ANGALIA LIVE NEWS

Wednesday, March 29, 2017

RC Simiyu amaliza mgogoro wa wanakijiji na wawekezaji

Mkuu wa Mkoa wa Simiiyu, Anthony Mtaka akifungua kikao cha usuluhishi baina ya mwekezaji wa Mwiba Holdings na wadau wa maendeleo mkoani Simiyu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
Na Mwandishi Wetu, Meatu
MKUU wa Mkoa wa Simiyu, Anthony Mtaka amefanikiwa kumaliza mgogoro wa muda mrefu kati ya mwekezaji katika Jumuiya ya Hifadhi ya Wanyamapori (WMA) Makao iliyopo wilayani Meatu, na baadhi ya vijiji vinavyounda jumuiya hiyo. Mwekezaji huyo Mwiba Holdings, amekuwa na mgogoro wa mipaka, mkataba wa kumiliki ardhi na uanzishaji wa ranchi na baadhi ya vijiji hivyo kiasi cha kusababisha kuwa na mahusiano mabaya na wananchi ambao wamekuwa wakisusia misaada mbalimbali inayotolewa na mwekezaji huyo.
Hata hivyo, chanzo halisi cha mgogoro huo kimegundulika kuwa ni viongozi wa baadhi ya vijiji ambao wamekuwa wakipigania maslahi yao binafsi huku wakisambaza taarifa za upotoshaji juu ya mwekezaji huyo na kujenga chuki kwa wananchi. Vijiji vinavyounda WMA ya Makao ni pamoja na Makao, Iramba ndogo, Sapa, Mwangudo, Jinamo, Lukale, Mbushi, Mwabagimu na Sunga.

Baadhi ya viongozi hao wa vijiji pia wamekuwa wakisambaza taarifa potofu kwa wananchi kwamba Mkuu huyo wa mkoa na mkuu wa wilaya ya Meatu wamehongwa na mwekezaji ili kuwakandamiza wananchi, jambo lililothibitika kuwa si la kweli.
Kutokana na mgogoro huo kuzidi kuota mizizi huku uongozi wa CCM Mkoa wa Simiyu nao ukichukua upande, Mtaka alilazimika kuitisha kikao cha usuluhishi kilichoshirikisha wadau wote wakiwamo Kamati ya Siasa ya CCM mkoa na wilaya, viongozi na watendaji wa serikali ngazi ya mkoa na wilaya, viongozi wa vijiji tisa vinavyounda WMA Makao, mwekezaji na wadau wengine akiwamo Mbunge wa Meatu na Mwakilishi wa Ofisi ya Waziri Mkuu.
Akizungumza katika kikao hicho kilichofanyika mwishoni mwa wiki mjini hapa, Mtaka aliwakemea viongozi wanaoeneza taarifa potofu wilayani humo na kusababisha shughuli za maendeleo kukwama huku akiahidi kuwachukulia hatua zinazostahili viongozi wa namna hiyo.
“Katika masuala ya maendeleo ya wananchi sina mzaha. Nipo tayari kuwa kiongozi unpopular (asiyependwa) ili mradi shughuli za maendeleo za wananchi zinaenda mbele.
“Mgogoro na Mwiba umekuwa kama mkuki mnaojichoma wenyewe kila siku kwa sababu wenyewe ndiyo mlioingia mikataba na mwekezaji wakati sisi hatukuwapo na wala hatuna maslahi yoyote binafsi hivyo acheni maneno maneno, kaeni chini mzungumze tusonge mbele,” alisisitiza Mkuu huyo wa mkoa.
“Mmefikisha malalamiko, tena kwa maandishi hadi kwa Waziri Mkuu lakini uhalisia ni kuwa mengi mliyopeleka hayana ukweli, ni hisia na mengine ni fitna tu. Sasa wekeni kila kitu hadharani hapa, tumalize suala hili leo na tujikite zaidi katika mambo ya maendeleo,” alisema.
Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk Titus Kamani akizungumza katika kikao cha usuluhishi baina ya wananchi wa Meatu na Mwekezaji wa Mwiba Holdings kilichofanyika mjini Mwanhuzi mwishoni mwa wiaki.

Mkuu wa Mkoa wa Simiiyu, Anthony Mtaka akifungua kikao cha usuluhishi baina ya mwekezaji wa Mwiba Holdings na wadau wa maendeleo mkoani Simiyu kilichofanyika mwishoni mwa wiki.
Kuhusu mgogoro wa mpaka hasa katika kijiji cha Buhongoja ambako alama ya mpaka yenye namba 314 inadaiwa kusogezwa kinyemela kwa umbali wa kilomita 10, Mkuu huyo wa mkoa alizitaka pande zinazohusika kukutana na kutatua tatizo hilo kwa kurejea katika eneo la awali bila ya mikwaruzano yoyote. Aliamuru pia pande zinazohusika katika suala la mkataba wa umiliki wa ardhi,kukaa meza moja na kuacha mambo ya kukimbilia kwa wasuluhishi ambao wamekuwa wakidai fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kwa maendeleo ya vijiji au wilaya ya Meatu.
Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini aliahidi kupeleka wataalam watatu watakaosaidiana kutatua mgogoro huo wa umiliki wa ardhi watakaosaidiana na wake wa wilaya ili kutatua suala hilo ndani ya wiki mbili.
Awali, Mwenyekiti wa Kijiji cha Makao, Anthony Phillipo alieleza kuwa kijiji kilazimika kupelaka suala hilo kwenye Tume ya Usuluhishi wa Migogoro Dar es Salaam ambako kijiji walishindwa kulipa gharama za usuluhishi huo walizotozwa na Jaji Mstaafu Thomas Mihayo. Mwenyekiti wa CCM mkoa wa Simiyu, Dk. Titus Kamani alieleza chama hicho tawala kusikitishwa na mgogoro huo unaokwamisha shughuli za maendeleo ya wananchi na utekelezaji wa ilani ya uchaguzi ya chama hicho.
“Ndugu zangu, sisi tunajiandaa kushinda katika uchaguzi wa serikali za mitaa mwaka 2019 na uchaguzi mkuu wa mwaka 2020, kwa hiyo tunawaomba tusikubali kuingizwa katika migogoro kama hii ambayo haina tija kwa wananchi.
“Tunataka wakati wa uchaguzi utakapofika tushinde pila pressure (msukumo) yoyote na tunachotaka ni mshikamano,maelewano mazuri baina ya wadau wote ili tufanye shughuli za maendeleo kwa faida ya mkoa wetu wa Simiyu na wilaya ya Meatu,” alisisitiza.
Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Mazingira) Mpina Luhaga ambaye pia ni mbunge wa Kisesa wilayani Meatu alisema katikA kikao hicho kuwa mwekezaji huyo amekuwa akifuata sheria zote za nchi katika utekelezaji wa majukumu yake na ni wazi kwamba wananchi watashindwa katika madai yote wanayofungua katika Tume ya Usuluhishi wa migogoro.
“Mimi nimefuatilia malalamiko haya ya wananchi serikalini na hasa Wizara ya Maliasili na Utalii na hawa jamaa wamefuata taratibu zote na wanalipa tozo zote wanazostahili kulipa hivyo tunapaswa kuwa waangalifu,” alisema.
Mkurugenzi wa Mwiba Holdings, Abdulkadir Mohamed Luta alisema kuwa Kampuni hiyo ipo tayari kukaa meza moja na kusaidia usuluhishi wa mgogoro wowote ili wajikite zaidi katika shughuli za maendeleo ya wananchi. Aliongeza kwamba kampuni hiyo ilikuwa tayari kugharamia hata suala la mkataba wa umiliki wa ardhi lililofikishwa Tume ya Usuluhishi wa Migogoro ili mradi tu suala hilo liishe na waendelee na mambo ya maendeleo
Alisema watazifanyia kazi hoja zote zilizotolewa na wananchi katika kikao hicho na kwamba sera ya kampuni hiyo ni kushirikiana na wananchi na wamekuwa wakitekeleza sera hiyo kwa vitendo.
Mbunge wa Meatu, Salum Khamis maarufu kwa jina la Mbuzi, alisema kuwa hana mgogoro na mwekezaji yoyote lakini hatakaa kimya kutetea maslahi ya wananchi wake ambao ndio waajiri wake kila atakapoona kuna sababu ya kufanya hivyo.
Naye Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Meatu, Pius Machungwa aliahidi kuipatia kiwanja cha kujenga ofisi Kampuni ya Mwiba Holdings katika makao Makuu ya wilaya hiyo ili iwe karibu na wananchi, na kwamba watashirikiana na kampuni hiyo katika shughuli za maendeleo wilayani humo.

No comments: