Advertisements

Tuesday, July 3, 2018

RAIS MAFUGULI: VIONGOZI NA WATENDAJI MSISUBIRI MAELEKEZO YA RAIS KUTIMIZA WAJIBU WENU


Na Immaculate Makilika-MAELEZO

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Magufuli amewataka viongozi na watendaji wa serikali kuuacha kusibiri maelekezo ya viongozi wakuu wa kitaifa katika kutekeleza majukumu katika maeneo yao ya kazi.

Rais Magufuli ameyasema hayo leo wakati wa hafla ya uapisho wa Viongozi na Watendaji 16 wa Serikali Ikulu jijini Dar es salaam, ambapo aliwataka viongozi na watendaji hao kutekeleza vyema wajibu wao katika kuwaletea maendeleo wananchi

“Nasikitika pale ambapo viongozi wa serikali kama vile kama mawaziri, naibu waziri hata wakurugenzi wanashindwa kutoa matamko na kutafutia ufumbuzi matatizo ya wananchi, ninataka mkafanye kazi katika maeneo yenu na si kusubiri mimi, Makamu wa Rais au Waziri Mkuu tutoe matamko” alisema Rais Magufuli.

Rais Magufuli alielezea sababu mbalimbali zilizosababisha kufanya mabadiliko hayo katika Baraza lake la Mawaziri, ambazo ni kutoridhishwa na utendaji kazi katika baadhi ya Wizara ikiwemo Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi ambapo aliutaja Mkataba baina ya Wizara hiyo na Kampuni ya Lugumi Enterprises Ltd kupitia mradi wa mashine za utambuzi wa alama za vidole katika vituo 108 vya Polisi uliogharibu Tsh. Bilioni 37.

Aidha Rais Magufuli pia aliieleza suala lingine ni pamoja na Mradi wa magari 777 yaliyoagizwa na Wizara hiyo kwa kutumia mkataba usio na maslahi na nchi, ambapo kati ya magari hayo, baadhi yake yalionekana kutumika kwa zaidi ya kilometa 4000, mengine kutoonesha mwaka ambao magari hayo yalitengenezwa.

“changamoto nyingine kuwa ni kuwepo kwa sare hewa za askari, upotevu wa mabilioni ya fedha, Jeshi la zima Moto na Uokoaji kutokuwa na vitendea kazi vya kutosha ambapo nimeelezwa jeshi hili lina magari 53 pekee na utoaji wa kiholela wa vibali vya wageni kufanyakazi nchini” alisema Rais Magufuli..

Aidha, akizungumzia kuhusu sekta ya maji, Rais Magufuli alimwagiza Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa kukamilisha miradi mbalimbali ya maji ili kutatua kero ya muda mrefu inayowakabili Watanzania hususani wa maeneo ya vijijini

Aliongeza kuwa hivi karibuni Serikali ilipokea kiasi cha Tsh trilioni 1.2 kutoka nchini India kwa ajili ya kugharamia shughuli za usambazaji wa maji katika mikoa 17 nchini, hivyo ni wajibu wa Wizara ya Maji na Umwagiliaji ijipange katika kuhakikisha kuwa miradi hiyo inatekelezwa bila kuwa na ucheleweshwaji.

Naye Waziri wa Maji na Umwagiliaji Prof. Makame Mbarawa alisisitiza kuwa Wizara yake itahakikisha kuwa itasimamia vyema wajibu na majukumu yake katika kuwahudumia Wananchi kwa kuwa kuna fedha za kutosha za zilizotengwa na Serikali katika kukamilisha miradi mbalimbali ya maji katika maeneo mbalimbali nchini.

Rais John Magufuli amewapisha viongozi mbalimbali wakiwemo Mawaziri, Naibu Waziri, Katibu Wakuu, Naibu Katibu Wakuu, Mwenyekiti, Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Makamu Mwenyekiti, Makamishana, pamoja na Katibu wa Tume ya Taifa ya Uchaguzi.

MWISHO

No comments: