Advertisements

Thursday, November 23, 2017

TUNDU LISSU KUSAFIRISHWA KWA MATIBABU NJE YA AFRIKA

Mbunge wa Singida Mashariki (Chadema), Tundu Lissu anatarajiwa kusafirishwa nje ya nchi kwa matibabu mwezi mmoja kuanzia sasa.
Familia yake imesema Lissu baada ya kupata matibabu nje ya nchi amepanga kufanya mambo matano akirejea salama .
Akizungumza na waandishi wa habari leo Alhamisi Novemba 23, kaka wa Tundu Lissu, Wakili Alute Mughwai alisema taratibu za kumsafirisha nje ya nchi zimeanza.
Lissu, ambaye ni mjumbe wa Kamati Kuu na mwanasheria mkuu wa chadema amelazwa katika Hospitali ya Nairobi nchini Kenya baada ya kushambuliwa kwa risasi zaidi ya 30 alipokuwa akirejea nyumbani kwake Area D mjini Dodoma Septemba7.
"Awamu ya tatu ya matibabu yake ni maalumu sana kwani itahusu pia mazoezi ambayo kama haitafanyika vyema ataweza kupata ulemavu wa kudumu,"alisema.
Hata hivyo, alisema Lissu atapelekwa nje kwa ndege ya kawaida tofauti na hali yake ya awali alipotakiwa kusafirishwa na ndege maalumu za wagonjwa.
"Itatolewa taarifa ni lini ataondoka kwa matibabu na atakwenda nchi gani, hasa baada ya kupata ushauri wa mwisho wa madaktari katika hospitali Nairobi," alisema.

Mambo matano ya Lissu akirejea nchini
Mughwai alisema amezungumza na Lissu akiwa Hospitali Nairobi na amemueleza kuwa akirejea tu nchini, kuna mambo makubwa matano ambayo atafanya.
Alisema jambo la kwanza, ambalo atafanya ni kwenda katika Hospitali ya Mkoa wa Dodoma kuwashukuru madaktari na wauguzi wa hospitali hiyo kwa kuokoa maisha yake siku aliyopigwa risasi.
Wakili Mughwai alisema Lissu amemwambia baada ya hapo atakwenda kanisani na msikitini kumshukuru Mungu kwa kuokoa maisha yake kwa kufanya ibada maalumu.
"Baada ya ibada, tutaangalia utaratibu kifamilia kama itawezekana kwenda kufanya matambiko kwenye makaburi ya wahenga wetu 76 waliofariki katika vita miaka 200 iliyopita," alisema.
Alisema baada ya hapo, anatarajia kuendelea kufanya kazi zake za siasa na uwakili pale alipoishia kwa ari kubwa .
Wakili Mughwai alisema jambo la tano atahakikisha anasimama na kupambana kisheria na watu waliotaka kukatisha maisha yake baada ya kumpiga risasi.
"Amesema atahakikisha anasimamia jambo hili kwa uwezo wake wote ili kuhakikisha wanafikishwa katika vyombo vya sheria waliohusika na uovu huo," alisema.
Familia yataka Lissu akahojiwe Nairobi
Akizungumzia juu ya upelelezi wa shauri la Lissu, Mughwai alisema bado msimamo wao upo palepale wanaomba wapelelezi kutoka nje ya nchi washirikiane na wapelelezi wa ndani kuwakamata watuhumiwa.
Alisema ingawa familia ya Lissu iliandika barua tangu Septemba 16, kutaka wapelelezi wa kimataifa na kujibiwa na mwanasheria mkuu Septemba 20 kuwa jukumu la upelelezi ni la polisi.
"Tunataka wapelelezi wa nje kushirikiana na wa ndani kwa sababu hatuna imani na upelelezi kutokana na kasi ndogo kwani hadi sasa wamekuwa wakieleza kukwama upelelezi kutokana na kutomuhoji dereva wa Lissu,"alisema.
Hata hivyo, alisema kwa sasa Lissu anaweza kuongea mwenyewe hivyo, jeshi la polisi linaweza kwenda Nairobi kumuhoji na atawapa maelezo yote ikiwepo watu ambao aliwatambua.
"Bila shaka Lissu atawaeleza watu hao, walimshambulia kwa sababu gani,"alisema.

Familia yaelezea gharama
Katika hatua nyingine, Mughwai alisema Oktoba 2, familia ya Lissu ilikutana na viongozi wa bunge kujadili matibabu yake ambayo ni haki yake kisheria.
Alisema baada ya mazungumzo hayo, Oktoba 8, familia iliandika barua rasmi kwa katibu wa bunge kwa kuzingatia sheria ya bunge namba 14 kifungu cha 24 kuhusu stahiki za mbunge.
Alisema barua hiyo, ilipelekwa bungeni kwa kutumia shirika la kubeba mizigo na vifurushi la DHL na kupokelewa Oktoba 19 na baadaye aliwasiliana na Spika Job Ndugai na kumweleza juu ya barua hiyo na aliahidiwa kuwa suala hilo litashughuliwa.
Hata hivyo, alisema familia haijapata mrejesho tangu wakati huo hadi Novomba 11, alipoamua kumpigia katibu mpya wa bunge baada ya kushauriwa na Spika Ndugai ambaye aliahidi kufuatilia.
"Hivyo hadi sasa bado Bunge halijaanza kugharamia matibabu ya Lissu kama sheria inavyosema na Lissu amekuwa akitibiwa kwa michango ya watu mbali mbali," alisema
Alisema michango hiyo ambayo inakusanywa katika akaunti maalumu ya Chadema na pia kupitia chama cha mawakili(TLS) ndio hadi sasa inatumika.
"Tutaendelea kulitaka Bunge kugharamia matibabu kwani sio suala la hiari, ni haki ya mbunge lakini pia tunaomba wananchi waendelee kuchangia matibabu ya Lissu kupitia akaunti iliyotolewa na Chadema, chama cha TLS na kwa familia"alisema

Akanusha mgawanyiko juu ya matibabu
Katika hatua nyingine, Mughwai alisema, familia ya Lissu, Chadema na chama cha Mawakili wa Tanganyika(TLS), hawana mgawanyiko wowote juu ya matibabu ama hatua zinazoendelea za kumtibu Lissu.
Wakili Mughwai alisema wanasikitishwa na taarifa kuwa familia imegawanyika juu ya uamuzi wa kuliomba bunge kugharamia matibabu ya Lissu.
"Tupo kitu kimoja wote familia yetu tupo pamoja kwa yote na Lissu anajua hatua zote kwani hata makamishna wa bunge walipomtembelea Oktoba 23 aliwauliza kuhusu stahiki zake kama mbunge,"alisema.
Tundu Lissu alipigwa risasi na watu wasiojulikana akiwa nje ya nyumba yake akirejea kutoka vikao vya bunge Dodoma, Septemba 7 na kukimbizwa hospitali ya Nairobi kwa matibabu ambapo hadi sasa anapatiwa matibabu.

Chanzo: Mwananchi

No comments: