Kaimu Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe.
Na Daniel Mbega
SHIRIKISHO la Vyama vya Ushirika Tanzania (TFC) limeanza
zoezi la kukusanya taarifa na kuhakiki wanachama ili kuimrisha kanzidata yake.
Akizungumza
na MaendeleoVijijini, Kaimu
Mkurugenzi wa Maendeleo ya Ushirika wa TFC, Bw. Henry Mwantwinza Mwimbe, amesema
zoezi hilo litarahisisha utendaji wa shirikisho katika kuwafikia wanachama wake
pamoja na kujua changamoto na vipaumbele ili kusukuma mbele maendeleo ya
kiuchumi.
“Tunahitaji
tupate idadi halisi ya wanachama wetu kwa sababu tunaamini kwa sasa
wameongezeka na hiyo itatusaidia kuweza kuwafikia kwa urahisi tukitambua kila
mwanachama anajishughulisha na nini, na nini changamoto zake pamoja na
vipaumbele,” alisema Mwimbe.
Mwimbe amesema
kwamba, jukumu la TFC ni kusimamia
vyama vya ushirika, lakini katika wakati huu ambao taifa linahitaji kujenga
uchumi wake na kuongeza kipato cha kila Mtanzania ili kufikia uchumi wa kati,
ni vyema kutambua na kufuatilia kwa karibu shughuli zinazofanywa na wanachama
hao.
Amesema asilimia
zaidi ya 80 ya wanachama wao wanajihusisha na shughuli za kilimo ambapo
wamekuwa wakikabiliwa na changamoto mbalimbali zikiwemo za ukame, pembejeo
pamoja na masoko, hivyo kwa kuimaridha kanzidata yao watakuwa na uwezo wa
kutambua fursa na changamoto zilizopo katika maeneo yote.
“Kwa kuwa
tutakuwa na mawasiliano yote ya wanachama, tunakusudia kuwaunganisha na masoko
ya ndani na yale ya nje kupitia simu za mkononi,” amesema Mwimbe.
Aidha,
amesema kwamba, kwa kuimarisha kumbukumbu hizo itawasaidia hata wao TFC
kutambua makisio ya uzalishaji wa mazao mbalimbali kwa msimu.
“Kumbukumbu
hizi ni muhimu, tunaweza kuwa tunajua kwamba kwa msimu huu, mathalan tumbaku
limelimwa katika eneo lenye ukubwa gani na makisio ya mavuno ni kiasi gani,
vivyo hivyo kwa mazao mengine kama kahawa, pamba, mahindi, mbaazi, ufuta,
korosho na mengineyo.
“Kama
tukipata taarifa kutoka nje kwamba kuna watu au kampuni inahitaji tani kadhaa
za pamba ni rahisi kuwaunganisha wananchama wetu moja kwa moja na kampuni hizo
na wakauza kwa uhakika zaidi,” amesema.
Kuhusu TFC
TFC ndiye
mrithi wa uliokuwa Muungano wa Vyama vya
Ushirika Tanzania (CUT) na ilibadilishwa kufuatia sera mpya na kuanzishwa
kwa Sheria mpya ya Ushirika ya mwaka 2003 ambayo ilikuwa mbadala wa Sheria ya
Ushirika ya mwaka 1991 iliyokuwa inaeleza kwamba vyama vya ushirika vilikuwa
kama sehemu ya vikundi vya kisiasa vya chama tawala.
Kwahiyo, Sheria
mpya ya Ushirika ya mwaka 2003 inaelezea tu usimamizi wa vyama vya ushirika na
wanachama wanastahili kuwa na sauti na ushiriki wa moja kwa moja.
TFC ni
chombo kinachojitegemea kisichofungamana na upande wowote kikiwa kinamilikiwa
na wanachama wenyewe katika mukhtadha wa kufuata sheria na kanuni za kimataifa
za ushirika.
Kwahiyo, TFC ni mwanachama wa Umoja wa
Kimataifa wa Ushirika (International Co-operative Alliance - ICA), Shirikisho
la Wakulima Afrika Mashariki (East African Farmers Federation - EAFF), Shirikisho
la Kimataifa la Wazalishaji Bidhaa za Kilimo (International Federation of
Agricultural Producers - IFAP) na Committee of Artisanal and Workers
Cooperatives (CICOPA).
Kitaifa, TFC
ni mwanachama mwanzilishi wa Tanzania Private Sector Foundation (TPSF) na Baraza
la Kilimo Tanzania (Agricultural Council Tanzania - ACT), zamani likijulikana
kama Tanzania Chamber of Agriculture and Livestock.
TFC inashirikiana
na wadau kadhaa wa kitaifa na kimataifa kama wizara za Seriali, Shirika la Kazi
Duniani (ILO), Shirika la Chakula na Kilimo la Umoja wa Mataifa (FAO), Shirika
la Kimataifa la Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi
Tanzania (TUCTA), Muungano wa Vikundi vya Wakulima Tanzania (MVIWATA), Shirika
la Maendeleo ya Viwanda Vidogo (SIDO), na kadhalika.
Wanachama wa TFC
TFC ilisajiliwa
rasmi Desemba 8, 1994 ikiwa na Hati ya Usajili Namba 5503 ambapo wanachama
waanzilishi walikuwa 13 tu.
Pamoja na
kwamba hivi sasa wanakusanya na kuhakiki taarifa kwa ajili ya kanzidata, MaendeleoVijijini
inafahamu kwamba, hadi kufikia mwaka 2015 TFC ilikuwa na vyama wanachama 3,339 Tanzania
Bara vyenye wanachama mmoja mmoja zaidi ya milioni 1.5.
No comments:
Post a Comment