Dar es Salaam. Kocha mkuu wa Yanga, Luc Eymael amesema kiungo mshambuliaji kutoka Ghana, Bernard Morrison atarejea katika timu hiyo jijini Dar es Salaam lakini kwa sharti la kuomba radhi wachezaji wenzake, benchi la ufundi, mashabiki na wanachama pamoja na viongozi na wadhamini wa Yanga.
Kocha huyo amesisitiza kwamba Morrison pamoja na mchezaji yoyote wa Yanga lazima ajue kwamba kila kitu anachokifanya ni kama timu na huku akionya kuwa hakuna mchezaji nyota asiyepata msaada uwanjani kutoka kwa wenzake.
Eymael amesema mchezaji huyo akishakamilisha masharti hayo ataunga na na wenzake kujiandaa kwa mechi dhidi ya Azam FC.
Alisema amezungumza na mchezaji huyo kwa dakika 50 na kusema kiungo huyo amebaini kosa lake ambalo anajutia huku akiwalaumu baadhi ya mawakala kwa tamaa na kushawishi vibaya wachezaji.
Eymael alisema Morrison amegundua njama hizo na kukiri kukosea na ataomba radhi mbale ya wachezaji ili kujiandaa na mechi hiyo ambayo itatoa picha halisi ya timu ipi itashika nafasi ya pili katika Ligi Kuu ya Tanzania Bara.
“Mimi sikuwepo, nimekutana mambo mengi ambayo si ya kawaida ndani ya klabu, kama kocha mkuu ni jukumu langu kutatua na kuiweka sawa timu.
Morisson ni moja ya tatizo hilo na hakuweza kusafiri kwenda Shinyanga, nilitaka kujua kuna tatizo gani, lakini muda haukutosha na kuamua kuondoka na (David) Molinga,” alisema Eymael. Alimtaka Morrison kujua kuwa hakuna mchezaji nyota duniani anayepata anayecheza mpira peke yake uwanjani bila msaada wa wengine, “hata ukiwachukua kina Cristiano Ronaldo wawili, Messi wawili na Sergio Ramos wawili wacheze dhidi ya wachezaji 11, lazima watafungwa. Timu ni mchango wa watu wengi.
“Najua Morrison kwa sasa ndiye mchezaji nyota wa Yanga, hilo halina ubishi, lakini lazima ajue kuwa umaarufu wake unatokana na msaada au ushirikiano na wachezaji wengine hilo ni jambo muhimu kujua, Yanga ni timu na wala si ya mchezaji mmoja pekee.”
Shangwe bungeni
Jana, wachezaji na viongozi wa Yanga walikaribishwa kwa shangwe katika Ukumbi wa Bunge Jijini Dodoma.
Spika wa Bunge, Job Ndugai ambaye mara kadhaa amekuwa akiweka wazi mapenzi yake kwa Simba alikiri kwamba bao 1-0 Yanga ililoshinda dhidi ya Simba katika mchezo wa mwisho limebaki kwenye vichwa vya mashabiki.
Katika ukumbi huo Spika alimtaka Morrison asimame asalimie wabunge lakini hakuwepo. Yanga itacheza na JKT Tanzania kesho kwenye Uwanja wa Jamhuri, Dodoma.
No comments:
Post a Comment