ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, October 31, 2017

JUMIA TANZANIA WAZINDUA KAMPENI YA SIKU YA BLACK FRIDAY KWA MIKOA SITA

Meneja Mauzo wa Jumia Tanzania, Iddy Mkumba akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa Black Friday utakaoweza kutoa punguzo la asilimia 70 kwa bidhaa atakayoinunua mteje kupitia tovuti ya Jumia Tanzania  itakayoanza mwezi wa Novemba 24 hadi Desemba 04 mwaka huu kwa mikoa ya Kilimanjaro, Arusha, Dar es Salaam, Dodoma, Iringa, Mwanza,Morogoro, Mara na Zanzibar.
Afisa Masoko na Mahusiano ya Jamii wa Jumia Travel, Geofrey Kijanga, akizungumza na waandishi wa habari kuhusu Jumia Travel inavyotoa huduma za malazi na namna walivyopunguza bei kwa msimu huu wa sikukuu leo kwenye ofisi za Jumia Tanzania jijini Dar Es Salaam.
Maneja Masoko wa Jumia Tanzania, Albany James(kulia) akizungumza na waandishi wa habari kuhusu jinsi Kampuni ya Jumia Tanzania akizungumzia kuhusu siku ya Black Friday itakayofanyika kwa takribani siku kumi na moja (11) kuanzia mwezi wa Novemba 24 hadi Desemba 04 mwaka huu.
Mkutano ukiendelea kwenye ukumbi wa ofisi ya Jumia Tanzania jijini Dar es Salaam leo

Ikiwa imebaki takribani miezi miwili mwaka 2017 kuisha, Jumia Tanzania imejizatiti kuja na kampeni iliyopewa jina la ‘BLACK FRIDAY’ ambayo itawawezesha wateja wake kufanya manunuzi ya bidhaa mbalimbali mtandaoni kwa punguzo la mpaka alisimia 70 kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 4 mwaka huu.

Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu ujio wa kampeni hiyo Meneja Mauzo wa Jumia Tanzania, Bw. Idd Mkumba amebainisha kuwa kutokana na mafanikio makubwa ya kampeni hiyo iliyofanyika mwaka jana na kushuhudia watanzania wakifanya huduma za mtandaoni ambapo takribani oda 600 kwa siku wameona ni vema kuirejesha tena kwa kishindo mwaka huu.

“Mwaka 2016 ulikuwa ni wenye mafanikio kwa upande wa kampeni yetu ya BLACK FRIDAY kwani ndani ya muda wa siku tano tuliyoifanya wateja wengi waliweza kufanya manunuzi mtandaoni. Hivyo basi kwa mwaka huu tena tumeiboresha Zaidi kwa kuongeza siku kutoka tano mpaka 11 ambapo kampeni itaanza rasmi kuanzia Novemba 24 mpaka Desemba 4. Na kwa kuongezea hapo ni kwamba safari hii wateja wa Dar es Salaam hawatofaidika pekee yao kwani tumejitanua Zaidi mpaka mikoa mingine kwa mara ya kwanza na kuzifikia sehemu za Visiwani Zanzibar, Dodoma, Mwanza, Morogoro, Arusha, Kilimanjaro, Iringa na Musoma,” alisema Bw. Mkumba.

Meneja Mauzo huyo wa Jumia Tanzania aliendelea kwa kufafanua kuwa, “Lengo kubwa la kampeni hii ni kuhakikisha kwamba tunawajengea uwezo na kuwarahisishia watanzania kufanya huduma mbalimbali kwa njia ya mtandao mahali popote walipo huku wakiendelea na shughuli zao. Tanzania ni mojawapo ya taifa linaloendelea Afrika na duniani likiwa na watumiaji wa simu za kisasa na mtandao wa intaneti wanaoongezeka kila kukicha. Hivyo basi nasi tunaitumia fursa hiyo kwa kuwahamisisha watanzania kuitumia teknolojia hiyo kwa manufaa Zaidi, ambapo badala ya kutumia muda mwingi kwenda madukani wanaweza kufanya hivyo wakiwa palepale walipo.”

“Katika kuwaondoa hofu wateja ambao wanahofia kwamba pengine bidhaa zinaweza kuwa hazina ubora kutokana na ukubwa wa ofa tunazotoa, ni kwamba Jumia Tanzania tunafanya huduma zetu kwa sera ya kulipia pale unapopokea bidhaa yako. Hii humpatia mteja kujiridhisha kwamba bidhaa aliyoiagiza ni sahihi ndipo alipie. Na kwa kuongezea, ada ya malipo ya kufikishiwa mzigo kwa wateja wetu popote walipo itashuka ili kuhamasisha manunuzi Zaidi. Kwa kumalizia kuhusiana na kampeni ya BLACK FRIDAY ambayo itawapatia fursa wateja kupata punguzo la bei mpaka la asilimia 70, tumeingia ubia na makampuni kadhaa makubwa ya utoaji wa huduma na uuzaji wa bidhaa kama vile Samsung, Startimes, Tronic,… Lakini pia kutokana na kuanza kwa huduma kwenye mikoa mipya niliyoiorodhesga hapo juu, tumetoa ofa kwa wateja watakaofanya manunuzi ya kuzidi shilingi 100,000 watajipatia punguzo la 50% ambapo itawabidi watumie neonsiri J695D,” alihitimisha Bw. Mkumba.

Akifafanua Zaidi juu ya dhana nzima ya kampeni hiyo, Meneja Masoko wa Jumia Tanzania, Bw. Albany James amesema kuwa utamaduni wa BLACK FRIDAY umeanzia nchini Marekani ambapo makampuni wafanyabiashara hutoa punguzo la bei za bidhaa na huduma mbalimbali ili kuukaribisha msimu wa mapumziko na Krisimasi.

“Utamaduni huu wa kufanya punguzo kubwa la bei mbalimbali za bidhaa na huduma ulianzia nchini Marekani na kushika kasi sehemu zingine duniani kutokana na faida kubwa kwa wafanyabiashara na wateja kwa ujumla. Ni kipindi ambacho watu wengi hufanya maandilizi ya msimu wa sikukuu za Krisimasi na Mwaka Mpya. Na nadhani utamaduni huo hata kwa sisi watanzania pia tunautumia hivyo basi kupitia Jumia Tanzania wateja wataweza kununua bidhaa mbalimbali muhimu kwa msimu huo kama vile za nyumbani, umeme, mavazi, vyombo vya kupikia nakadhalika. Kwa hiyo ningependa kuwatoa hofu wateja wetu kwamba ni bei za bidhaa ndizo zitakazopungua na sio ubora kama wengi wanavyodhahania,” alisema na kumalizia Bw. James.

Katika kunogesha kampeni hii Jumia Tanzania pia imeshirikiana na makampuni tanzu ya Jumia hapa nchini kama vile Jumia Travel na Jumia Food ambayo nayo yanajihusisha na huduma kwa njia ya mtandao. Ushirikiano huo utawapatia faida wateja watakaokuwa wakifanya manunuzi mtandaoni kupata ofa kama vile za malazi ya bure pamoja na punguzo kubwa kwa hoteli mbalimbali za kifahari nchini.

Akizungumza kwa upande wake Meneja Uhusiano wa Umma na Masoko wa Jumia Travel Tanzania, Bw. Geofrey Kijanga ameelezea kuwa wao kama watoaji wa huduma za hoteli kwa njia ya mtandao mbali na kutoa ofa ya kulala bure kwenye hoteli kwa wateja lakini pia watatoa punguzo kubwa la bei za huduma za malazi ambalo litadumu mpaka mwezi Desemba.

“Tunafahamu kwamba tunaelekea kuumaliza mwaka ambao hugubikwa na msimu wa mapumziko na sikukuu za Krisimasi na Mwisho wa Mwaka, suala la watu kwenda kutembelea na kupumzika sehemu mbalimbali ni muhimu. Katika kulirahisisha hilo Jumia Travel itatoa punguzo kubwa la huduma za malazi kwa hoteli inazofanya nazo kazi nchini. Kwa hiyo mteja hatowaza kuhusu gharama za malazi popote atakaposafiri yeye au pamoja na familia yake. Hivyo basi ni muda muafaka kwa watanzania kuzitumia ofa hizi kwani huwa ni za kweli na hurahisisha gharama kubwa ambazo wanaweza kuziingia kuzipata kwa njia nyinginezo za kawaida,” alisema na kuhitimisha Bw. Kijanga.

Hii ni fursa kwa watanzania wote kwa ujumla kujiaandaa vema na msimu wa mapumziko na sikukuu unaokuja kwa kufanya manunuzi ya gharama nafuu Zaidi mahali popote walipo kuanzia Novemba 24 na kuendelea kwa siku 11 mwaka huu. Ili kufahamu Zaidi na kujua mengi juu ya ofa zitakazotolewa watanzania wanatakiwa kuwa kutembelea mitandao ya Jumia Tanzania pamoja na kurasa zao za mitandao ya kijamii. Lakini pia kutakuwepo na zawadi mbalimbali kupitia njia za vocha na kuponi kwa wale watakaokuwa wakifuatilia kurasa hizo kwa karibu na kujibu maswali mbalimbali.

No comments: