Askari polisi wa Kituo cha Babati mkoani Manyara, Boniface Masunga (32) amefariki dunia baada ya baiskeli aliyokuwa akiendesha wakati akielekea kazini kumgonga mtembea kwa miguu.
Baada ya kumgonga mtu huyo, askari huo aliangukia kichwa na kufariki dunia papo hapo.
Akizungumza, Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Manyara, Agostino Senga amesema tukio hilo limetokea jana katika barabara kuu ya Babati-Singida.
Amemtaja aliyegongwa kuwa ni Awadhi Ashraf (20) mkazi wa mjini Babati na kwamba, chanzo cha ajali hiyo ni Ashraf ambaye ni fundi ujenzi kuingia barabarani bila kuchukua tahadhari.
"Huyo fundi alikuwa anaingia kwenye barabara kuu ya lami bila kuchukua tahadhari, hivyo akagongwa na baiskeli aliyokuwa anaendesha polisi huyo," amesema Kamanda Senga.
Hata hivyo, baadhi ya mashuhuda wa ajali hiyo walishangazwa na ajali hiyo kwani hawajawahi kuona mtu akagongwa na baiskeli na mwendeshaji kufa.
Mkazi wa eneo la Sawe mjini Babati, Mariki John amesema tukio hilo ni la kushangaza kwani askari huyo japo alikuwa mdogo kiumri, lakini baiskeli imesababisha kifo chake.
Chanzo: Mwananchi
No comments:
Post a Comment