Advertisements

Friday, March 22, 2019

MAREKANI YATOA VIFAA VYA KUPIMIA MAJI KWA BODI ZA MABONDE YA MAJI RUFIJI NA WAMI/RUVU


Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam
TANZANIA
Machi 21, 2019
TAARIFA KWA VYOMBO VYA HABARI

Marekani Yatoa Vifaa vya Kupimia Maji kwa Bodi za Mabonde ya Maji Rufiji na Wami / Ruvu

Machi 21, 2019, Serikali ya Marekani ilikabidhi vifaa vya kupimia maji kwa Bodi za Mabonde ya Maji Rufiji na Wami / Ruvu. Vifaa na huduma za ziada vitasaidia bodi kukusanya na kuchambua takwimu juu ya ubora na kiasi cha maji. Ufuatiliaji wa uboreshaji wa maji utasaidia wilaya kufanya maamuzi sahihi juu ya ugawaji wa maji ili kusimamia na kulinda rasilimali za maji kwa vizazi vijavyo.

Mbali na vifaa vya kupimia maji, Bodi za Maji zilipata boti/mashua, kompyuta, redio, vifaa vya kukadiria umbali, na vifaa vya mtandao kwa shughuli za zinazofanyika katika eneo la mradi na ofisini. Wafanyakazi watafundishwa namna ya kutumia vifaa vya kupimia maji ya mtoni.

Vifaa na huduma, vyenye thamani ya shilingi bilioni 2.3 za Kitanzania (dola 980,000 za Kimarekani), zilikabidhiwa na Shirika la WARIDI, na kufadhiliwa na Shirika la Marekani la Maendeleo ya Kimataifa (USAID). WARIDI inaendeleza usimamizi wa rasilimali maji na kuboresha upatikanaji wa huduma za maji.

"Kwa sababu maji yana jukumu muhimu katika kupunguza umasikini, kuboresha afya, na kuongeza uzalishaji, ni lazima yapewe kipaumbele cha juu serikalini na jumuiya ya wafadhili," alisema Andrew Karas, Kaimu Naibu Balozi wa Ubalozi wa Marekani.

Kupitia WARIDI, Serikali ya Marekani pia ilipatia Wizara ya Maji mwongozo wa matumizi ya kutathmini uwezo wa Jumuiya za Watumia Maji (WUAs), asasi za kijamii zinazohusika na usimamizi wa rasilimali za maji. WUA wana mamlaka ya kisheria ya kupata na kutumia vibali vya matumizi ya maji, kutatua migogoro ya matumizi ya maji, kulinda vyanzo vya maji, kuwakilisha maslahi ya watumiaji katika ngazi ya jamii, na kukusanya tozo za watumiaji wa maji kwa niaba ya Bodi za Mabonde za Maji. Kifaa kinaweza kutumika kwa ufuatiliaji wa mara kwa mara wa WUA na kutambua hatua za kuboresha utendaji. Ilianzishwa kupitia mchakato shirikishi unaohusisha wawakilishi kutoka Bodi ya Maji ya Bonde, Mamlaka za Serikali za Mitaa, Wizara ya Maji, na washauri wa ndani.

Ili kuomba taarifa zaidi, tafadhali piga simu Ofisi ya Habari ya Ubalozi wa Marekani Dar es Salaam kupitia: +255 22 229-4000 au barua pepe: DPO@state.gov.

WARIDI ni mradi wa miaka mitano unaofadhiliwa na USAID. WARIDI hufanya kazi kupitia mamlaka za serikali za kitaifa na za mitaa, Bodi mbili za Bonde, jamii, taasisi binafsi, na mashirika ya kiraia ili kuboresha utoaji wa usawa wa huduma zinazohusiana na maji na kuongeza usimamizi jumuishi wa maji kutoka bonde la maji hadi ngazi ya nyumbani. Mradi huo pia unafanya kazi ili kuboresha usafi wa mazingira, kuboresha maisha katika sekta za maji na usafi wa mazingira, na kukuza jamii imara wakati wa mabadiliko ya tabia nchi.


Soma zaidi kuhusu mradi huo hapa: https://www.usaid.gov/documents/1860/water-resources-integration-development-initiative-waridi.

No comments: