Advertisements

Saturday, January 7, 2017

BALOZI SEIF AWEKA JIWE LA MSINGI UJENZI WA UKUTA WA UKINGO WA BAHARI MIZINGANI FORODHANI

Waziri wa Fedha na Mipango Zanzibar Dr. Khalid Salum Mohamed kulia akimuongoza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi kwenda kuweka jiwe la msingi la Ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar.  Kulia ya Balozi Seif ni Kamishna wa Polisi Zanzibar Hamdan Makame.

Makamu wa Pili a Rais wa Zanzibar Balozi Seif akiweka jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ikiwa ni shamra shamra za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi ya Zanzibar. 
Wa kwanza kushoto ni Waziri wa Fedha na Mipango wa SMZ Dr. Khalid Salum Mohamed ambapo wa nyuma yake ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid.
Mandhari nzuri ya kuvutia ya muonekano wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ambapo ujenzi wake umewekwa jiwe la Msingi na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi.
Mkurugenzi Mtendaji wa Mamlaka ya Utunzaji na Uhifadhi wa Mji Mkongwe wa Zanzibar Nd. Issa Sarboko Makaran akimpatia maelezo Balozi Seif jinsi ya wajenzi wa Ukuta wa Kuzuia Maji ya Bahari Mizingani wanavyozingatia uhifadhi wa urithi wa Dunia uliomo ndani ya Mji Mkonhgwe.
Balozi Seif akizungumza na Wananchi katika hafla ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar.
Kikundi cha Utamaduni cha Cha Mkoa Mjini Mgharibi kikifanya vitu vyake wakati wa kutoa burdani kwenye hafla ya ya uwekaji wa jiwe la msingi la ujenzi wa Ukuta wa kuzuia maji ya Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar.
Balozi Seif akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi, wahandisi wa ujenzi wa ukuta, watendaji wa Wizara ya Fedha pamoja na washauri walekeza wa ujenzi huo mara baada ya kukamilisha kwa hafla hiyo.  Kulia ya Balozi Seif waliokaa vitini ni Spika wa Baraza la Wawakilishi Zanzibar Mh. Zubeir Ali Maulid, Katibu Mkuu Wizara ya Fedha Nd. Khamis Mussa, Kamishna wa Polisi Zanzibar Kamanda Hamdan Makame.  Kushoto ya Balozi Seif ni Waziri wa Fedha Dr. Khalid Salum, Mkuu wa Mkoa Mjini Magharibi Mh. Ayoud Mohamed Mahmoud na Waziri wa Habari, Utamaduni, Utalii na Michezo Mh. Rashid Ali Juma.  Picha na – OMPR – ZNZ.


 


Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema adha ya mafuriko yanayotokea kila mwaka wakati wa msimu wa Mvua za Masika na kuwakumba Wananchi yataondoka au kupungua zaidi baada ya kukamilika kwa miradi tofauti iliyonzishwa na Serikali chini ya Mradi wa huduma za Jamii Mijini.

Alisema mafanikio ya mradi huo tayari yameanza kuonekana katika ujenzi wa michirizi ya maji ya mvua kwenye maeneo ya Daraja Bovu, Mnazi Mmoja, Kijangwani na baadhi ya maeneo ya Jang’ombe na Wananchi wake tayari wanafaidika na matunda ya mradi huo.

Balozi Seif Ali Iddi alieleza hayo wakati wa hafla ya Uwekaji wa Jiwe la Msingi la Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ikiwa ni miongoni mwa harakati za shamra shamra za kusherehekea miaka 53 ya Mapinduzi Matukufu ya Zanzibar.

Alisema Serikali ya Mapinduzi imejipanga kuimarisha miradi hiyo ikiwa sehemu ya Jududi za utekelezaji wa Ilani ya uchaguzi ya CCM ya Mwaka 2015 ikilenga kuwaondoshea usumbufu unaowakumbwa wananchi walio wengi hasa wale wa maeneo ya Ng’ambo ya Mji.

Balozi Seif alisema ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar ukiwa miongoni mwa miradi ya Jamii Mijini ni muhimu kwa maendeleo ya Mji Mkongwe wa Zanzibar uliobahatika kuwemo kwenye Miji ya urithi wa Dunia ambao unategemewa kwa uchumi wa Taifa kwa upande wa Sekta ya Utalii.

Alifahamisha kwamba Ukuta huo pamoja na bara bara yake, njia ya waendao kwa miguu, na ujenzi wa Bustani ya Forodhani utabadilisha mazingira na mandhari ya eneo zima la Mizingani, Forodhani pamoja na Mji Mkongwe kwa ujumla utachochea kuimarika kwa shughuli mbali mbali za Kijamii na Kitalii.

Balozi Seif aliwaomba Wananchi katika maeneo mbali mbali nchini kuendelea kuwa na sura katika kipindi hichi cha mpito katika uimarishaji na ujenzi wa miundombinu hiyo iliyoelekezwa katika miradi yao ya Kijamii.

Hata hivyo Balozi Seif aliwanasihi Wananchi kufanya juhudi ya kuitunza miradi hiyo wakati itakapokamilika ujenzi wake kwa kuacha tabia ya kutupa taka taka kwenye michirizi iliyojengwa ili iweze kupitisha maji machafu vizuri.

Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar amempongeza mshirika mkubwa wa Maendeleo wa Zanzibar, Benki ya Dunia {World Bank } kwa misaada yake kadhaa inayotoa kwa Zanzibar na Tanzania kwa ujumla katika Sekta za Elimu, Miundombinu pamoja na huduma za Kijamii akiitolea mfano Sekta ya Afya.

Balozi Seif aliwahakikishia Wananchi kwamba kupitia mradi huo wa Jamii Mijini Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar inakusudia kuendelea na awamu ya pili ya uwekaji wa Taa za Bara barani kutoka Mwanakwerekwe hadi Kiemba samaki, Uwanja wa Ndege hadi Mnazi Mmoja na Mikunguni hadi Muembenjugu kwa upande wa Unguja.

Alisema kwa upande wa Kisiwa cha Pemba Serikali itaweka Taa za Bara barani katika Miji yote Mitatu ya Pemba , Wete, Chake chake na Mkoani kupitia mradi wa huduma za Jamii Mijini {ZUSP}.

Aidha Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar alisisitiza kwamba kupitia Mradi huo kutoka Mkunazini hadi eneo lote la Majengo ya Nyumba za Maendeleo Michenzani litaboreshwa kwa kazi itakayokwenda sambamba na ujenzi wa Jaa la Kisasa katika mtaa wa Kibele Wilaya ya Magharibi :B” litakalohudumia Mji wa Zanzibar.

Mapema Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango wa Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar Nd. Khamis Mussa Omar alisema chimbuko la mradi wa ujenzi wa ukuta wa Mizingani umetokana na athari kubwa iliyojitokeza siku za nyuma ya kasi kubwa ya maji ya Bahari iliyoathiri eneo hilo.

Alisema Ujenzi wa Ukuta huo ulioanza Tarehe 22 April 2015 ukiwa na urefu wa Mita 320, upana Mita sita na ongezeko na mita sita kuelekea usawa wa Bahari unatarajiwa kukamilika rasmi ndani ya Mwaka huu wa 2017.

Alieleza kwamba asilimia 65% ya ujenzi huo imekamilika kwa upande wa ukuta wenyewe na kazi iliyobaki na kuendelezwa kwa hivi sasa ni ujenzi wa bustani pamoja na bara bara ya watembeao kwa miguu.

Nd. Khamis alisema Mradi wa Jamii Mijini unaotekelezwa na Serikali kupitia Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar chini ya mkopo nafuu kutoka Benki ya Dunia umejigawa sehemu tatu katika utekelezaji wake akizitaja kuwa ni pamoja na kuimarisha Taasisi, Mabaraza ya Miji pamoja na usimamizi wa mradi husika.

Akimkaribisha Balozi Seif kuzindua ujenzi huo wa Ukuta, Waziri wa Fedha na Mipango Dr. Khalid Salum Mohamed alisema uimarishaji wa Mji Mkongwe kupitia mradi wa Jamii Mijini utakuwa chachu ya kuimarika kwa Sekta ya Utalii Nchini.

Dr. Khalid aliwaomba Wamiliki Binafsi wa majengo yaliyomo ndani ya Mji Mkongwe kushirikiana na Serikali Kuu katika kuyaweka kwenye mazingira bora yatakayotoa haiba nzuri ya Mji wa Zanzibar unaotegemewa katika makusanyo ya Mapato ya Taifa kupitia sekta hiyo ya Utalii.

Ujenzi wa Ukuta wa Ukingo wa Bahari hapo Mizingani Forodhani Mjini Zanzibar unasimamiwa na Wizara ya Fedha na Mipango ya Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kupitia Mkono wenye masharti nafuu wa shilingi Bilioni 7,222,577,890 kutoka Benki ya Dunia.

Kampuni ya Seyani Brothers ya Mjini Dar es salaam ndio iliyopewa jukumu la kujenga Ukuta huo chini ya Msimamizi Mshauri muelekezi Kampuni ya Aurecon kutoka Nchini Afrika Kusini.

Othman Khamis Ame
Ofisi na Makamu wa 9ili wa Rais wa Zanzibar

7/1/2017. 



No comments: