Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa akimpokea Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea Mhe.Lee Nak-Yon siku alipowasili katika uwanja wa Julius Nyerere Dar es Salaam, Tanzania
Na. Immaculate Makilika- MAELEZO.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Kassim Majaliwa amesema serikali itaendelea kushirikiana na kuimarisha uhusiano wake wa kidiplomasia na Jamhuri ya Korea ili kuimarisha uchumi wa nchi hizo mbili.
Akizungumza na waandishi wa habari Ikulu Jijini Dar es salaam leo, Waziri Mkuu Majaliwa akiwa pamoja na Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Korea, Lee Nak-Yon amesema kuwa nchi hizo mbili zimetia saini mkataba wa mahusiano ya kidiplomasia ili kuimarisha uhusiano baina yao.
“Leo hii tumeshuhudia utiaji saini mkataba wa kidiplomasia wa kuondoa hitaji la visa kwa watumishi wa umma pamoja na wenye hati za kusafiria za kidiplomasia ikiwa ni sehemu ya kuimarisha uhusiano wetu” amesema Waziri Mkuu Majaliwa
Mkataba huo wa kihistoria ulitiwa saini na Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki, Balozi Dkt.Agustine Mahiga, pamoja na Makamu wa Kwanza wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Jamhuri ya Korea, Sung Nam.
Aidha, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa nchi hizo mbili zitaendelea kushirikiana ili kuimarisha maendeleo ya uchumi, utamaduni, teknolojia ya habari na mawasiliano pamoja na sekta ya utalii.
Ameitaja miradi mikubwa mitatu wanayotarajia kutekelezwa katika ushirikiano wan chi hizo kuwa ni ujenzi wa daraja la Busisi lililopo Kigoma lenye urefu wa mita 3200, ujenzi wa eneo lililobaki la barabara Cheya mkoani Tabora lenye urefu wa km 2.
Miradi mingine mikubwa ya ushirikiano huo ni pamoja na kuimarisha sekta ya afya kwa kujenga hospitali tano za rufaa katika kanda mbalimbali nchini.
Sambamba na hilo, Waziri Mkuu Majaliwa amesema kuwa Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea Lee Nak- Yon amefurahishwa na amani iliyopo nchini, na kumuahidi kuwa Tanzania itaendelea kuwaunga mkono katika mazungumzo yao ya amani huko Korea.
Waziri Mkuu huyo wa Jamhuri ya Korea, aliyewasili nchini jana anaendelea na ziara yake ya siku tatu, ambapo baadae leo atatembelea kituo cha taarifa cha NIDA kilichopo Kibaha,mkoni Pwani.
Mwisho.
No comments:
Post a Comment