Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na
wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake
mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta
hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa
utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto
ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Mej. Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu,
Dk. Aloyce Nzuki (kulia).
Na Hamza Temba, Dodoma
Serikali imesikia kilio cha wadau wa sekta ya uwindaji wa
kitalii nchini na kuamua kuongeza muda wa miaka miwili ya umiliki wa leseni za vitalu
95 vya uwindaji wa kitalii ambazo zilikuwa ziishe muda wake tarehe 31 Desemba
mwaka huu (2017).
Uamuzi huo umefikiwa na Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk.
Hamisi Kigwangalla wakati wa kikao cha majumuisho na watendaji wa Wizara hiyo
muda mfupi baada ya kumalizika kwa mkuano wa wadau wa sekta hiyo ulioandaliwa
na Wizara hiyo mjini Dodoma jana.
Akizungumzia uamuzi huo Dk. Kigwangalla alisema, lengo ni kuwapa
muda wawekezaji hao ili waweze kujiandaa na mabadiliko ya mfumo mpya wa utowaji
wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada ikiwemo kurudisha
baadhi ya gharama za uwekezaji walizoweka katika vitalu hivyo.
Awali akizungumza katika mkutano huo wa wadau Mwenyekiti wa
Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini, Michael Mantheakis
alimuomba Waziri Kigwangalla kuwaongezea muda wa umiliki wa leseni zao kuanzia
miaka mitano au mitatu na nusu ili waweze kurudisha gharama za uwekezaji walizowekeza
katika vitalu hivyo ikiwemo ujenzi wa miundombinu, makambi na vifaa vyake
pamoja na maji.
Hata hivyo, Waziri Kigwangalla aliweka wazi msimamo wa Serikali
wa kutimiza azma yake ya kuingia kwenye utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu
vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na kusema kuwa kamwe haitorudi nyuma
na kwamba utekelezaji wa zoezi hilo hauwezi kusubiri muda mrefu kiasi hicho.
Akizungumzia kuhusu hatua ya utekelezaji wa utaratibu huo,
Waziri Kigwangalla alisema kwa sasa taratibu za kuandaa Sheria za usimamizi zinaendelea
na zinatarajiwa kukamilika mwezi Februari 2018 pamoja na kanuni zake
zinazotarajiwa kukamilika mwezi Aprili 2018.
Aidha, alisema mfumo maalumu wa kielektroniki unaandaliwa ambapo
maombi yote ya leseni za umiliki wa vitalu vya uwindaji kwa njia ya mnada yatafanyika
kwa uwazi kwa njia ya mtandao.
Alisema baada ya kukamilika kwa taratibu zote na mfumo huo mpya
wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada na
maombi kuwasilishwa, mnada wa kwanza utaanza tarehe 1 Julai, 2018 kwa kuanza
kunadi vitalu 61 ambavyo kwa sasa havina wawekezaji.
Mnada wa pili utafanyika mwaka 2020 baada ya kuisha kwa muda huo
wa nyongeza wa miaka miwili ukihusisha vitalu 95 vilivyoongezewa muda wa
umiliki wa leseni pamoja na vitalu vingine endapo vitabaki katika mnada huo wa
kwanza kwa sababu mbalimbali.
Alisema sheria na kanuni zinazoandaliwa hivi sasa zitazingatia mambo
muhimu ikiwemo kuwapa nafasi watanzania wenye mitaji midogo kuweza kuingia
kwenye biashara hiyo pamoja na kuweka adhabu kali dhidi ya wafanyabiashara
watakaohujumu biashara hiyo kwa makusudi.
Mkutano huo wa siku moja ulihudhuriwa pia na Katibu Mkuu wa
Wizara hiyo, Meja Jenerali Gaudence Milanzi, Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce
Nzuki, wakurugenzi, wakuu wa vitengo na wakuu wa taasisi zilizopo chini ya
wizara hiyo na waandhishi wa habari.
Oktoba 22 mwaka huu (2017) wakati akiongoza kikao cha wadau wa sekta ya
Maliasili na Utalii mjini Dodoma, Waziri Kigwangalla alitangaza
kufuta leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii zilizokuwa zianze mwezi
Januari, 2018 ili kupisha utarartibu mpya wa utoaji wa leseni hizo kwa njia ya
mnada ikiwa ni mkakati wa Serikali wa kuimarisha sekta hiyo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na
wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake
mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya kuimarisha sekta
hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha utaratibu mpya wa
utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya mnada. Kushoto
ni Naibu Katibu Mkuu,
Dk. Aloyce Nzuki.
Katibu Mkuu Wizara ya Maliasili na Utalii, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi (kushoto) akizungumza katika mkutano huo. Kulia ni Waziri wa
Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla.
Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Kampuni za Uwindaji wa Kitalii nchini,
Michael Mantheakis (kulia) akiwasilisha mapendekezo yake katika mkutano wa wadau
wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara ya
Maliasili na Utalii mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali
ya kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya kuanzisha
utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa kitalii kwa njia ya
mnada.
Mdau wa sekta ya uwindaji wa kitalii, Dk. Licky Abdallah
akizungumza katika mkutano huo.
Mdau wa sekta ya uwindaji wa kitalii ambaye pia ni mmilikia wa
kampuni ya uwindaji wa kitalii ya Bushman Hunting Safaris, Talal Abood
akiwasilisha mapendekezo yake katika mkutano huo.
Waziri wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akisikiliza kwa
makini mapendekezo ya wadau wa sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano
uliondaliwa na Wizara yake mjini Dodoma jana. Kushoto ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Meja Jenerali
Gaudence Milanzi.
Waziri
wa Maliasili na Utalii, Dk. Hamisi Kigwangalla akizungumza na wadau wa
sekta ya uwindaji wa kitalii katika mkutano uliondaliwa na Wizara yake
mjini Dodoma jana kwa ajili ya kujadili mikakati mbalimbali ya
kuimarisha sekta hiyo ikiwemo utekelezaji wa azma ya Serikali ya
kuanzisha utaratibu mpya wa utoaji wa leseni za vitalu vya uwindaji wa
kitalii kwa njia ya mnada. Kulia kwake ni Katibu Mkuu wa Wizara hiyo,
Mej. Jen. Gaudence Milanzi na Naibu Katibu Mkuu, Dk. Aloyce Nzuki
(kushoto kwake).
No comments:
Post a Comment