ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, September 26, 2017

Maalim Seif awanyima usingizi CCM Zanzibar

By Waandishi Wetu, Mwananchi

CCM imewataka wananchi kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo kama kawaida na kuachana na ilichoita upotoshaji unaofanywa na Katibu Mkuu wa Cuf, Maalim Seif Sharif Hamad kuwa ataapishwa kuwa Rais wa Zanzibar karibuni.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Abdallah Juma maarufu Mabodi alitoa kauli hiyo baada ya Maalim Seif kuendelea kutoa kauli hiyo kwa wananchi.

Mabodi alisema hakuna kiongozi wa CCM hata mmoja aliyewahi kufanya mazungumzo na Maalim Seif, kuhusu suala la kukabidhiwa madaraka.

Alisema kilichopo ni kiongozi huyo wa upinzani kutoa taarifa zisizo rasmi kwa jamii, huku baadhi ya wananchi wakipata taharuki.

“Amini kuwa hatujawahi kukaa na mahasimu wetu hao hata siku moja kujadili suala la hali ya siasa Zanzibar, hasa kuhusu hili la mabadiliko ya kiongozi, wao wana kazi zao za kisiasa na sisi tuna kazi zetu ambazo tunaendelea kuzifanya ili kujiweka tayari kwa ushindi uchaguzi wa mwaka 2020,” alisema Mabodi.

Kauli ya Mabodi imekuja kufuatia Maalim Seif kuendelea kutoa kauli za kuwaweka njia panda juu ya uwapo wa mabadiliko ya uongozi Zanzibar.

juzi, Maalim Seif akiwa katika kongamano maalumu lililoandaliwa na Jumuiya ya Vijana wa chama chake (Juvcuf) kupitia wanafunzi wa vyuo vikuu, alisema huu ni wakati wa wananchi kukaa tayari kupokea mabadiliko ya uongozi.

Maalim Seif alisema atakakabidhiwa madaraka ya urais hivi karibuni.

“Nataka mfahamu hakuna hata mtu mmoja mwenye nguvu ya kunizuia kuapishwa kuwa Rais wa Zanzibar, kinachofanyika sasa ni CCM kuhangaika tu ila mambo mazuri yaja,” alisema.

Alisema akiwaambia vijana hao kuwa haki ya Wazanzibari haitapotea. (Imeandikwa na Haji Mtumwa na Muhammed Khamis)

No comments: