ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 9, 2017

Sheria ya marehemu kurithisha moyo, figo yaja

By Aurea Simtowe, Mwananchi asimtowe@mwananchi.co.tz

Dar es Salaam. Taasisi ya Moyo ya Jakaya Kikwete (JKCI) inaandaa mapendekezo ili kuyapeleka bungeni yaridhiwe na kupitishwa sheria itakayoruhusu mtu kuandika wosia wa viungo vyake kutumika baada ya kufariki dunia.

Sanjari na hilo, kwa sasa inatararajia kuanza upasuaji wa kupandikiza moyo kwa wagonjwa wenye matatizo hayo nchini. Mkurugenzi wa Upasuaji na Daktari Bingwa wa Moyo na Mishipa ya Damu, Dk Bashir Nyangasa ameyasema hayo jijini Dar es Salaam jana alipokuwa akizungumza na vyombo vya habari kuhusu malengo ya taasisi hiyo.

“Tuko katika maandalizi ya kuandaa mapendekezo kwa ajili ya kupeleka Bungeni ili Bunge liridhie na kupitisha sheria itakayoruhusu mtu kuandika wosia wa viungo vyake kutumika mara baada ya kufariki ikiwamo moyo na figo,” alisema Dk Nyangasa.

Alisema kuwa umefika wakati kwa Watanzania kujiwekea utaratibu wa kuacha wosia wa kutumika kwa viungo vyao baada ya kufariki kwa ajili ya kuhifadhiwa kwenye benki za viungo ili viweze kutumiwa na watu ambao watavihitaji.

Dk Nyangasa alisema Hospitali ya Apolo Bangalole ya India na nyingine za kimataifa za magonjwa ya moyo kwa sasa zimehamia JKCI kutokana na kuwapo kwa huduma pamoja na vifaa vya kisasa.

Naibu Mkurugenzi wa Huduma za Tiba na Daktari Bingwa wa Magonjwa wa Moyo, Dk Tulizo Shemu alisema mwaka 2016 JKCI ilifanya uchunguzi wa tiba kwa wagonjwa 973 na kati yao 620 walipata matibabu bila kufunua vifua kwa kupitia mishipa ya damu, huku 353 wakifanyiwa upasuaji wa kufungua vifua.

Taasisi hiyo inategemea kuwa na kambi maalumu ya matibabu ya moyo kwa kushirikiana na Open Heart International ya Australia kuanzia kesho.

No comments: