ANGALIA LIVE NEWS

Tuesday, November 6, 2018

Wabunge wanne waapishwa, upinzani wasusia

By Habel Chidawali,Mwananchi

Dodoma. Wabunge wa Chadema na wa CUF upande wa katibu mkuu Maalim Seif wamesusia kushuhudia kiapo cha wabunge wanne wa CCM wote hawakuwepo bungeni leo wakati wabunge hao wa CCM walipokuwa wanaapishwa.

Mkutano wa Bunge umeanza leo asubuhi Jumanne Novemba 6, 2018 na kuongozwa na Spika Job Ndugai.

Mara baada ya kumaliza dua na wimbo wa Taifa, uliwadia wasaa wa kiapo kwa wabunge wanne waliokuwa upinzani ambao walijiuzulu na kuhamia CCM ambako waliibuka washindi.

Wakati wa shughuli hiyo ya kiapo, wabunge hao wa Chadema na CUF upande wa Maalim Seif hawakuwapo bungeni.

Aliyekuwa wa kwanza kuapishwa ni Julius Kalanga (Monduli), akafuatia Mwita Waitara (Ukonga), akaja Timotheo Mzava (Korogwe vijijini) aliyepita bila kupingwa akichukua nafasi ya marehemu Stephen Ngonyani ‘Majimarefu’ aliyefariki dunia.

Wa mwisho kuapishwa alikuwa Zuberi Kuchauka (Liwale) ambaye awali alikuwa mbunge kupitia CUF.

Shangwe zilitawala wakati wote ambapo wabunge wanawake wa CCM waliwasindikiza kwa makofi huku Mbunge wa Ulanga (CCM), Goodluck Mlinga akiwaongoza baadhi ya wabunge wa CCM, kukaa upande wa viti vya upinzani.

Mara baada ya kumaliza kuapishwa, wabunge hao wa Chadema na CUF walirejea bungeni.

Endelea kufuatilia Mwananchi

No comments: