Mhandisi Mshauri wa Kitengo maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa kutoka Wakala wa Barabara Nchini (TECU), Eng. Mushubira Kamuhabwa (kulia), akitoa taarifa kwa Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (kushoto), kuhusu mradi wa ujenzi wa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akiruka mtaro wa maji uliopo pembezoni mwa barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera.
Muonekano wa sehemu ya barabara ya Kyaka-Bugene KM 59.1 inayojengwa kwa kiwango cha lami, wilayani Karagwe, mkoa wa Kagera. Barabara hiyo inajengwa na mkadarasi kutoka Kampuni ya CHICO na imegharimu kiasi cha Shilingi Bilioni 64.96.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa akitoa maelekezo kwa Mhandisi Jumanne Werema (wa kwanza kulia), kuhusu kukamilisha ujenzi kwa wakati wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Mhandisi Jumanne Werema kutoka Kampuni ya ujenzi wa CMG akimpa taarifa ya mradi Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa kuhusu hatua iliyofikiwa ya ujenzi wa Shule ya Msingi Tumaini iliyopo eneo la Mafumbo, wakati alipokagua, wilayani Bukoba, mkoa wa Kagera.
Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa (katikati), akiongozana na Mhandisi Salum Chanzi (kushoto), kutoka Wakala wa Majengo nchini (TBA), pamoja na Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro (kulia), kukagua maendeleo ya ujenzi wa Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita
Moja
ya Jengo la Shule ya Sekondari ya Wavulana ya Ihungo linalojengwa na
Wakala wa Majengo Nchini (TBA), baada ya Shule hiyo kuathiriwa na tetemeko la
ardhi takriban miezi sita iliyopita, mkoani Kagera.
Serikali
imesema haitavumilia wala kusita kumchukulia hatua yeyote anayevamia na kujenga
katika hifadhi za miundombinu ya barabara na reli kwani kufanya hivyo ni kosa
kisheria.
Akizungumza
na waandishi wa habari wilayani Karagwe, mkoani Kagera mara baada ya kukagua
barabara ya Kyaka hadi Bugene yenye urefu wa kilometa 59.1, Waziri wa Ujenzi,
Uchukuzi na Mawasiliano Profesa Makame Mbarawa amewataka wananchi kuacha
dhana ya kuingilia miundombinu hiyo kwa imani ya kulipwa fidia na Serikali.
"Najua
bado kuna watu wanaendelea kuvamia miundombinu ya usafirishaji, sasa nasema
kuwa Serikali itaendelea kubomoa pasipo kulipa fidia kwa yeyote anayevunja
sheria", amesema Profesa Mbarawa.
Kuhusu
mradi wa ujenzi wa barabara hiyo, Waziri Profesa Mbarawa amekipongeza Kitengo
maalum cha Wahandisi Washauri Wazawa (TECU), kinachosimamiwa na Wakala wa
Barabara nchini (TANROADS), kwa kusimamia ujenzi wa barabara hiyo kwa
kuzingatia viwango na kuwataka kuendelea kuimarisha kitengo hicho ili
kiweze kufikia hatua ya kujenga barabara nchini.
Aidha,
amewataka viongozi wa wilaya hiyo kuwahamasisha wananchi wake kuilinda na
kuitunza barabara hiyo ili iweze kudumu kwa muda mrefu kama
ilivyokusudiwa.
Kwa
upande wake, Mhandisi Mshauri wa mradi huo Eng. Mushubira Kamuhabwa, amesema
kuwa kazi inaendelea vizuri kwani mpaka sasa mradi huo umefika asilimia 98
ambapo kazi iliyobaki ni uwekaji wa alama za barabarani.
Eng.
Kamuhabwa ameongeza kuwa kukamilika kwa barabara hiyo kutarahisisha
usafirishaji wa mizigo na abiria kutokana na barabara hiyo kuwa kiungo kati ya
Tanzania na nchi jirani za Uganda, Rwanda na Burundi.
Mradi
wa ujenzi wa barabara ya Kyaka hadi Bugene umejengwa na kampuni ya CHICO kutoka
nchini China na kugharimu kiasi cha shilingi bilioni 64.96.
Katika
hatua nyengine Waziri Mbarawa ametembelea na kujionea maendeleo ya ujenzi
wa shule ya Sekondari ya wavulana ya Ihungo mkoani Kagera iliyoharibiwa
na tetemeko la ardhi takriban miezi sita iliyopita.
Akiwa
katika shule hiyo Profesa Mbarawa ameridhishwa na kasi ya mkandarasi anayejenga
shule hiyo na kusema nia ya Serikali ni kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali
ya juu ili kukabiliana na majanga mbalimbali.
Naye,
Mkuu wa Wilaya ya Bukoba, Bw. Deodatus Kinawiro pamoja na mambo mengine ameishukuru
Serikali kwa kuwajali wananchi wake na kuijenga shule hiyo kwa ubora wa hali ya
juu.
Ni
takribani miezi sita tangu kutokea kwa tetemeko la ardhi mkoani Kagera na
kuharibu miundombinu mbalimbali ikiwemo ya barabara, madaraja, hospitali, shule
pamoja na makazi ya watu.
Kutokana
na uharibifu huo Serikali pamoja na wadau mbalimbali ilianza juhudi za
ukarabati na ujenzi wa miundombinu hiyo.
Imetolewa
na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini, Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na
Mawasiliano
No comments:
Post a Comment