ANGALIA LIVE NEWS

Sunday, April 2, 2017

WATANZANIA WAASWA KUPAMBANA NA VITENDO VYA RUSWA

Na Mussa Mbeho,Katavi

WATANZANIA wametakiwa kuungana kwa pamoja katika kuijenga Tanzania ya uchumi wa viwanda ikiwa ni pamoja kupambana na kuzuia vitendo vya rushwa vinavyokwamisha miradi mbalimbali ya maendeleo hapa nchini.

Wito huo umetolewa leo na Makamu wa pili Rais wa serikali ya Mapinduzi Zanzibar Mh.Balozi Seif Ally Idd katika uzinduzi wa mbio za mwenge wa uhuru mkoani Katavi.

Amesema Tanazania inapanga kutenga maeneo maalumu ya uwekezaji pamoja na kujenga kituo cha uratibu wa shughuli za viwanda katika maeneo mbalimbali hapa nchini ili kuwezesha Tanzania kuwa kitovu cha uzalishaji malighafi na bidhaa mbalimbali zitakazouzwa ndani na nje ya nchi.

Katika hatua nyingine Mh.Balozi Seif Idd amesema kwa kipindi cha mwezi Januri hadi Septemba 2016 idadi ya watuhumiwa wa madwa ya kulevya waliokamatwa ni 16,026 ambapo kiasi kg 13.129 za Heroin,Kg 17.33 za Cocain,Kg 56,739.48 za bangi na Kg 14,863.63 za mirungi zilikamatwa huku kwa kipindi cha mwaka huo jumla ya hekari 54 za mashamba ya bangi zikiteketezwa katika mikoa yenye kilimo haramu cha bangi.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa Katavi Meja Jenerali Mstaafu Raphael Muhuga amesema zaidi ya miradi 60 yenye thamani ya shilingi Bilioni 7.2 inatarajiwa kuzinduliwa katika Halmshauri tano za Mkoa wa Katavi.

Ametaja baadhi ya miradi kuwa ni pamoja na Ujenzi wa Uwanja Mpya wa Mpira wa Miguu unaojengwa katika kata ya Ilembo,Ofisi Mbalimbali za Serikali,klabu za kupambana na maambukizi ya Ukimwi pamoja na uanzishwaji shughuli za ujenzi wa viwanda vitatu kikiwemo cha kusindika maziwa.

Naye kiongozi wa mbio za mwenge wa Uhuru kitaifa kwa mwaka 2017 Bw.Amour Hamad Amour mara baada ya kukabidhiwa mwenge wa Uhuru na Makamu wa Rais amesema, Mwenge wa uhuru unatarajiwa kukimbizwa kwa siku 195 katika Halmshauri 195 ndani ya mikoa 31 ya Tanzania.

Sherehe za uzinduzi wa mwenge wa Uhuru pia zimehudhuriwa na viongozi mbalimbali wa kitaifa akiwemo Waziri Mkuu mstaafu wa awamu ya nne wa Tanzania Mh.Mizengo Pinda,Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu sera,Bunge ,Kazi, vijana , ajira na wenye Ulemavu Tanzania bara Mh.Jenesta Mhagamapia Waziri wa kazi, Uwekezaji,vijana, wazee, Wanawake na watoto kutoka Zanzibar huku Kauli mbiyu ya mwenge wa Uhuru kwa mwaka 2017 ni ‘’Shiriki Kukuza Uchumi wa Viwanda kwa Maendeleo ya nchi yetu’’

No comments: