Dar es Salaam. Siku chache baada ya diwani mwingine wa Chadema mkoani Arusha kujiunga na CCM, katibu wa itikadi na uenezi wa chama hicho, Humphrey Polepole amesema tukio hilo halikuwa limeandaliwa.
Diwani huyo wa Kimandolu (Chadema), Mchungaji Rayson Ngowi alitangaza kuihama Chadema dakika chache baada ya Rais John Magufuli kutoa fursa kwa wanachama wa vyama tofgauti kutangaza kujiunga na vyama vingine.
Tukio hilo lilifanyika wakati wa hafla ya kutunuku kamisheni kwa maofisa 422 wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) iliyofanyika Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Baada ya tukio hilo la madiwani, wabunge wa Chadema, Godbless Lema(Arusha Mjini) na JoshuaNassari (Arumeru Mashariki) walijitokeza kukemea kitendo cha kutumia shughuli ya kiserikali kujenga chama na kwamba wana taarifa kuwa rushwa ilitumika na wanao ushahidi wa kumuonyesha Rais.
Pamoja na Rais kueleza katika hotuba yake kuwa ameambiwa kuwa kulikuwa na watu wanataka kujiunga na CCM, Polepole ambaye alihudhuria mkutano huo, alisema hakuna utaratibu uliokuwa umeandaliwa kwa ajili ya kupokea wanachama wapya mbele ya hadhara.
“Hakuna maandalizi yoyote na mimi nilikuwapo hapo. Wapo watu wameona kazi za Rais kwamba anachokifanya, anakifanya kwelikweli,” alisema Polepole alipohojiwa na gazeti hili jana.
“Amezungumzia mipango, mikakati, kama ni rushwa, ameishughulikia. Wanaamua kujitokeza kwenye mikutano na kusema huku tuliko ni mizengwe. Tunaona tuje tuungane na wewe (Rais Magufuli).”
Alipoulizwa ni kwa nini Rais Magufuli aliuliza watu wanaotaka kujiunga na wakajitokeza wakati huo wakati haikuwa ni maandalizi, Polepole alisema Rais kwa ushawishi wake katika utekelezaji wa sera na ilani ya chama, imekuwa sababu ya kujitokeza hadharani bila kushawishiwa.
Baadhi ya madiwani wengine waliojiuzulu nyadhifa zao kwa maelezo kuwa wanamuunga mkono Rais Magufuli ni Credo Kifukwe (Murieti), Anderson Sikawa (Leguruki), Emmanuel Mollel (Makiba), Greyson Isangya (Maroroni) na Josephine Mshiu (Viti Maalumu) na Solomon Laizer (Ngabobo).
No comments:
Post a Comment