi wa Reli ya Tanzania na Zambia { TAZARA }.
“ Ndani ya Ardhi ya Tanzania Kampuni yetu tayari imeshashughulikia ujenzi wa miradi Mikubwa kama Ujenzi wa Bara bara, Viwanja vya Ndege Mwanza na ule Zanzibar, Daraja la Kigamboni Pamoja na Mji wa Kisasa unaojengwa nje ya Jiji la Dar es salaam”. Alisema Bwana Fan.
Alisema ushirikiano mzuri wa Kihistoria ulipo kati ya Tanzania na China chini ya waasisi wa Mataifa hayo  Mawili Marehemu  Mao Tsetung  na Hayati Mwalimu Julius K. Nyerere  umeiwezesha Kampuni hiyo kuendelea kuaminiwa na hatimae kukubalika  kupewa miradi ya ujenzi Nchini Tanzania ukiwemo pia upande wa Zanzibar.
Meneja Mkuu huyo wa Kampuni ya Kimataifa ya Ujenzi ya BCEG aliuhakikisha Ujumbe huo wa Zanzibar kwamba Taasisi hiyo itakuwa tayari wakati wowote kutekeleza mradi wowote itakayokabidhiwa kwa vile tayari imeshafungua Tawi lake Mjini Dar es salaam.
Bwana Fan alifahamisha kwamba BCEG  Matawi ya Taasisi hiyo yamesambaa katika Mataifa 37 ulimwenguni ambapo katri ya hayo Matawi 27 yamo ndani ya Bara la Afrika.
Mapema asubuhi Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif na Ujumbe wake  alifanya mazungumzo na Uongozi wa Shirika la Bima la China Makao Makuu yake Mjini Beijing.
Katika mazungumzo yao Meneja Mkuu wa Shirika hilo { SINO SURE } Bwana Wu Han alisema Taasisi hiyo kupitia Serikali Kuu pamoja wa Wizara inayosimamia Bishara Nchini china imejiwekea utaratibu wa kusaidia udhamini kwenye miradi ya Maendeleo katika Mataifa marafiki Duniani hasa yale ya Bara la Afrika.
Bwana Wu  Han alisema Jamuhuri ya Watu wa China itatekeleza mpango maalum wa kusaidia Nchi changa katika azma ya kuona zinajikwamua Kiuchumi ikilenga maalum kwa Mataifa ya Bara la Afrika.




Othman Khamiks Ame
Ofisi ya Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar
20/11/2016.

No comments: