Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi, Jenerali Venance Mabeyo aliwaambia waandishi wa habari kwamba wanajeshi wamejiandaa kuonesha umahiri wao katika sherehe hiyo na katika kulinda usalama wa nchi. Wakati maandalizi yakiendelea, ndege za jeshi zilikuwa zikifanya maonesho angani juzi na jana; na zitaonesha umahiri leo, hali iliyoongeza morali ya wananchi katika maadhimisho haya.
Katika kuadhimisha siku hii, Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan amewahimiza Watanzania kuudumisha na kuuenzi Muungano kwa amani, upendo, mshikamano na kufanya kazi kwa juhudi na maarifa. Aliwahakikishia wananchi wa pande zote mbili kuwa, serikali inafanya kila liwezekanalo kumaliza kero zilizosalia za Muungano haraka kupitia mazungumzo ya pamoja kama hatua ya kuudumisha. Rais Magufuli aliwasili mjini Dodoma tangu Jumatatu, siku moja kabla ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dk Ali Mohamed Shein kuwasili.
Pamoja na viongozi hao, pia yupo Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa ambaye amekuwa akikagua maandalizi ya sherehe hizi. Wabunge mbalimbali wamekuwa wakishiriki kikamilifu katika maandalizi hayo kutokana na Bunge kusitisha shughuli zake kujadili Bajeti za Serikali ili kushiriki na kushuhudia tukio hili la kihistoria. Kwa mujibu wa Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Jordan Rugimbana, maandalizi yote yamekamilika kwa asilimia 100 na wananchi kutoka kila kona za mkoa na mikoa jirani, wanakaribishwa kushuhudia matukio mengi hasa gwaride, maonesho ya makomandoo, mbwa na farasi na burudani.
Rugimbana aliwaambia waandishi jana kwamba tukio hilo la kihistoria, linahusisha mabalozi, viongozi wastaafu, waliochanganya udongo wakati wa kuunganisha pande mbili za Muungano na waasisi wengine, linafungua milango kwa wawekezaji, hasa wafanyabiashara na watu mbalimbali kuwekeza katika mkoa huu. “Mkoa wa Dodoma upo tayari kwa ajili ya kupokea wageni. Mkoa huu umepata heshima ya kuandaa sherehe hizi, baada ya kuwa zikifanyika mkoani Dar es Salaam kwa muda mrefu.
Hii ni sifa kubwa kwa mkoa,” alisema Rugimbana ambaye pia ni Mwenyekiti wa Kamati ya Ulinzi na Usalama wa Mkoa. Fundi madirisha wa eneo la jirani na Uwanja wa Jamhuri, Batista Kipene alisema anafurahia kitendo cha sherehe hizo kufanyika Dodoma, hasa kutokana na kuwapo kwa askari wengi wanaofanya mafunzo kwa ukakamavu. Waziri wa Kilimo, Maliasili, Mifugo na Uvuvi, Hamad Rashid Mohamed ambaye ni Mwenyekiti wa chama cha ADC, alisema Wazanzibari wanayo fursa kubwa ya kuitumia katika Muungano kwa ajili ya kujiimarisha kiuchumi na maendeleo.
Hamad Rashid aliyewahi kuwa Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati wa uongozi wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere, alisema ardhi ni moja ya eneo ambalo Wazanzibari wananufaika kwa kuwekeza katika miradi mbali mbali Tanzania Bara. Mwenyekiti wa Chama cha Wakulima (AFP), Said Soud aliwataka wananchi kuwapuuza watu wanaokejeli Muungano ambao wao ndiyo waliofaidika na fursa hizo kwa muda mrefu wakati wakiwa viongozi. Alisema Muungano umepita katika majaribio mbalimbali na wapo viongozi wanaoukejeli kwamba hauna tija kwa wananchi wa Zanzibar.
Katibu wa Kamati Maalumu ya Halmashauri Kuu ya CCM Zanzibar, Idara ya itikadi na Uenezi, Waride Bakari Jabu alisema Chama Cha Mapinduzi kitahakikisha kinalinda Muungano kwa nguvu zake zote, kwani ni hazina inayotokana na viongozi wetu, ambapo ni sehemu ya sera zake. Kwa upande wake, Makamu wa Rais, Samia amewahimiza wananchi kudumisha na kuuenzi Muungano wa Tanganyika na Zanzibar na kuwahakikishia wananchi wa pande mbili kuwa kero chache za Muungano ambazo zimebaki zitamalizwa kwa mazungumzo kama hatua ya kudumisha Muungano huo.
Katika mahojiano na vyombo mbalimbali vya habari katika kuelekea katika kilele cha maadhimisho ya miaka 53 leo, Makamnu wa Rais alisisitiza kuwa tangu Muungano huo uasisiwe, umekuwa na manufaa makubwa kwa pande zote mbili kwani jamii zimefahamiana na kushirikiana katika shughuli za kiuchumi na za kimaendeleo hasa uimarishaji wa ulinzi na usalama kwa wananchi wa pande mbili. Alisema hatua zinazochukuliwa za kutatua kero za Muungano kwa haraka ni jambo jema na la msingi kwani linalenga kuhakikisha unakuwa ni wa mfano wa kuigwa duniani.
Kamanda wa Polisi mkoani Dodoma, Lazaro Mambosasa alisema wamejipanga kuhakikisha kuna hali ya utulivu wakati wa maadhimisho hayo, na katika kuhakikisha maadhimisho hayo yanafanyika kwa amani na utulivu, Polisi itahakikisha wageni wote wanasherehekea kwa amani na utulivu na wataimarisha ulinzi, doria na misako. Imeandikwa na Magnus Mahenge, Sifa Lubasi (Dodoma) na Khatib Suleiman, Zanzibar.
HABARI LEO
No comments:
Post a Comment