ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, March 23, 2017

TUTASAIDIA JUHUDI ZA TTB - MABALOZI

Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB Bi devota Mdachi akizungumza na Mabalozi waliomtembelea ofisini kwake jana.Kushoto ni Balozi Omari Yusuph Mzee na kulia ni Balozi Abdallah Kilima.
Balozi mteule wa Tanzania nchini Kenya Dkt Pindi Chana akisisitiza jambao wakati wa mazungumzo baina yao na Mkurugenzi Mwendshaji wa TTB walipomtembelea ofisini kwake Dar es salaam.
Mkurugenzi Mwendshaji wa Bodi ya Utalii Tanzania Bi Devota Mdachi (kulia) akimkabidhi Balozi Abdallah Kilima moja ya majarida ya TTB yanayozungumzia utalii wa Tanzania wakati timu ya mabalozi sita walioteuliwa hivi karibuni walipomtembela Mkurugenzi huyo ofisini kwake jijini Dar es salaam.
Mabalozi wanaowakilisha Tanzania katika baadhi ya nchi duniani wakiwai katika picha ya pamoja na Mkurugenzi wa TTB Bi Devota Mdachi (wa nne kushoto) na baadhi ya Maafisa waandamizi wa TTB . Kutoka kushoto ni Bw. Geofrey Meena Meneja Masoko wa TTB, Mh. Balozi dkt Pindi Chana , Mh. Balozi Omari Yusuph Mzee, Mh. Balozi Fatma Rajab (wa tano), Mh. Balozi Grace Mgovano (wa sita), Mh. Balozi Matilda Masuka (wa saba) na Bw. Philip Chitaunga Meneja Huduma kwa watalii wa TTB.


Na: Geofrey Tengeneza


Mabalozi walioteuliwa hivi karibuni na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt John Pombe Magufuli kuiwakilisha Tanzania katika nchi mbalimbali duniani wameihakikishia Bodi ya Utalii Tanzania (TTB) kuwa wamejizatiti kikamilifu kwenda kusaidia juhudi kubwa za Bodi hiyo katika kuitangaza Tanzania kama eneo bora la Utalii duniani katika nchi wanazokwenda kufanyakazi sambamba na kuhamasisha wafanyabiashara kutoka mataifa hayo kuwekeza nchini katika sekta ya utalii ikiwa ni utekelezaji wa jukumu lao kubwa la kukuza diplomasia ya uchumi.

Wamepongeza juhudi zinazofanywa na TTB katika kuvitangaza vivutio vyetu vya utalii lakini wakaomba iangalie namna gani inaweza kusaidia katika kuboresha huduma zitolewazo na wadau wa utalii kwa watalii wanaotembelea Tanzania kama vile mahotelini kwani bado hatufanyi vema katika suala la huduma bora na nzuri kwa watalii. Aidha wameiomba TTB kushauri mamlaka na watoa huduma wengine katika sekta ya utalii kupunguza gharama wanazotoza kwani ni kubwa sana kiasi cha kuifanya Tanzania kulalamikiwa na wageni wengi kuwa ni eneo la utalii ghali sana ukilinganisha na nchi nyingine ambazo ni washindani wetu katika sekta ya Utalii.

Hayo yamesemwa leo na mabalozi hao wakiongozwa na Balozi Omari Yusuph Mzee walipotembelea makao makuu ya Bodi ya Utalii Tanzania kwa lengo la kuzungumza na Mkurugenzi Mwendeshaji wa Bodi hiyo Bi Devota Mdachi na kupanga mikakati ya namna balozi hizo zinavyoweza kushirikiana na TTB katika kuitangaza Tanzania na kuhamashisha wawekezaji kutoka nchi wanazokwenda kufanyakazi kuja nchini kuwekeza katika sekta ya utalii.

Mapema Mkurugenzi Mwendeshaji wa TTB Bi Devota Mdachi aliwaelezea waheshimiwa mabalozi mikakati mbalimbali ambayo Bodi yake imekuwa ikitekeleza katika kuitangaza Tanzania nje ya nchi kwa lengo kuvutia watalii wengi zaidi na kukuza utalii kwa ujumla. Alitaja baadhi ya mikakati hiyo kuwa ni pamoja na kuweka matangazo katika maeneo na vyombo mbalimbali vya habari nje ya nchi, kualika na kuleta nchini watu maarufu ili kuja kutembelea vivutio vyetu vya utalii, kuteua mabalozi wa hiari wa utalii na kutumia mitandao mbalimbali ya kijamii.Mkurugenzi Mwendeshaji Bibi Devota Mdachi aliwakabishi mabalozi hao vielelezo mbalimbali vya utalii wa Tanzania na kuahidi kuwa bodi yake itakuwa ikiwatumia vielelezo mbalimbali vya utalii vitakavyo wasaidia katika kutekeleza jukumu la kusaidia utangazaji utalii katika nchi walizopangiwa. Mabalozi hao watano na nchi wanazo kwenda ni Omari Yusuph Mzee (Algeria), Matilda Masuka (Korea Kusini), Dkt. Pindi Chana (Kenya), Grace Mgovano (Uganda), Fatma Rajab (Qatar) na Balozi Abdallah Kilima (Oman).

No comments: