ANGALIA LIVE NEWS

Monday, July 31, 2017

TUME YA TAIFA YA UCHAGUZI YAITAHADHARISHA CUF

Na Margareth Chambiri, NEC

Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) imekishauri Chama cha Wananchi (CUF) kumaliza mgogoro unaoendelea ndani ya Chama hicho kwani unaweza kusababisha kupoteza nafasi za Udiwani katika Uchaguzi Mdogo unaotarajiwa kufanyika wakato wowote kuanzia sasa.

Tahadhari hiyo imetolewa leo na Mkurugenzi wa Uchaguzi wa Tume hiyo Bw. Kailima Ramadhani katika mahojiano maalum Ofisini kwake kuhusu tuhuma  mbalimbali zilizoelekezwa Tume hiyo ikiwemo suala la Uteuzi wa Wabunge wa Viti Maalum kupitia CUF.
Bw. Kailima amesema mvutano unaoendelea ndani ya Chama cha Wananchi (CUF) hauna tija, hivyo ameshauri pande mbili zinazovutana kukutana na kumaliza tofauti zao kwani hali hiyo itawanyima nafasi ya kutoa wagombea kwenye uchaguzi huo mdogo.
 ‘Mimi niwashauri, CUF wana mgogoro wao wamalize mgogoro wao. Ni vizuri wakutane wamalize mgogoro wao kwani hii inaweza kuwaletea matatizo wagombea wakati wa Uchaguzi.’ alisesema Kailima na kusisitiza kuwa mgogoro ndani ya chama hicho hauna tija na badala yake unakidhoofisha. 
Amesema Sheria ya Taifa ya Uchaguzi, inakitaka Chama cha Siasa kumsimamisha Mgombea mmoja kwa nafasi moja, lakini pia mgombea wa nafasi ya Rais na Mbunge  lazima fomu yake isainiwe na Viongozi wa ngazi ya Taifa wanaotambuliwa na Msajili wa Vyama vya Siasa.
‘Lakini ukisoma Maelekezo ya Vyama vya Siasa na Wagombea yanasema iwapo chama cha Siasa kina mgogoro ni lazima fomu zake zisainiwa na kiongozi wa juu wa ngazi ya Mkoa, sasa kwa hali hii iwapo CUF wasipokutana watapoteza nafasi.’ Amesema Mkurugenzi huyo wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.  
Bwana Kailima amesema Tume ya Taifa ya Uchaguzi inatambua taarifa za Vyama vya Siasa iliyowasilishwa na Msajili wa Vyama vya Siasa na kwa Chama cha CUF viongozi wanaotambuliwa na Tume hadi hivi sasa ni Mwenyekiti Prof. Ibrahim Lipumba na Katibu Mkuu ni Maalim Seif Sharif Hamad. 
‘Tume inatambua kuwa Mwenyekiti wa CU ni Prof. Ibrahim Lipumba, Inatambua Katibu Mkuu wa CUF ni Maalim Seif Sharif Hamad na Naibu Katibu Mkuu upande wa Bara ni Magdalena Sakaya’ amesema.
Amesema Tume haijazuiliwa na Mahakama wala na Msajili wa Vyama vya Siasa kwamba isifanye mawasiliano na Viongozi hawa, na kubainisha kuwa Tume itaendelea kufanya mawasiliano na Viongozi mpaka hapo itakavyoelekezwa vinginevyo na Msajili wa Vyama au Mahakama.
Mkurugenzi huyo wa Uchaguzi amesema Tume inafanya kazi kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na Taratibu na kwamba mawasiliano ya Tume na Chama cha Siasa ni kwa mujibu wa maelekezo ya Msajili wa Vyama vya Siasa ambaye ndiye anayesajili Vyama vya Siasa nchini.  
Aidha katika hatua nyingine Bwana Kailima ameelezwa kusikitishwa na taarifa za upotoshaji zinazoihusisha Tume kwenye kikao cha Wanasheria kwa lengo la kumshauri Spika wa Bunge kuhusu Chama cha Wananchi CUF na kubainisha kuwa taarifa hizo hazina ukweli wowote.
 Akielezea hatua zinazoweza kuchukuliwa na Tume dhidi ya upotoshwaji unaofanywa na baadhi ya Wanasiasa na Vyombo vya Habari kuhusu utendaji kazi wa Tume Kailima amesema Tume itatumia Mamlaka zinazohusika na usajili ingawa hata hivyo amesisitiza kuwa ni vyema Vyama vya Siasa vitumie Wanasheria wao kusoma Sheria na taratibu za Uchaguzi ili kupata habari sahihi.
‘Hatua ya kwanza tunayochukua ni hii ya kuelimisha Chama pengine ni bahati mbaya lakini hatua ya pili ni ya kuzitaarifu mamlaka Kwa upande wa Vyama ni Msajili wa Vyama kwa upande wa Vyombo vya Habari vya Magazeti tunamtaarifu Msajili wa Magazeti ili ashughulike nao’ lakini kubwa tunawashauri jamani someni au ulizeni Tume,’ amesema Kailima.  

No comments: