Saa tatu baada ya viongozi wa CUF kukutana na Kamanda wa Polisi wa Kanda Maalumu ya Dar es Salaam, Simon Sirro, kuhoji sababu za kutokamatwa watu waliofanya vurugu kwenye mkutano wa waandishi wa habari na viongozi wa chama hicho wa wilaya ya Kinondoni, Jeshi la Polisi limetangaza kushikilia watu watatu.
Wakiongozwa na Mwenyekiti wa Kamati ya Uongozi ya Chama hicho Julius Mtatiro, viongozi hao waliwaeleza wanahabari kuwa ni ajabu kuona Polisi haijachukua hatua huku ikijulikana wazi kuwa watu hao walijeruhi wanahabari na viongozi wa chama hicho katika tukio ambalo liliripotiwa na vyombo vya habari.
Viongozi hao walikutana na Sirro jana saa 5 asubuhi na kuzungumza kwa takribani saa moja, na kisha saa 8 mchana Kamanda huyo alizungumza na waandishi wa habari na kueleza kukamatwa kwa watu hao, wakituhumiwa kuhusika katika tukio hilo.
Jumamosi iliyopita takribani watu watano wakiwa kwenye gari lenye nembo na bendera za CUF, walivamia mkutano huo uliokuwa ukifanyika kwenye hoteli ya Vinna, Mabibo wilayani Kinondoni na kufanya vurugu.
Miongoni mwa watu hao, mmoja aliyekuwa amejifunika uso kininja alichomoa bastola na kutishia huku mwingine akishindwa kuondoka baada ya kuachwa na wenzake, jambo lililosababisha wananchi wamzingire na kumshushia kipigo.
Katika ufafanuzi wake, Mtatiro alisema tukio hilo ni la 13 dhidi ya upande unaomwunga mkono Katibu Mkuu wa Chama hicho, Maalim Seif Sharif Hamad lakini vyombo vya Dola viko kimya.
“Baada ya tukio la juzi (Jumamosi) tulikaa kimya ili kuona kama polisi watasema chochote ila imekuwa tofauti. Wako kimya tu,” alisema Mtatiro.
Akieleza kilichowapeleka kituoni hapo, alisema: “Tulitaka kujua yule mvamizi aliyekuwa na bastola mpaka sasa yuko wapi. Mvamizi mmoja tunajua alikamatwa na wananchi, akapigwa kidogo na kuokolewa. Tulitaka kujua alitoa maelezo gani.”
Alisema baada ya tukio hilo, Mkuu wa Upelelezi aliwapigia simu viongozi waliovamiwa akiomba waende kituo cha Polisi Magomeni wakapatanishwe.
“Tulishangazwa na taarifa hiyo, kwa watu waliovamiwa kwenda kupatanishwa. Tulijihoji kama Jeshi la Polisi linaweza kupatanisha watu wenye makosa ya jinai, kwani mtu wa makosa hayo upelelezi unapokamilika hupelekwa mahakamani,” alisema Mtatiro.
Alisema sababu nyingine ya kwenda kituoni hapo ni kutaka kufahamu kama watu wanaofanya matukio hayo wako juu ya sheria.
“Tulimwonya Kamanda Sirro kwamba sisi (upande wa Maalim) tuna nguvu kuliko Lipumba na kuiomba Polisi kutekeleza majukumu yake kwa kuchukua hatua dhidi ya wavamizi hao,” alisema.
Katika mkutano wake na wanahabari, Sirro alisema Polisi inashikilia watu watatu wakituhumiwa kufanya vurugu kwenye mkutano huo.
“Tulipata taarifa ya kuvamiwa kwa mkutano wa wanachama wa CUF na watu wasiofahamika wakiwa na silaha. Baada ya taarifa hizo kupokewa askari walifuatilia na kukamata watu watatu,” alisema Sirro.
Alisema watuhumiwa hao wanaendelea kuhojiwa na upelelezi ukikamilika hatua za kisheria zitafuatwa.
Alisema hakuna mtu aliye juu ya sheria na kusisitiza kuwa waliohusika watasakwa kokote watakokuwa.
No comments:
Post a Comment