Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kushoto akiwa na mwenyeji wake kulia ambaye ni Mkurugenzi wa Maswala ya Afrika Nchini Cuba, Balozi Jose Prieta Cintado August 25/2017 wakiangalia Sanamu ya aliyekuwa Rais wa Msumbiji Hayati Samora Masheli ambayo ipo katika Makumbusho ya Mashujaa wa Africa yaliopo Havana Cuba. Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu .
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa kulia pamoja na Mama Mary Majaliwa kushoto pamoja na mwenyeji wao katikati ambaye ni Mkurugenzi wa Maswala ya Africa nchini Cuba, Balozi Jose Prieta Cintado wakiweka Shada la Maua August 25/2017 katika Makumbusho ya Mashujaa wa Africa yaliyopo Havana Cuba .Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu
WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa ameishukuru Serikali ya Cuba kwa kutambua na kuthamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa wa ukombozi wa Bara la Afrika, akiwemo Baba wa Taifa Mwl. Julius Nyerere kwa kuwajengea mnara wa kumbukumbu.
Mnara huo umejengwa katika Manispaa ya Playa jijini Havana kwenye eneo maalumu la makumbusho ya mashujaa hao walioshiriki katika ukombozi wa Afrika, ambapo zimewekwa sanamu zao pamoja na maelezo mafupi ya historia zao na nchi wanazotoka.
Waziri Mkuu alifanya ziara katika eneo hilo jana (Ijumaa, Agosti 25, 2017) na kuweka shada la maua katika mnara huo uliozungukwa na sanamu za mashajuaa wa Bara la Afrika na kuoneshwa sehemu itakayowekwa sanamu ya Mwl. Nyerere.
Akiwa katika eneo hilo, Waziri Mkuu aliishukuru Serikali ya Cuba kwa kujenga makumbusho ya mashujaa hao na kwamba Serikali ya Tanzania itashirikiana na Cuba kuhakikisha kuwa sanamu ya Mwl. Nyerere inawekwa katika sehemu iliyotengwa.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Instuto Cubano De Amistad Con El Pueblo (Taasisi ya Ushirikiano wa Cuba na Nchi Marafiki), Bw. Jose’ Prieto Cintado alisema mnara huo umejengwa kwa lengo la kutambua thamani na umuhimu wa viongozi hao.
Mkurugenzi huyo alisema Serikali ya Cuba inathamini mchango mkubwa uliotolewa na mashujaa hao katika vita ya ukombozi wa Bara la Afrika, ambapo iliamua kujenga mnara wa kumbukumbu katika nchi yao.
Alisema wananchi wa Cuba pamoja na watu kutoka mataifa mbalimbali ndani na nje ya Bara la Afrika wanakwenda katika eneo hilo la makumbusho na kujifunza historia za viongozi hao. Pia eneo hilo linatumiwa na watafiti wa masuala ya kihistoria.
Mashujaa ambao tayari sanamu zao zimekwishawekwa kwenye eneo la kuzunguka mnara huo ni pamoja na Jomo Kenyatta (Rais wa kwanza wa Kenya), Modibo Keita (Rais wa Mali), Amilcar Cabral (Rais wa kwanza wa Guinea Bissau).
Wengine ni Dkt. Kwame Nkrumah (Rais wa kwanza Ghana), Oliver Thambo (Kiongozi Mwandamizi wa Chama cha Ukombozi cha ANC cha Afrika Kusini), Eduardo Chivambo Mondlane (Kiongozi wa ukombozi nchini Msumbuji).
Wengine ni Samora Moises Machel (Rais wa kwanza wa Msumbuji), Sekou Toure (Rais wa kwanza wa Senegal), Seretse Khama (Rais wa kwanza wa Botswana), Alhaji Aboubakar Tafawa Balewa na Obafemi Jeremiah Awolowo (Mawaziri Wakuu wa zamani wa Nigeria) na Chifu Jeremia Azikiwe (Rais wa zamani wa Nigeria) .
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
No comments:
Post a Comment