ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 7, 2017

SERIKALI IMETOA BURE MBEGU NA VIUATILIFU KWA AJILI YA KILIMO CHA PAMBA KWA MKOA WA SINGIDA.

 Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi (katikati) akimkabidhi mmoja kati ya wa wakulima wa Pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama kilo kumi za mbegu za zao la pamba zilizotolewa bure na Serikali kwa wakulima hao. Kushoto kwa Mkuu wa Mkoa ni Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga.
 Mkulima wa Pamba Bi Johari kutoka kijiji cha Kinyagiri Wilayani Mkalama akibeba mbegu za Pamba kilo kumi alizokabidhiwa na Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi, mbegu hizo zimetolewa bure kwa wakulima wa Pamba Mkoa wa Singida.
 Mama Devid Mkulima wa Pamba wa Kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama akijifunza kwa vitendo namna ya kuandaa kamba inayotumika kuonyesha vipimo vya upana na urefu katika kupanda pamba badala ya kilimo cha mazoea cha kumwaga mbegu bila kufuata kipimo chochote.
 Wakulima wa Pamba wa Kijiji cha Lyelembo Wilayani Mkalama wakiwasikiliza Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi na Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini Marco Mtunga (hawapo pichani) kabla ya kupewa mbegu za pamba zilizotolewz bure.
 Wakulima wa pamba wa kijiji cha Kinyangiri Wilayani Mkalama wakimfuatilia kwa makini mtaalam kutoka Bodi ya Pamba Nchini akiwaelekeza namna ya kupuliza dawa ya kuuwa wadudu waharibifu wa pamba, viuatilifu hivyo vitatolewa bure na serikali kwa wakulima wote wa pamba Mkoani Singida.

Serikali imeahidi kutoa bure pembejeo za kilimo kwa wakulima mbali mbali wa zao la pamba mkoani Singida kuanzia msimu huu wa kilimo ikiwa ni moja ya juhudi za kuhamasisha na kufufua kilimo hicho mkoani hapa.  
Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Bodi ya Pamba nchini, Marco Mtunga ameeleza hayo juzi katika vijiji vya Kinyangiri na Lyelembo wilayani Mkalama katika siku ya kwanza ya ziara yake ya siku mbili kuhimiza Kilimo cha pamba mkoani Singida. 
Kwa mujibu wa Mkurugenzi huyo, Kampuni ya Biosustain iliyopo mjini hapa imepewa jukumu la kuleta na kusambaza mbegu na madawa yote yahusuyo kilimo cha pamba bure na kwamba gharama ya pembejeo hizo italipwa na Serikali. 
Kutokana na hilo, Mkurugenzi huyo amewataka Wakulima kutumia vyema fursa hiyo kwa kulima mashamba makubwa zaidi lakini pia kwa kuzingatia tija na ubora wa pamba. 
Amesema kuwa Wakulima wataweza kufanya hivyo tu iwapo pia watawatumia kikamilifu wataalamu wao wa kilimo na kufuata Kanuni na Taratibu za kilimo bora. 
“Mmepewa upendeleo maalum, kazi yenu sasa ni kulima tu, malipo ya mbegu na viuatilifu vyote italipwa na Serikali. Hapa hakuna kisingizio cha kushindwa kulima”, amesema Mtunga na kuongeza;
“Pandeni vizuri ili wakati mnatumia dawa, kiwango kikubwa cha dawa kisipotee bure maana kama hukupanda kwa mstari lazima kutakuwa na ugumu wa kupulizia mimea yako. Jengeni utamaduni wa kuwatumia wataalamu wa kilimo kama ilivyo kwa wafugaji mifugo yao inapopatwa na maradhi”.  
Aidha, amewataka wakulima wa zao hilo kuhakikisha wanang'oa masalia yote ya misitu ya pamba na kuichoma moto kwa kuwa, kwa kuacha kufanya hivyo wanaruhusu wadudu waliomo kwenye masalia kuendelea kunenepeana na hivyo kuhatarisha mazao mapya yanayopandwa.  
Mkurugenzi huyo amewasihi wakulima kuacha kuchanganya kilimo cha pamba na mazao mengine akisema kuwa tafiti zinaonesha pamba iliyochanganywa na mazao mengine hutoa vitumba vitatu tu ikilinganishwa na vitumba 10 kwa kilimo cha pamba iliyolimwa peke yake. 
Wakulima wa zao hilo wamemueleza Mkurugenzi huyo kuwa, moja ya sababu za kushuka kwa uzalishaji pamba kwenye maeneo yao ni pamoja na bei kuwa ndogo kwa kisingizio cha Soko la Kimatafa kushuka na kuchezewa mizani wanazotumia kupima mazao yao, hali inayowapunja kimapato.  
Hata hivyo, wamejibiwa kuwa suluhisho la kuchezewa mizani lipo mikononi mwao ili mradi tu wajenge tabia ya kuhoji mara moja wanapoona mambo yanaenda isivyo badala ya kusubiri hadi siku ya vikao.
Wakati huohuo Mkuu wa Mkoa wa Singida Dkt Rehema Nchimbi amewataka watendaji wote wa serikali na Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoani Singida kulima ekari moja ya pamba kila mmoja ili kuamsha hamasa kwa wananchi wengine.
Dkt Nchimbi ameongeza kwa kuwataka watendaji hao kuliweka zao la pamba kama ajenga katika vikao vyao, huku akiwataka viongozi wa dini na vikundi vya kwaya kuonyesha mfano kwa kulima vizuri pamba.
Ameongeza kuwa vijana wanaocheza vijiweni ‘pooltable’ waache mara moja na kujikita katika kilimo cha pamba kwa kuwa ni chanzo kikubwa na cha uhakika cha kujipatia fedha na hivyo kuchangia kukuza uchumi.
Aidha amewataka wakulima wa pamba kuwasikiliza wataalamu na sio kupanda kwa mazoea huku akishauri kuwa mikutano yote inayohusu kilimo cha pamba ifanyike katika mashamba ya wakulima.
Dkt Nchimbi ameeleza kuwa kauli mbiu mpya ya kilimo cha pamba kwa Mkoa wa Singida ni, ‘Singida Mpya, kwa Pamba yenye Tija’.

No comments: