ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 2, 2017

Wabunge walia na Sheria ya kunyonga

KAMATI ya Kudumu ya Bunge ya Katiba na Sheria imependekeza kwa Serikali kupitia upya sheria inayotoa adhabu ya kunyongwa kwa kutenga muda maalumu wa kutekelezwa na ukipita, adhabu hiyo igeuke moja kwa moja kuwa kifungo cha maisha jela.

Katika hatua nyingine, Kamati hiyo imewataja marais wastaafu Ali Hassan Mwinyi, Benjamin Mkapa na Jakaya Kikwete kutotekeleza adhabu hiyo walipokuwa madarakani.

Mapendekezo hayo ya kamati yaliyotolewa jana na Mwenyekiti wa kamati hiyo, Rashid Shangazi, yalieleza kuwa, kamati hiyo imewahi kupendekeza adhabu ya kunyongwa iangaliwe upya kwa kuwepo na muda wa utekelezaji, na kama haitatekelezwa kwa kipindi hicho, aliyehukumiwa atumikie kifungo cha maisha jela.

"Watanzania wengi wanasubiri kunyongwa magerezani, kuanzia Nyerere, hakuna tena uongozi uliotekeleza adhabu hii, Mwinyi, Mkapa, Kikwete wote hawa hawakuitekeleza, na sasa utawala huu bado haijatekelezwa, kwanini hii sheria iendelee kuwepo?" alihoji Shangazi.

Alisema aliyehukumiwa adhabuhiyo anapokaa muda mrefu gerezani, ni adhabu kubwa zaidi na anaathirika zaidi na ni kinyume cha haki za binadamu ambazo Tanzania imesaini mikataba ya Kimataifa kuzitekeleza na kuzilinda na nyingine zipo katika Katiba ya nchi.

"Kamati inashauri Serikali iangalie hii adhabu, inaweza kupendekeza katika sheria kutengwa kwa muda fulani kwa aliyehukumiwa na unapofika, automatic (moja kwa moja) inageuka kuwa kifungo cha maisha jela," ilishauri kamati.

Kamati ilishauri hayo kama mapendekezo yake ya awali kwa Wizara ya Katiba na Sheria baada ya kupitia bajeti ya wizara hiyo kifungu kwa kifungu na kuipitisha kwa maagizo ya kufanya baadhi ya marekebisho.

Mapendekezo kamili watayatoa wakati wa kuwasilisha bajeti katika Bunge linaloanza Aprili 4, mwaka huu. Juzi katika majadiliano ya wajumbe wa kamati hiyo wakati wakipitia utekelezaji wa bajeti na mpango kwa mwaka 2016/17 na mapendekezo ya bajeti ya wizara hiyo kwa mwaka 2017/2018, walishauri kuwa, suala la adhabu ya kifo na mahabusu kusongamana magerezaji yatazamwe upya.

Kwa upande wake, Waziri wa Katiba na Sheria, Profesa Palamagamba Kabudi, aliishukuru kamati hiyo kwa mapendekezo na ushauri kwa serikali na kueleza kuwa, watayafanyia kazi mapendekezo yaliyotolewa kwa maslahi ya umma.

"Naomba niwahakikishie kuwa, mapendekezo yote mliotoa tumeyachukua, tutayazingatia na kuyafanyia kazi," alisema Profesa Kabudi.

Takwimu zinaonesha kuwa, Watanzania 465 wanasubiri kunyongwa katika Magereza mbalimbali nchini na tangu mwaka 1994 hukumu hiyo haijatekelezwa nchini.

Taarifa mbalimbali za Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (THBUB) nchini, zinabainisha kuwa, hakuna hukumu yoyote ya kifo iliyosainiwa na Rais tangu utawala wa Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere ili kutekelezwa hadi sasa.

Ripoti ya Mpango wa Kujitathmini Kuhusu Hali ya Utekelezaji wa Haki za Binadamu (UPR), unaotekelezwa kwa mara ya pili nchini Tanzania, inaonesha kuwa hadi mwaka jana, kulikuwa na mahabusu 465 wanaosubiri adhabu ya kifo.

Kati yao wanaume ni 445 na wanawake ni 20. Wadau mbalimbali wa haki za binadamu wamekuwa wakiitaka Serikali kuifuta adhabu hiyo kwa kuwa haitekelezeki na ni kinyume cha haki ya binadamu ya kuishi ambayo pia imetamkwa katika Katiba ya Tanzania ya mwaka 1977, Sehemu ya Tatu, Ibara ya 14 inayosema; "Kila mtu anayo haki ya kuishi na kupata kutoka kwa jamii hifadhi ya maisha yake, kwa mujibu wa sheria."

Hata hivyo, baadhi ya asasi hasa zinazohusika na haki za walemavu wa ngozi (albino), zinapinga kufutwa kwa adhabu hiyo kwa madai kuwa, hata wao wana haki ya kuishi hivyo anayewaua hana haki ya kuishi kama alivyoondoa haki hiyo kwa albino.

Kamati hiyo ilipitia vifungu kwa vifungu bajeti ya wizara hiyo ya Sh bilioni 159.3 kwa mwaka wa fedha 2017/18 kutoka Sh bilioni 191.4 mwaka 2016/17 ikiwa ni pungufu ya asilimia 4 kutokana na fedha za washirika wa maendeleo wa nje kutojumlishwa.

HABARI LEO

No comments: