ANGALIA LIVE NEWS

Thursday, August 8, 2019

WAZIRI MKUU MSTAAFU MIZENGO PINDA AIHIMIZA BENKI YA CRDB KUENDELEA KUWEKEZA KWA WAJASIRIMALI WADOGO

Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akizungumza wakati akifungua semina ya siku moja kwa wajasiriamali wa Kilimo, Mifugo na Uvuvi wanaoshiriki maonyesho ya Nane Nane iliyodhaminiwa na Benki ya CRDB, yanayofanyika kitaifa, kwenye eneo la Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

Waziri Mkuu mstaafu, Mizengo Pinda amesema Benki ya CRDB ikiwa benki kinara katika uwezeshaji katika sekta mbalimbali za maendeleo nchini inapaswa kuelekeza nguvu zaidi kwa wajasirimali wadogo kwani kwa kufanya hivyo kutasaidia juhudi za Serikali ya awamu ya tano za kujenga uchumi wa kati.

"Kuna makundi ya wakulima wadogo, bodaboda, machinga  na wajasiriamali wengine wadogo ambao wamekuwa wakisahaulika kutokana na kutokuwa na dhamana na mikopo yao inatolewa kwa riba kubwa. Niwaombe Benki ya CRDB mtengeneze mpango mkakati mzuri wakuyahudumia makundi haya kwa unafuu na tuelekeze nguvu zetu huku kwani hawa ni wengi zaidi," alisema Mizengo Pinda.

Mheshimiwa Pinda amezungumza maneno hayo alipotembelea banda la Benki ya CRDB katika maonyesho ya kilimo, ufugaji na uvuvi yanayoendelea mkoani Simiyu.

Meneja Mahusiano wa Benki ya CRDB anayehusika na Mikopo ya Kilimo, Maregesi Shaaban alimhakikishia Waziri Mkuu mstaafu kuwa Benki hiyo imejipanga vilivyo kuhudumia wajasiriamali wadogo katika sekta zote kupitia huduma na bidhaa mbalimbali zinazotolewa na Benki hiyo.

"Kwa upande wa wakulima tumeanzisha akaunti za FahariKilimo ambayo ni mahsusi kabisa kwa ajili ya wakulima, akaunti hii hufunguliwa bure na hakuna gharama za uendeshaji tukilenga kumpa mkulima unafuu wa kupokea malipo pindi anapouza mazao yake" alisema Maregesi.

Maregesi alisema pia Benki hiyo ipo kwenye mchakato wa kuanzisha mikopo maalum kwa ajili ya wamachinga inayolenga kuwapa uwezo wa kukuza biashara yao kw kuwapa mitaji.

"Mheshimiwa Rais wetu mpendwa Dokta John Pombe Magufuli amefanya jitihada kubwa sana na za kupongezwa katika kurasimisha kundi hili la wajasiriamali, hivyo kuunga juhudi hizi Benki ya CRDB ipo katika mchakato wa kuingiza mikopo maalum kwa ajili ya wamachinga huku vitambulisho vyao vikitumika kuwatambulisha" alisema Maregesi.

Maregesi aliongezea kuwa Benki ya CRDB pia inatoa mikopo maalum ya kwa madereva na wamiliki wa Uber na mikopo ya pikipiki kwa madereva na wamiliki wa bodaboda.

Mapema kabla ya kutembelea banda la Benki ya CRDB, Waziri Mkuu mstaafu Mizengo Pinda alifungua semina maalum kwa wajasiriamali iliyoandaliwa na Taasisis ya Tafiti za Kiuchumi na Kijamii (ESRF) katika maonyesho hayo ya Nane nane yanayofanyika kitaifa mkoani Simiyu.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akimpongeza Meneja Mahusiano wa Benki ya CRDB anayehusika na masuala ya Mikopo ya Kilimo, Maregesi Shaaban kwa maelezo mazuri aliyoyapata juu huduma za Benki ya CRDB kwa wakulima, wakati alipotembelea Banda lao katika maonyesho ya Kilomo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayofanyika kitaifa, kwenye eneo la Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu. Kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Mara, Adam Malima na katikati ni Katibu Tawala wa Mkoa wa Simiyu, Jumanne Sagini.
Waziri Mkuu Mstaafu, Mizengo Pinda akifurahia jambo na baadhi ya wafanyakazi wa Benki ya CRDB, wakati alipotembelea Banda lao katika maonyesho ya Kilomo, Mifugo na Uvuvi (Nane Nane) yanayofanyika kitaifa, Nyakabindi, Bariadi mkoani Simiyu.

No comments: