Meneja wa TTCL Mkoa wa Arusha na Manyara Bwana Brown Japhet (wa pili kushoto) akifafanua jambo mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani) ilipofanya ziara ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini kwenye kijiji cha Sigino kata ya Singo iliyopo wilaya ya Babati Mjini mkoani Manyara. Wa kwanza kushoto ni Mtendaji Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Eng. Peter Ulanga.
Kaimu Mkurugenzi wa kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Arusha Bwana Philemon Joel (wa kwanza kulia) akitoa maelezo kwa wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu (hawapo pichani) kuhusu utayari wa kampuni hiyo kujenga mnara kwenye kijiji cha Timbolo, kata ya Sambasha Wilaya ya Arumeru mkoani Manyara baada ya mgogoro wa ardhi kumalizika. Wa kwanza kushoto ni Mkuu wa Idara ya Uendeshaji wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote Bwana Albert Richard.
Mwenyekiti wa kijiji cha Timbolo, kata ya Sambasha wilaya ya Arumeru mkoani Manyara Bwana Samwel Saning’o akisisitiza umuhimu wa uwepo wa mawasiliano vijijini mbele ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu wakati wa ziara ya Kamati kwenye kijiji hicho ya kukagua upatikanaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King (wa kwanza kushoto) na wajumbe wengine wa Kamati wakiwa wamekalia mnara wa Halotel wakipata maelezo kutoka kwa Kaimu Mkurugenzi wa Kampuni ya Halotel Bwana Philemon Joel (hayupo pichani) kuhusu utayari wa kampuni hiyo kujenga mnara baada ya mgogoro wa ardhi kumalizika kwenye kijiji kijiji cha Timbolo, kata ya Sambasha Wilaya ya Arumeru mkoani Arusha
NA WUUM, ARUSHA
SERIKALI kupitia Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote imeendelea na kazi ya kuhakikisha kuwa wanachi wote waishio vijijini na maeneo yasiyo na mvuto wa kibiashara wanapata huduma za mawasiliano kwa wakati ili kuweza kuchangia ukuaji wa uchumi na upatikanaji wa huduma za kijamii na maendeleo ya taifa kwa ujumla.
Hayo yameelezwa na Mtendajii Mkuu wa Mfuko wa Mawasiliano kwa Wote (UCSAF) Eng. Peter Ulanga wakati wa ziara ya wajumbe wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu ya kukagua ujenzi wa minara ya simu za mkononi na upatikanaji wa huduma za mawasiliano kwenye maeneo mbalimbali vijijini ya mkoa wa Arusha na Manyara. Eng. Ulanga amesema kuwa migogoro ya ardhi kwenye baadhi ya vijiji mbalimbali nchini inachangia ucheleweshaji wa ujenzi wa minara na ufikishaji wa huduma za mawasiliano vijijini.
Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kupitia Mfuko huu uliweka lengo la kufikisha mawasiliano kwenye vijiji 4,000 nchi nzima ifikapo mwezi Novemba mwaka huu. Uwepo wa migogoro ya ardhi unachangia kuchelewesha kampuni za simu zilizopatiwa ruzuku na Serikali kujenga minara, “mgogoro wa ardhi kwenye kijiji cha Timbolo kata ya Sambasha Wilayani Arumeru umeichelewesha kampuni ya Halotel kujenga mnara na hivyo wananchi wa kata hii kukosa mawasiliano kwa kuwa mgogoro huo umechukua zaidi ya miaka miwili kukamilika mahakamani,”amesema Eng. Ulanga.
Kaimu Mkurugenzi wa kampuni ya simu ya Halotel wa Mkoa wa Arusha Bwana Philemon Joel amesema kuwa mahakama iliweka zuio la ujenzi wa mnara kwenye eneo la kijiji cha Timbolo kata ya Sambasha ambapo kesi ya mgogoro huo umechukua miaka miwili kufanyiwa maamuzi kwenye ngazi ya mahakama. “Tumekuwa tukienda mahakamani mara kwa mara na kupigwa tarehe kuambiwa Hakimu hayupo na mara nyingine inapita miezi minne bila ya kesi kusikilizwa hivyo imetuchelewesha kuanza ujenzi,”amesema Bwana Joel.
Naye Mwenyekiti wa kijiji cha Timbolo, kata ya Sambasha Bwana Samwel Saning’o amesema kuwa Serikali ya kijiji ilisimama na kusema kuwa wanataka mawasiliano na sio utalii kwa kuwa kulikuwa na mgogoro baina ya mmiliki wa eneo la jirani na eneo la mwingine ambapo mnara unatakiwa kujengwa. Bwana Saning’o amemshukuru sana Mkuu wa Wilaya ya Arumeru Bwana Alexandra Mnyeti kwa kuingilia kati mgogoro huu, kusimamia na kuhakikisha kuwa unakamilika ili wananchi waweze kupata mawasiliano. Eng. Ulanga amesema ujenzi wa mnara wa Halotel kwenye eneo hili hauwezi kukamilika mwezi Novemba mwaka huu, hivyo sisi kama Mfuko wa UCSAF tutawapatia muda wa ziada ili waweze kukamilisha ujenzi wa mnara na wananchi waweze kupata mawasiliano. Pia Eng. Ulanga amewataka wanachi wa vijiji husika kushirikiana na kampuni za simu kulinda miundombinu ya mawasiliano na minara ili mawasiliano yaweze kupatikana muda wote.
Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ametoa rai kwa mamlaka zinazosimamia haki na vyombo vya ulinzi viambata vya Jeshi la Polisi na mahakama kufanya uchunguzi na kuendesha kesi kwa wakati ili kuharakisha kutoa haki. “Ukichelewa kutoa shauri la hukumu kwa jambo la umma linalogusa maslahi ya wananchi unachelewesha maendeleo ya wananchi,”amesema Prof. Norman Sigalla King. Ameongeza kuwa wananchi washirikiane na kampuni za simu za mkononi kulinda minara na kutoa ardhi bila migogoro ili waweze kupata huduma za mawasiliano kwenye vijiji vyao kwa wakati.
Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa Kamati ya Bunge ya Miundombinu Prof. Norman Sigalla King ameitaka Kampuni ya Simu Tanzania (TTCL) kukamilisha ujenzi wa minara yake ya simu kwa wakati kwenye vijiji mbalimbali nchini ili wananchi wa maeneo husika waweze kupata huduma za mawasiliano. Hayo ameyasema Prof. Norman Sigalla King wakati wa ziara ya Kamati yake walipotembelea kijiji cha Sigino kata ya Singo iliyopo wilaya ya Babati Mjini mkoani Manyara.
Naye Meneja wa TTCL Mkoa wa Arusha na Manyara Bwana Brown Japhet amesema kuwa TTCL imekamilisha ujenzi wa minara kwenye vituo vyote vya Mkoa wa Arusha na viko hewani wananchi wanapata mawasiliano. Bwana Japhet ameilieza Kamati kuwa kwa vituo viwili vilivyobaki vya TTCL kama pale Saitabau, Arusha kulikuwa na mgogoro wa ardhi ambapo Serikali ya Mkoa imeingilia kati na kumaliza mgogoro huo na vituo vingine viwili vipo kwenye hifadhi ya Taifa ya Ngorongoro ambapo vinasubiri tathmini ya mazingira ikamilike ili ujenzi wa minara kwenye vituo hivyo uweze kuanza na suala hili limefikishwa Wizara ya Maliasili na Utalii ili liweze kukamilishwa.
Prof. Norman Sigalla King ameyataka makampuni ya simu kuhakikisha kuwa mawasiliano yanasambaa nchi nzima. Pia ameitaka TTCL kukamilisha ujenzi wa minara yake kwa wakati na kuhakikisha kuwa kila wanapopatiwa ruzuku na Serikali wakamilishe jukumu lao kwa wakati na wafanye kazi kwa ushindani. Ameoneza kuwa Kamati yake imeridhishwa na kazi nzuri inayofanywa na TTCL. Kamati inazitaka mamlaka nyingine zinazohusika na ujenzi wa minara na upatikanaji wa mawasiliano vijijini washirikiane kwa pamoja na kufanya maamuzi kwa wakati ili kuwawezesha wananchi kupata huduma za mawasiliano vijijini kwa wakati.
No comments:
Post a Comment